Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Trump afungua mlango wa mazungumzo na Iran

Iran bado haijatoa jibu kwa matamshi ya Trump. Trump amekuwa akisisitiza mara kwa mara kwamba mwisho wa vita kupitia mazungumzo uko karibu kufikiwa, lakini mashambulizi ya kulipizana yamekuwa yakirejea tena na tena.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Massive Attack watoa tamko baada ya Singapore kupiga marufuku onyesho lao kuhusu Palestina

    Kundi la Massive Attack limesema lilishangazwa na kukatishwa tamaa na jinsi mamlaka za Singapore zilivyolichukulia baada ya kuonyesha uungaji mkono kwa Palestina wakati wa onyesho katika jiji la taifa hilo.

    Kundi hilo liliandika kwenye Instagram siku ya Jumapili kwamba wanachama wake "walizuiliwa na polisi, kutengwa na kuhojiwa kivyao," huku wengine wakikabiliwa na upekuzi wa vyumba vyao vya hoteli na kunyang'anywa pasipoti kwa muda.

    Wanachama wawili wa kundi hilo walinyanyua bendera ya Palestina wakati wa onyesho lao la tarehe 29 Julai na kupaza sauti wakisema "Palestina iwe huru" (free Palestine) pamoja na baadhi ya watu waliokuwa wakitazama onyesho hilo.

    Singapore, ambayo ina sheria kali kuhusu hotuba za hadhara na mikusanyiko, baadaye ilitangaza kuwa imepiga marufuku kundi la Massive Attack kurejea nchini humo kwa muda usiojulikana.

    Msemaji wa polisi aliambia BBC siku ya Ijumaa kuwa wanachama hao wawili wa kundi hilo hawangeruhusiwa kuingia tena Singapore na walipigwa marufuku kufanya maonyesho huko.

    Robert Del Naja na Grant Marshall "waliopewa maonyo makali" kuhusiana na madai ya makosa chini ya sheria mbili zinazozuia kuonyeshwa hadharani kwa bendera za kigeni na kudhibiti kauli za kisiasa katika hafla za umma.

    Massive Attack ilisema kuwa kabla ya onyesho na tena mwishoni mwake, "sehemu kubwa ya hadhira ilianza kwa hiari yao wenyewe kupaza sauti wakisema 'Palestina iwe huru', wakijua vyema lakini bila kuogopa kwamba kitendo hicho cha hiari kingeweza kukiuka sheria za udhibiti wa maoni za serikali yao".

    Kundi hilo halikuzungumzia moja kwa moja marufuku hiyo, lakini lilielezea hali hiyo kama "tukio la ajabu lisilo la kawaida" na kusema kuwa "hawakudhani kwamba kitendo cha kunyanyua bendera ya taifa huru linalotambuliwa na nchi 157 kingeweza kukiuka sheria yoyote".Waliongeza kusema: "Anatoa onyesho linalohitaji nguvu nyingi za kimwili na ustadi wa hali ya juu wa kimichezo. Anafanya maonyesho hayo kwa kiwango cha juu sana, kwa mafanikio na akiwa na afya njema, usiku baada ya usiku."

    Onyesho la mwisho la ziara hiyo limepangwa kufanyika tarehe 1 Septemba jijini London.

  2. Ariana Grande kusitisha kwa muda shughuli zake za hadharani kutokana na kufuatiliwa mara kwa mara

    Ariana Grande anatarajiwa kujiondoa katika shughuli zinazomfanya aonekane hadharani na hatahusika tena katika tamasha la muziki litakalofanyika London baada ya kuhitimisha ziara yake ya *Eternal Sunshine* mwezi ujao.

    Mwakilishi wa mwimbaji huyo kutoka Marekani, mwenye umri wa miaka 33, aliambia jarida la *People* kuwa "atapunguza kujionyesha hadharani" mara ziara hiyo itakapomalizika, kufuatia kuonekana kwake kusababisha "uchunguzi na mjadala usioisha wa umma".

    Kampuni inayoandaa toleo jipya la tamasha la muziki la Stephen Sondheim, *Sunday in the Park with George*—ambalo linatarajiwa kuonyeshwa katika ukumbi wa Barbican mwaka wa 2027—ilithibitisha kuwa hatahusika tena katika tamasha hilo na kwamba wanaelewa na kuunga mkono uamuzi wake kikamilifu.

    Muonekano wa mwili na afya ya Grande vimekuwa mada ya uvumi katika miaka ya hivi karibuni.

    Uvumi huo umeongezeka tangu kutolewa kwa albamu yake mpya, *Petal*, siku mbili zilizopita na kuonekana kwake katika vifaa vya kuitangaza albamu hiyo.

