Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Trump atishia Iran usitishaji mapigano "umefutiliwa mbali"; Iran yaonya kuwa "watajibu bila uwoga"

Trump alipokuwa akiuita uongozi wa Iran kuwa "wakihuni" na "unaougua", Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema: "Hatulipizi matusi kwa matusi, bali kwa vitendo."

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Lizzy Masinga & Asha Juma

  1. Kurejea kwa mapigano kikamilifu kutakuwa na "madhara makubwa" - UN

    Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa atoa wito kwa Iran na Marekani kurejea kwenye meza ya mazungumzo

    Antonio Guterres amesema katika taarifa kwamba kurejea kwa mapigano kikamilifu kati ya nchi hizo mbili kutakuwa na "madhara makubwa" kwa watu wa eneo hilo, amani na usalama wa kimataifa, pamoja na uchumi wa dunia.

    Pia ametoa wito kwa pande zote kuchukua hatua za haraka za kupunguza mvutano.

  2. Habari za hivi punde, "Hatulipizi matusi kwa matusi, bali kwa vitendo" – Iran

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X kuwa,

    "Kuliita taifa la Iran, ambalo ni la kistaarabu na jasiri, kwa lugha ya kudhalilisha hakupunguzi ukuu wake."

    "Wairani wanajulikana kwa ustaarabu, utamaduni, na maadili yao thabiti."

    "Hatulipizi matusi kwa matusi, bali kwa vitendo; bila uwoga na kwa ujasiri mkubwa."

  3. Wanajeshi wanane wa Iran wauawa katika mashambulizi ya Marekani - jeshi la Iran

    Wanajeshi wanane wa Iran wameuawa katika mashambulizi yaliyofanywa na Marekani usiku kucha, kwa mujibu wa taarifa inayodaiwa kutolewa na jeshi la Iran.

    Taarifa hiyo, ambayo imesambazwa na vyombo kadhaa vya habari vya Iran, imesema wanajeshi hao walikuwa wanahudumu katika jeshi la anga na jeshi la wanamaji.

    Aidha, imeeleza kuwa wanajeshi hao walikuwa wamepangiwa kufanya kazi katika miji ya Bandar Abbas na Bushehr.

  4. Vyombo vya habari vya Iran vyajibu kauli ya Trump

    Press TV, kituo cha habari cha Kiingereza kinachomilikiwa na shirika la utangazaji la serikali ya Iran (IRIB), kimenukuu chanzo cha usalama kikisema kuwa Iran itafunga Mlango-Bahari wa Hormuz kwa shughuli zote za usafiri wa majini iwapo nchi hiyo itashambuliwa.

    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, chanzo hicho pia kimesema Iran italenga takriban maeneo mawili kwa kila eneo moja linalolengwa la Iran, kikiongeza kuwa: "Iran haitofautishi kati ya Marekani na washirika wake katika eneo hilo."

    Wakati huo huo, shirika la habari la Tasnim, linalohusishwa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC), limesema kuwa "kufutiliwa mbali" kwa makubaliano ya usitishaji mapigano ya Islamabad "kumetangazwa rasmi" na Trump.

    Chombo hicho cha habari kiliongeza kuwa Iran sasa ina "mamlaka yaliyo wazi zaidi" ya kukabiliana na Marekani, Israel na washirika wao katika eneo hilo na duniani.

    Awali, mshauri mwandamizi wa Kiongozi Mkuu wa Iran alionya kuwa hali itakuwa "mbaya" katika eneo la Mashariki ya Kati kufuatia matamshi ya Trump.

    Soma Zaidi:

  5. Trump atishia kuzingira tena maji ya Iran baharini

    Rais Donald Trump amesema Marekani inazingatia kurejesha mzingiro wa majini kwenye bandari za Iran, hatua ambayo ilisitishwa kama sehemu ya makubaliano ya awali ya kumaliza vita tarehe 17 Juni.

    "Tunaweza kuurejesha mzingiro huo," Trump alisema. "Utawahusu Iran pekee; nchi nyingine zinaweza kuendelea kufanya shughuli zao kama kawaida."

