Pakistan yashambulia maeneo ya mpakani mwa Afghanistan

Chanzo cha picha, Getty Images
Pakistan imesema imefanya mashambulizi ya anga na ardhini dhidi ya maeneo iliyodai kuwa ni maficho ya wanamgambo wa Kiislamu ndani ya mpaka wa Afghanistan.
Waziri wa Habari wa Pakistan, Attaullah Tarar, amesema mashambulizi hayo yamefanyika katika majimbo ya Paktia, Paktika na Kunar.
Maafisa wa Taliban nchini Afghanistan wamesema makumi ya raia wameuawa au kujeruhiwa katika mashambulizi hayo.
Mashambulizi hayo yamejiri siku chache baada ya kundi la wanamgambo wa Kiislamu kushambulia kambi ya askari wa Pakistan Rangers katika mji wa Karachi kusini mwa nchi hiyo na kuwaua wanajeshi watatu.
Islamabad imekuwa ikiishutumu serikali ya Taliban mjini Kabul kwa kuwapa hifadhi na ulinzi wanamgambo wanaoshambulia vikosi vya Pakistan, madai ambayo utawala wa Kabul umeyakanusha vikali.