    Mwakilishi wake alisisitiza kwa jarida la *People* kuwa Grande anatarajia kuhitimisha ziara yake "kwa mafanikio makubwa, akiwa na afya njema na furaha, na kisha kuchukua mapumziko yanayostahili kutokana na kazi na shughuli zinazomfanya aonekane hadharani, ambazo zimesababisha uchunguzi na mjadala usioisha wa umma".

  3. Mwanamke afanyiwa upasuaji wa mfuko wa uzazi ili kumtibu mtoto aliye na utumbo nje ya mwili

    Madaktari wametumia upasuaji wa aina yake na wa kipekee kwa mtoto ambaye bado hajazaliwa ili kurekebisha kasoro ya kuzaliwa akiwa bado tumboni mwa mama yake.

    Mama yake, Maisie Savage, kutoka London, alifanyiwa upasuaji na madaktari nchini Marekani akiwa na ujauzito wa wiki 26.

    Mtoto Theo, ambaye sasa ana umri wa miezi mitano na anaendelea vizuri, alikuwa na tatizo la *gastroschisis*—hali ambapo kitovu hakikutengenezwa vizuri, na kusababisha utumbo kukua nje ya mwili.

    Madaktari walifungua sehemu ya tumbo la uzazi la mama yake na kisha kurudisha viungo vya mtoto ndani ya tumbo lake kwa upole kwa kutumia mbinu ya upasuaji wa tundu dogo (keyhole surgery).

    Yeye alikuwa mtoto wa tatu duniani kufaidika na jaribio hili la kimatibabu ambalo ni la kwanza la aina yake.

  4. Chelsea yamsajili kiungo wa Strasbourg, Barco

    Chelsea imekamilisha usajili wa kiungo wa Strasbourg, Valentin Barco, kwa mkataba wa miaka saba.

    Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 anakuwa mchezaji wa sita kusajiliwa na Chelsea katika dirisha hili la majira ya joto, kufuatia kuwasili kwa Morgan Rogers, Danny Welbeck, Emmanuel Emegha, Maxence Lacroix na Marco Palestra.

    Kiungo huyo ataungana na kikosi cha Chelsea katika sehemu iliyosalia ya ziara yao ya maandalizi ya msimu, huku timu hiyo ikitarajiwa kucheza dhidi ya klabu ya Italia, Juventus, jijini Hong Kong mnamo tarehe 5 Agosti.

    Chelsea haikuweka wazi kiasi cha ada ya uhamisho.

    Barco aliwahi kuichezea Argentina mara moja katika Kombe la Dunia la 2026—ambapo timu hiyo ilimaliza ya pili nyuma ya Uhispania—na alipigwa kofi na Jude Bellingham baada ya ushindi wa nusu fainali dhidi ya Uingereza.

    Akiwa ameibukia katika akademi ya Boca Juniors, Barco alijiunga na Brighton mwaka 2024 kwa ada ya pauni milioni 7.9.

    Hata hivyo, alikaa mwaka mmoja tu katika eneo la pwani ya kusini na kujiunga na Strasbourg katika majira ya joto yaliyofuata, baada ya kipindi cha mafanikio cha mkopo.

    Anakuwa mchezaji wa pili katika majira haya ya joto kujiunga na Chelsea akitokea Strasbourg; klabu zote mbili zinamilikiwa na Todd Boehly pamoja na Clearlake Capital.

    Huu ni usajili wa 13 kufanyika kati ya klabu hizo mbili tangu kuanza kwa msimu uliopita.

  5. Uganda yazindua sanamu ya kaka yake Waziri Mkuu wa Israel aliyefariki katika operesheni ya uokoaji ya Entebbe

    Uganda imezindua sanamu ya Yonatan Netanyahu, kaka mkubwa wa Waziri Mkuu wa Israel, ambaye aliuawa wakati wa operesheni ya kuwaokoa mateka huko Entebbe miaka 50 iliyopita.

    Mkuu wa jeshi la Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, alisema kuwa mnara huo unaenzi ushujaa wake na moyo wake wa kujitolea.

    Netanyahu alikuwa askari pekee wa Israel aliyeuawa katika operesheni hiyo—ambayo ilifanikiwa kuwaokoa zaidi ya mateka 100—baada ya Wapalestina wawili na Wajerumani wawili kuteka ndege ya shirika la Air France iliyokuwa imetoka Tel Aviv na kuielekeza kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Uganda.

    Kainerugaba alielezea operesheni hiyo kama "moja ya matukio muhimu zaidi katika historia ya kisasa" na akazungumzia uhusiano wa karibu uliopo sasa kati ya nchi hizo mbili kama "safari ya kipekee".