    Trump pia alisema Iran inaweza kujaribu kutega mabomu ya baharini ikiwa itapata fursa, lakini akaongeza kuwa Marekani ina meli maalumu za kuondoa mabomu hayo baharini.

    Aidha, alisema kuwa nchi wanachama wa NATO zimejitolea, wakati wa mkutano wa kilele uliofanyika leo, kutuma meli za kuondoa mabomu ya baharini katika eneo hilo.

    Soma Zaidi:

  6. Tutaishambulia Iran tena leo usiku - Trump

    Rais wa Marekani Donald Trump alipoulizwa na wanahabari akihudhuria mkutano wa Nato, kuhusu Iran alijibu kuwa

    "Tuliwashambulia sana jana usiku," na kuongezea kuwa "tutawashambulia tena kwa nguvu kubwa usiku wa leo"

    Trump ameonya kuwa mashambulizi ya sasa yanaweza kulenga miundombinu muhimu nchini humo ikiwemo madaraja na kampuni za kutoa chumvi kwa maji ya matumizi.

    Rais huyo pia amesema Marekani inaweza kuchukua udhibiti wa Kisiwa cha Kharg ambacho ni kituo kikubwa cha kusafirisha mafuta kilichopo kwenye pwani ya Iran na kusema kuwa hakuna kitu ambacho Tehran inaweza kufanya kuzuia hilo.

    Rais huyo alisisitiza kuwa "huenda kukawa na shambulio kubwa" usiku wa leo nchini Iran.

    Awali Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth, alikuwa ametoa onyo la shambulio kufanyika maeneo ya ndani sana nchini Iran.

    Soma pia:

  7. Maelfu ya watu wajumuika mjini Najaf, nchini Iraq kumuaga Khamenei

    Umati mkubwa wa waombolezaji ulikusanyika hii leo kwa ajili ya kumuaga aliyekuwa kiongozi wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei katika mji wa Najaf nchini Iraq.

    Jeneza la kiongozi huyo wa zamani wa Iran liliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Najaf jana jioni huku Waziri Mkuu wa Iraq Ali Zaidi pamoja na maafisa kadhaa wakuu wa serikali na viongozi wa kidini wakihudhuria hafla rasmi ya kupokea jeneza hilo.

    Iraq ilitangaza leo Jumatano kuwa siku ya mapumziko ya kitaifa.

    Ibada ya mazishi mjini Najaf ilianza saa kumi na mbili asubuhi saa za eneo hilo.

    Rais wa Iran Masoud Pezeshkian na Mustafa Khamenei, mmoja wa wana wa kiongozi huyo wa Iran, pia walihudhuria hafla hiyo.

    Mazishi ya mwisho ya Khamenei yatafanyika hapo kesho eneo analotoka la Mashhad, kaskazini mashariki mwa Iran.

    Msafara wa mazishi mjini Najaf umefanyika wakati mvutano kati ya Marekani na Iran unazidi kutokota kuhusu mlango bahari wa Hormuz.

    Awali, Marekani ilikuwa imetangaza kuwa ilikuwa imeipa Iran wiki moja kufanya shughuli hiyo ya mazishi.

    Soma Pia:

  8. Trump: Makubaliano ya kusitisha mapigano na Iran yamefutiliwa mbali

    Rais wa Marekani Donald Trump akiwa pembeni mwa mkutano wa NATO mjini Ankara, amesema kwamba makubaliano ya kusitisha mapigano kati yao na Iran yamefutiliwa mbali, na kuongezea kuwa mazungumzo na Iran ni “kupoteza muda.”

    Trump, alipoulizwa na waandishi wa habari kama makubaliano ya kusitisha mapigano na Iran yamekwisha, alijibu, “Nadhani yamekwisha.”

    Trump ameyasema hayo baada ya Iran na Marekani kushambuliana, huku pande zote mbili zikilaumiana kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano.