    Sanamu hiyo ya Netanyahu, inayomwonyesha akipiga hatua mbele huku akiwa ameshika bunduki aina ya 'machine gun', imesimikwa nje ya jengo la zamani la uwanja wa ndege ambapo tukio hilo la uokoaji lilifanyika.

    Wakati wa operesheni hiyo, mateka watatu—Jean-Jacques Mimouni, Pasco Cohen na Ida Borochovitch—pia walipoteza maisha, huku Dora Bloch akiuawa baadaye akiwa anapatiwa matibabu katika hospitali moja jijini Kampala.

    "Kumbukumbu zao ziendelee kuhamasisha vizazi vijavyo katika harakati za kutafuta amani, haki na utu wa binadamu," alisema mkuu huyo wa jeshi.

    Watekaji nyara hao na washirika wao watatu waliojiunga nao nchini Uganda pia waliuawa, pamoja na angalau askari 45 wa Uganda, katika mapigano dhidi ya vikosi vya Israel.

  6. Wafanyakazi wawili wafariki baada ya helikopta za kuzima moto kugongana nchini Ugiriki

    Wafanyakazi wawili wamefariki dunia baada ya helikopta mbili kugongana angani nchini Ugiriki wakati zikishiriki kuzima moto wa nyika.

    Waliofariki ni rubani wa Denmark na afisa wa mawasiliano wa idara ya zimamoto ya Ugiriki. Rubani raia wa Uingereza na mratibu mwingine raia wa Ugiriki waliokuwa kwenye helikopta ya pili walinusurika.

    Video ya tukio hilo, lililotokea takribani umbali 65 (mail42) magharibi mwa mji mkuu wa Athens, inaonesha helikopta aina ya Bell ikigonga mbawa za helikopta nyingine, ambayo ilishika moto. Helikopta nyingine ilitua kwa dharura.

    Moto wa nchi umezuka nchini Ugiriki wiki hii na kusababisha uhamishaji wa watu kwa wingi. Nchi nyingine za Ulaya pia zimekumbwa na moto mkubwa na hatari wakati wa vipindi virefu vya joto kali.

    Kwa mujibu wa Idara ya Zimamoto ya Ugiriki, helikopta hizo aina mbili za Bell—ambazo zimekodishwa kutoka kampuni ya Australia ya McDermott Aviation—ziligongana Jumapili wakati zikishiriki juhudi za kuzima moto mkubwa uliokuwa ukiwaka katika mpaka wa Attica na Boeotia.

    Wafanyakazi wa helikopta moja waliokolewa wakiwa hai, huku wa helikopta ya pili wakipatikana wakiwa hawajitambui na baadaye kuthibitishwa kufariki dunia.

    Waziri Mkuu wa Ugiriki, Kyriakos Mitsotakis, alielezea "masikitiko yake makubwa" kufuatia ajali hiyo.

    Katika ujumbe kwenye mtandao wa X, alisema kupotea kwa mratibu huyo raia wa Ugiriki na rubani raia wa Denmark "kunatujaza sote huzuni." Pia alitoa rambirambi kwa familia zao.

  7. WAFCON 2026: Mali yaibuka na ushindi wa kwanza, Cameroon yakaribia kutinga hatua ya mtoano

    Mali Yaibuka na Ushindi wa Kwanza, Cameroon Yakaribia Kutinga Hatua ya Mtoano AFCON ya Wanawake

    Katika mashindano ya soka kuwania kombe la taifa bingwa barani Afrika kwa kina dada yanayoendelea nchini Morocco, Mali ilijinyakulia alama tatu muhimu pale ilipoilaza Cape Verde magoli matatu kwa mawili.

    Ushindi huo ndio uliokuwa wa kwanza kwa mali katika mashindano hayo.

    Katika mechi nyingine Cameroon, iliilaza Ghana bao moja kwa bila.

    Cameeron sasa ina alama sita baada ya kushinda mechi yao ya kwanza dhidi ya Mali.

    Cameroon sasa inahitaji sare au ushindi katika mechi yao ya mwisho dhidi ya Cape Verde ili kufuzu kwa hatua ya muondoano.

    Hii leo wenyeji Morocco wanatoa na jasho na Senegal huku Kenya ikipepetana na Algeria.

    Pia unaweza kusoma:

  8. Mahakama yaamuru kusitishwa kwa mpango wa kutumia mamba kuzunguka gereza la Wapalestina nchini Israel

    Mahakama ya Israeli imetoa amri ya muda ya kusimamisha mpango tata wa kutumia mamba wa mto Nile kuzunguka gereza linalowashikilia wafungwa wa Kipalestina hadi taarifa zaidi itakapotolewa, baada ya kundi la haki za wanyama kuwasilisha ombi la dharura la kuzuia mpango huo.