    Soma pia:

  9. Shirika la UN linawataka wahudumu wa meli kusitisha safari katika Mlango Bahari wa Hormuz

    Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Bahari (IMO), linalosimamia usafirishaji wa kimataifa wa njia za bahari, amelaani mashambulizi dhidi ya meli zinazopitia Mlango Bahari wa Hormuz, kwa muda wa siku mbili zilizopita.

    IMO imewataka nahodha wa meli kutotumia njia hiyo ya bahari.

    “Mashambulizi haya yamewaweka tena mabaharia wasio na hatia katika hatari kubwa,” amesema Katibu Mkuu wa IMO, Arsenio Dominguez.

    Safari za meli, zikiwemo meli za kubeba mafuta zilikuwa zimeongezeka baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Marekani na Iran.

    Aidha kampuni ya meli ya Bahri imethibitisha kuwa moja ya meli zake, Wedyan, ilishambuliwa wakati ikipita katika Mlango bahari wa Hormuz siku ya Jumanne.

    Kampuni ya Bahri imesema shehena ya meli hiyo iko salama pamoja na wafanyikazi wake.

    Awali, BBC Verify ilithibitisha kuwa Wedyan ilikuwa miongoni mwa meli tatu zilizolengwa katika shambulio hilo.

    Pia unaweza kusoma:

  10. Rais wa Iran aikashifu Marekani kwa kuingilia sheria za Kombe la Dunia

    Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, ameikosoa serikali ya Marekani kama mwenyeji wa Kombe la Dunia, akiishutumu kwa “kupindisha sheria, kuwanyanyasa washindani wenza, kuwawekea vikwazo na udanganyifu.”

    Hii inajiri baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kusema aliomba FIFA irejelee upya adhabu ya kusimamishwa kwa mechi moja kwa mchezaji wa soka wa Marekani Folarin Balogun, ambapo baadaye FIFA ilimruhusu kucheza katika mechi inayofuata.

    Ushiriki wa Iran katika Kombe la Dunia ulikumbwa na vikwazo kutokana na matatizo ya visa na masuala ya usafiri.

    Soma Zaidi:

  11. Qatar yaishutumu Iran kwa "ukiukaji wa wazi" wa sheria za kimataifa

    Qatar imelaani mashambulizi ya Iran dhidi ya Bahrain na Kuwait, ikiyataja kuwa hayana uhalali.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar imesema mashambulizi hayo ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na wa mamlaka ya Bahrain na Kuwait.

    Qatar pia imesisitiza umuhimu wa mazungumzo na diplomasia, kupunguza mvutano, na kuendeleza yaliyofikiwa kupitia makubaliano ya maelewano.

    Iran imesema inalenga maeneo ya kijeshi ya Marekani yaliyoko Bahrain na Kuwait, kufuatia mashambulizi ya Marekani dhidi yake yaliyofanyika usiku.

  12. Video: Tazama Marekani ilivyoishambulia Iran

  13. Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa asaini sheria inayoongeza muda wa urais wake

    Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa amesaini kuwa sheria muswada unaoongeza muda wake wa kuhudumu madarakani kwa miaka miwili zaidi, hadi mwaka 2030, msemaji wa serikali Nick Mangwana amesema Jumanne.

    Mwezi uliopita, mabunge yote mawili ya Zimbabwe yaliidhinisha muswada huo.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X, Mangwana alisema: "Imesainiwa, imethibitishwa na sasa ni sheria," akiambatanisha nakala ya sheria hiyo.

    Sheria hiyo pia ina kipengele kinachoruhusu rais kuchaguliwa na Bunge badala ya kuchaguliwa moja kwa moja na wananchi kupitia kura.

    Dalili kwamba Mnangagwa, mwenye umri wa miaka 83, alitaka kuendelea kubaki madarakani baada ya kumalizika kwa muhula wake wa pili mwaka 2028 zilianza kujitokeza takribani miaka miwili iliyopita.

    Wafuasi wake walianza kuimba kaulimbiu katika mikutano ya chama tawala ZANU–PF wakimtaka apewe muda zaidi ili akamilishe ajenda yake ya maendeleo.