    Kulingana na mpango huo, ambao unaungwa mkono na Waziri wa Usalama wa Taifa wa Israeli Itamar Ben-Giver, mtaro ulipaswa kuchimbwa kuzunguka moja ya malango ya usalama ya gereza la Katziut katika Jangwa la Negev na mamba wa Nile wangewekwa hapo.

    Maafisa wa Israeli wanasema lengo la hatua hii ni kuongeza hatua za usalama na kuzuia majaribio yoyote ya wafungwa kutoroka.

    Uchimbaji wa mtaro ulianza kama mwezi mmoja uliopita, lakini ripoti zinaonyesha kuwa hakuna mamba ambaye amehamishwa hadi eneo hilo. Kulingana na hati zilizochapishwa, mtaro huo utakuwa na urefu wa takriban mita 170 na unakusudiwa kuzunguka sehemu ya gereza ambalo wafungwa wa Kipalestina wanazuiliwa.

    Mpango huo umekabiliwa na ukosoaji mkubwa kutoka kwa makundi ya haki za binadamu na haki za wanyama tangu kutangazwa kwake.

    Mashirika ya haki za wanyama yamesema katika kesi yao kwamba kuwatumia wanyama wa porini kama walinzi wa usalama kunakiuka sheria za ustawi wa wanyama na ulinzi wa wanyamapori na kuwaweka katika hali zisizofaa.

  9. Watu wenye silaha waua 12, wateka wanawake na watoto kaskazini mwa Nigeria

    Watu waliojihami kwa silaha wamewaua takribani watu 12 na kuwateka wanawake na watoto wakati waliposhambulia kijiji kimoja katika jimbo la Sokoto kaskazini magharibi mwa Nigeria, walioshuhudia tukio hilo wanasema.

    Jamaa sita wa familia moja walifariki baada ya washambuliaji kuchoma nyumba yao. Mmoja wa wakaazi aliiambia shirika la Habari la Reuters.

    Washambuliaji waliokuwa na silaha waliingia katika kijiji cha Lajinge mwendo wa saa tano usiku siku ya Jumamosi na kuwashambulia wakazi hadi saa tisa usiku kuamkia Jumapili, wakazi walisema.

    Eneo hilo limeshuhudia mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa magenge yenye silaha kali, wanaojulikana kama majambazi, ambao huvamia vijiji, kuwateka nyara wakaazi kwa lengo la kulipwa kikombozi na kuiba mifugo.

    "Waliua takriban watu 12, wakajeruhi wengine wanne, waliwateka nyara wanawake na watoto baada ya kuiba mifugo mingi," mkazi Auwal Hassan aliambia Reuters kwa njia ya simu.

    Polisi walikuwa wakichunguza na watatoa taarifa baadaye, msemaji wa kikosi cha Sokoto Ahmed Rufai alisema.

    Shambulio hilo linakuja wiki moja baada ya majambazi kuwaua wakulima wasiopungua 24 katika jimbo jirani la Zamfara.

    Soma Zaidi Hapa:

  10. Trump afungua mlango wa mazungumzo na Iran

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema mazungumzo mapya na Iran yataanza leo Jumatatu, baada ya kusitisha kile alichosema kingekuwa mashambulizi "makubwa" dhidi ya taifa hilo.

    "Walijua ukubwa wa shambulio hilo kwa sababu walilikisia jinsi litakavyokuwa," aliwaambia waandishi wa habari akiwa ndani ya ndege ya Air Force One siku ya Jumapili. "Tunazungumza nao kupitia majadiliano. Mazungumzo hayo yataanza kesho alasiri," yaani leo.

    Katika mtandao wa Truth Social, rais wa Marekani alisema ameombwa na Iran na nchi nyingine za Mashariki ya Kati "kusitisha kwa muda," shambulio lolote akidai kuwa misingi ya makubaliano ilikuwa tayari imeafikiwa.

    Iran bado haijatoa jibu kwa matamshi ya Trump. Rais huyo wa Marekani amekuwa akisisitiza mara kwa mara kwamba mwisho wa vita kupitia mazungumzo uko karibu kufikiwa, lakini mashambulizi ya kulipizana yameendelea kurejelewa.

    Akizungumza akiwa ndani ya ndege ya Air Force One, Trump alikataa kuweka muda maalum wa kufikiwa kwa makubaliano na Tehran, akisema: “Tutaona tu hali itakavyokuwa. Tuko tayari kuchukua hatua wakati wowote tutakapotaka... Sitafuti kuua watu.”

    Soma Zaidi:

  11. Hujambo na Karibu katika matangazo yetu mubashara, 03//08/2026.