    Mwaka uliopita, chama cha ZANU–PF kilipitisha azimio la kufanya marekebisho ya katiba ili kuongeza muda wa mihula ya urais. Pendekezo hilo lilipata idhini ya Baraza la Mawaziri mwezi Februari.

    Unaweza kusoma;

  14. Washirika wa NATO watangaza pauni bilioni 37 kwa mradi mpya wa makombora

    Mataifa kumi na mawili, yakiwemo Uingereza, yanatarajiwa kutumia zaidi ya pauni bilioni 37 sawa na dola bilioni 50 za Marekani katika kipindi cha miaka 10 ijayo kutengeneza kombora jipya la masafa marefu kwa ajili ya kuimarisha ulinzi wa Ulaya.

    Mradi huo unaojulikana kama Deep Precision Strike umetangazwa rasmi na Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza na unatarajiwa kujadiliwa baadaye Jumatano katika mkutano wa NATO unaofanyika mjini Ankara, Uturuki.

    Waziri Mkuu wa Uingereza, Sir Keir Starmer, anahudhuria mkutano huo ambao unatarajiwa kuwa wa mwisho kwake akiwa waziri mkuu.

    Anatarajiwa kukosolewa na Rais wa Marekani, Donald Trump, kwa kushindwa kuweka mpango wa kufikia lengo la kutumia asilimia 3.5 ya Pato la Taifa (GDP) kwa matumizi ya ulinzi ifikapo mwaka 2035, ambalo lilikubaliwa na karibu wanachama wote wa NATO mwaka uliopita.

    Hata hivyo, Jumatano Sir Keir ataongoza mkutano wa viongozi wapatao 12 kujadili mpango huo mpya wa utengenezaji wa kombora.

    Kombora la Deep Precision Strike linaelezwa kuwa miongoni mwa silaha za kisasa zaidi za NATO, likiwa na uwezo wa kushambulia malengo yaliyo umbali wa karibu kilomita 300 kwa usahihi mkubwa, huku uwezo wake ukitarajiwa kuongezwa hadi kufikia kilomita 2,000.

    Sir Keir alisema mpango huo unaoongozwa na Uingereza "utasaidia kuwaunganisha washirika wa Ulaya na kuimarisha usalama wa NATO kwa miaka mingi ijayo."

    Hata hivyo, kama ilivyo kwa miradi mingine mingi ya kijeshi inayopangwa, kombora la Deep Precision Strike halitarajiwi kuwa tayari kutumika hadi katika miaka ya 2030.

    Mnamo Juni, Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth, alitangaza mapitio ya miezi sita kuhusu uwepo wa majeshi ya Marekani barani Ulaya.

  15. Samatta astaafu kucheza timu ya taifa ya Tanzania

    Nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania Mbwana Samatta ametangaza kustaafu rasmi kuichezea timu hiyo baada ya kuitumikia kwa miaka 15, miaka 10 kati ya hiyo akiwa nahodha.

    Kupitia chapisho lake katika ukurasa wa Istagram, Samatta amewashukuru wote alioshirikiana nao wakiwemo wachezaji na mamlaka za soka za nchi na serikali katika nyakati za furaha na huzuni.

    ''Ulikuwa wakati mzuri na wa kipekee katika maisha yangu kuwa mchezaji wa timu ya taifa kwa takribani miaka 15, ninajisikia fahari kusema ninashukuru kwa nafasi hii'' Aliandika Samatta.

    Amesema kuwa miaka 10 ya kuwaongoza wenzake akiwa nahodha imekuwa alama kubwa katika maisha yake ikiwemo kufunzu fainali za AFCON mara tatu na kutimiza ndoto yake ya muda mrefu ya kuweka historia ya kuingia 16 bora kwa mara ya kwanza.

    ''Nina imani huu ni wakati wa vipaji vipya kupewa nafasi ya kutufikisha katika hatua za juu zaidi.''

    ''Nikijivunia Utanzania wangu, ninaahidi kuendelea kutoa mchango wangu kwa timu ya taifa katika maeneo mengine yaliyo ndani ya uwezo wangu na uzoefu wangu.'' Aliandika

  16. Jeshi la Iran limesema limeshambulia maeneo 85 ya kijeshi ya Marekani nchini Kuwait na Bahrain

    Jeshi la Iran limetangaza kuwa limeanzisha mashambulizi dhidi ya vituo vya kijeshi vya Marekani katika kile lilichokitaja kuwa ni jibu la mashambulizi yaliyofanywa na Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) dhidi ya zaidi ya malengo 80 kusini mwa Iran.

    Katika taarifa iliyotolewa Jumatano, Julai 8, IRGC ilidai kuwa Marekani ilikiuka makubaliano ya kusitisha mapigano na makubaliano ya Islamabad kwa kufanya mashambulizi ya anga mapema asubuhi dhidi ya vituo vya pwani na maeneo ya kiraia katika mikoa ya Hormozgan na Mahshahr.

    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, katika "hatua ya awali ya kujibu uchokozi huo," vikosi vya majini na anga vya IRGC vilifanya mashambulizi ya pamoja ya makombora na ndege zisizo na rubani (droni), yakidai kulenga na kuharibu vituo 85 muhimu vya kijeshi vya Marekani, vikiwemo eneo la Port Salman, Makao Makuu ya Kikosi cha Tano cha Wanamaji wa Marekani nchini Bahrain, pamoja na Kambi ya Anga ya Ali Salem nchini Kuwait.

    IRGC pia ilidai kuwa ilidungua ndege moja isiyo na rubani aina ya MQ-9 ya Marekani iliyokuwa ikijaribu kuingilia operesheni hiyo.

    Kabla ya tangazo hilo, jeshi la Kuwait lilisema lilikuwa limewasha mifumo yake ya ulinzi kutokana na kile lilichokiita mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani, huku pia kukiwa na ripoti za ving'ora vya tahadhari kusikika nchini Bahrain.

    Tangazo la IRGC kuhusu mashambulizi dhidi ya malengo ya kijeshi ya Marekani nchini Kuwait na Bahrain limetolewa wakati Iran imeendelea kukanusha kuhusika na mashambulizi dhidi ya meli tatu za kubeba mafuta katika Mlango wa Hormuz yaliyotokea Jumanne, Julai 6.

    Mashambulizi hayo yamezua mzozo mpya wa kijeshi kati ya Iran na Marekani. Wakati Iran ikikanusha kuhusika, Qatar, Saudi Arabia na Marekani zimeilaumu IRGC kwa kuhusika na mashambulizi dhidi ya meli hizo.

    Unaweza kusoma;

  17. Wafanyakazi wa bandari wanavyohofu kupoteza kazi kutokana na maatumizi ya AI

    Wafanyakazi wa bandari nchini Australia wanadai wiki ya kazi ya saa 28 bila kupunguziwa mishahara, huku matumizi ya akili mnemba (AI) na teknolojia ya otomatiki yakizidi kuongezeka katika bandari za nchi hiyo.

    Shinikizo la kuanzishwa kwa AI linaongozwa na kampuni kubwa ya usafirishaji na uendeshaji wa bandari, DP World, ambayo Chama cha Wafanyakazi wa Baharini cha Australia (MUA) kinasema kimeweka ajira za wafanyakazi "kwenye hatari kubwa."

    Chama hicho kilisema: "Ikiwa DP World inataka kutumia AI na otomatiki, basi lazima ilipe faida za kijamii zinazotokana na teknolojia hiyo. Teknolojia mpya haipaswi kuwagharimu wanachama wetu ajira zao au kuhatarisha maisha yao ili tu kampuni iongeze faida."

    BBC imewasiliana na DP World kuomba maoni yao na pia imeiomba MUA kutoa maelezo zaidi kuhusu madai hayo.

    DP World, yenye makao makuu yake Dubai, imekuwa ikijaribu kutumia zana za AI kusimamia wafanyakazi na kupanga ratiba za kazi katika shughuli zake, kwa mujibu wa utafiti wa Kituo cha Kimataifa cha Uwajibikaji na Utafiti wa Kodi za Makampuni, uliofanywa kwa agizo la MUA.

    Utafiti huo unasema mpango wa kuongeza matumizi ya otomatiki ni sehemu ya mwenendo wa kuingiza AI katika shughuli za kampuni "bila mashauriano ya kweli," na kwamba unaweza kuhatarisha ajira za hadi wafanyakazi 1,000, sawa na zaidi ya asilimia 60 ya wafanyakazi wa bandarini na wa matengenezo.

    Pia ilielezwa kuwa kampuni hiyo imependekeza matumizi ya kreni zinazoendeshwa kwa udhibiti wa mbali kwa msaada wa AI pamoja na magari yanayojiendesha yenyewe.

    Chama cha MUA kimesema teknolojia hiyo "inapaswa kutumika kuboresha maisha ya wafanyakazi, si kuyaharibu," huku kikisisitiza wito wake wa kuanzishwa kwa wiki ya kazi ya saa 28.

    Kwa mujibu wa gazeti la Australian Financial Review, ambalo lilikuwa la kwanza kuripoti kuhusu mazungumzo hayo, wafanyakazi wa DP World kwa sasa wanaaminika kufanya kazi kati ya saa 32 na 35 kwa wiki, kutegemea eneo walipo.

    DP World, kampuni inayomilikiwa na serikali ya Dubai, ni miongoni mwa waendeshaji wakubwa zaidi wa bandari duniani na iko chini ya usimamizi wa mtawala wa Dubai, Sheikh Mohammed bin Rashid Al Maktoum.

    Nchini Australia, kampuni hiyo husafirisha mamilioni ya makasha ya mizigo kila mwaka kupitia bandari zake zilizopo Sydney, Melbourne na maeneo mengine ya nchi.

    Ikiwa na shughuli katika nchi 84 na zaidi ya wafanyakazi 126,000 duniani kote, DP World hushughulikia takriban asilimia 10 ya usafirishaji wa makasha ya mizigo duniani.

    Unaweza kusoma;

  18. Misri yakerwa na 'dhuluma' na kudai Messi alipendelewa

    Zikiwa zimesalia dakika 12 kabla ya kumalizika kwa muda wa kawaida wa mchezo, Misri ilikuwa karibu kuandika historia kwa kupata ushindi wake mkubwa zaidi kuwahi kutokea katika Kombe la Dunia.

    Mafarao walikuwa mbele kwa mabao 2-0 dhidi ya Argentina, mabingwa watetezi wa dunia, kwenye Uwanja wa Atlanta.

    Nafasi ya kufuzu kwa robo fainali kwa mara ya kwanza ilikuwa karibu kutimia kwa taifa hilo la Afrika linalopenda sana soka.

    Lakini mambo yalibadilika kwa kasi kubwa.

    Cristian Romero alipofunga bao la kwanza la Argentina katika dakika ya 79, Misri ilihitaji tu kujilinda hadi mwisho wa mchezo. Hata hivyo, hali ilibadilika ghafla wakati nahodha Lionel Messi aliposawazisha matokeo kuwa 2-2 dakika nne baadaye.

    Kisha Enzo Fernandez alifunga bao la ushindi kwa kichwa katika dakika ya pili ya muda wa nyongeza, na kuwafanya mashabiki wa Argentina kushangilia kwa furaha.

    Misri ilitoka uwanjani ikiwa imevunjika moyo na yenye hasira, hasa baada ya Mfumo wa Usaidizi wa Waamuzi kwa Video (VAR) kulifuta bao la pili la Mostafa Zico kutokana na faulo iliyodaiwa kufanywa na kiungo Marwan Attia, aliyepatikana amemkanyaga kidogo Lisandro Martinez mwanzoni mwa shambulizi hilo wakati Misri ikiwa inaongoza kwa bao 1-0.

    Wachezaji wa Misri pia walisisitiza kuwa Mohamed Salah alifanyiwa faulo ndani ya eneo la penalti la Argentina sekunde chache kabla ya mabingwa hao wa dunia kuanzisha shambulizi lililozaa bao la ushindi.

    Mwamuzi wa Ufaransa, Francois Letexier, alipopuliza filimbi ya mwisho, wachezaji wengi wa Misri walianguka chini kwa mshangao na huzuni kutokana na kilichotokea.

    Katika mahojiano makali baada ya mchezo, kocha wa Misri, Hossam Hassan, alisema timu yake "haikutendewa haki" na kwamba "ilidhulumiwa." BBC Sport imesema imeiomba FIFA kutoa maoni kuhusu madai hayo.

    "Kuna mambo mengi ya kuhojiwa ndani na nje ya uwanja," alisema Hassan.

    "Kulikuwa na mambo mengi yasiyoridhisha. Kinachozungumziwa hapa ni uaminifu na namna mchezo ulivyochezeshwa.

    "Huenda walitaka mabingwa wa dunia waendelee kubaki kwenye mashindano. Huenda walitaka Messi aendelee kushiriki.

    "Mabingwa wa dunia walipata msaada katika kila namna. Inaonekana kulikuwa na shinikizo kutoka upande wa Argentina kuhusu matokeo haya."

    Mchezo huo ulikuwa na kila aina ya drama: penalti iliyookolewa, bao lililofutwa na VAR, kadi nyekundu, pamoja na kurejea kwa kushangaza kwa Argentina kutoka nyuma kwa mabao mawili na kushinda bila kuhitaji muda wa nyongeza.

    BBC Sport imechambua mechi hiyo, ambayo itaingia kwenye historia ya Kombe la Dunia kama mojawapo ya mechi za kusisimua zaidi, baada ya timu iliyokuwa nyuma kwa mabao mawili hadi dakika za mwisho kuibuka na ushindi ndani ya muda wa kawaida.

    Unaweza kusoma;

  19. Marekani yaanzisha mashambulizi dhidi ya Iran baada ya meli za mafuta kushambuliwa katika Mlango wa Hormuz

    Marekani imeanzisha mashambulizi makali dhidi ya Iran kujibu mashambulizi yaliyolenga meli tatu za kubeba mafuta katika Mlango wa Hormuz.

    Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (Centcom) ilisema Jumanne kuwa ilishambulia zaidi ya malengo 80, yakiwemo zaidi ya boti ndogo 60 za Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) zilizokuwa katika mlango huo wa bahari.

    Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema mashambulizi ya Marekani ni ukiukaji wa makubaliano ya maelewano kati ya Marekani na Iran yaliyotiwa saini mwezi uliopita, na kuonya kwamba Tehran "itachukua hatua madhubuti."

    Vyombo vya habari vya serikali ya Iran vilisema mashambulizi yalilenga Kisiwa cha Qeshm, Bandar Abbas na Sirik, ambapo baadhi ya watu walijeruhiwa. Iran haijatangaza rasmi kuhusika na mashambulizi dhidi ya meli tatu za mafuta yaliyosababisha Marekani kuanzisha mashambulizi hayo.

    Centcom ilisema mbali na kushambulia boti hizo ndogo zaidi ya 60, pia ililenga maeneo ya kurushia makombora na vituo vya uongozi vya Iran, lakini haikutaja maeneo halisi ya mashambulizi hayo.

    Marekani ilikuwa imeonya kwamba kungekuwa na madhara kufuatia kile ilichokiita mashambulizi "yasiyokubalika kabisa" dhidi ya meli hizo tatu za mafuta.

    Kabla ya mashambulizi hayo, Wizara ya Fedha ya Marekani ilifuta msamaha uliokuwa umesitisha kwa muda vikwazo vya mafuta dhidi ya Iran. Msamaha huo ulikuwa sehemu ya makubaliano ya maelewano yaliyotiwa saini kati ya Washington na Tehran mwezi uliopita.

    Unaweza kusoma;

  20. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu leo