Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Wanawake wa Manipur kwenye video ya kushambuliwa wakiwa uchi 'hawatakata tamaa'
- Author, Na Divya Arya
- Nafasi, BBC News, Manipur
- Iliyochapishwa
Miezi sita baada ya kuvuliwa nguo, kuonyeshwa uchi na kudaiwa kubakwa na genge la watu kaskazini-mashariki mwa India, wanawake wawili, ambao masaibu yao yalitangazwa hadharani katika video iliyosambazwa kwa njia ya mtandao, walizungumza na BBC katika mahojiano yao ya kwanza ya ana kwa ana. Wanazungumza juu ya kuishi mafichoni, kupigania haki na wito wao wa utawala tofauti kwa jamii yao.
Onyo: Makala haya yana maelezo ya unyanyasaji wa kingono
Mara ya kwanza, ninachoona ni macho yao yaliyoangalia chini
Barakoa kubwa nyeusi zinaficha nyuso zao nyuso na mitandio ya Glorr na Mercy inafunika vipaji vya nyuso zao.
Wanawake wawili wa Kuki-Zomi hawataki kuonekana. Lakini wanataka kusikilizwa.
Masaibu yao yalirekodiwa na kushirikishwa mtandaoni. Yanasumbua fikra kutazama. Chini ya dakika moja, inaonyesha kundi la wanaume kutoka jamii iliyo ya wengi ya Meitei katika jimbo la Manipur wakitembea karibu na wanawake wawili walio uchi, wakiwasukuma, kuwapapasa, na kisha kuwaburuta hadi kwenye uwanja ambapo wanasema walibakwa na genge la watu.
"Nilitendewa unyama ," anasema Glory, akianza kulia. "Ilikuwa vigumu kuishi na kiwewe hicho, lakini miezi miwili baadaye wakati video ya shambulio hilo iliposambaa, karibu nilipoteza matumaini kabisa ya kuendelea kuishi," anaongeza.
"Unajua jinsi jamii ya Kihindi ilivyo, jinsi wanavyowatazama wanawake baada ya tukio kama hilo," anasema Mercy. "Ninapata ugumu kukutana na watu wengine, hata katika jamii yangu.Fahari yangu imetoweka. Sitakuwa sawa tena."
Video hiyo iliongeza mateso yao lakini pia ikawa ushahidi wa ukosefu wa haki kwa sababu ilileta umakini kwenye mapigano ya kikabila kati ya jamii ya Meitei na Kuki ambayo yalizuka Manipur mwezi wa Mei. Lakini wakati video hiyo ilizua hasira na kuchochea hatua, kuangaziwa huko kulifanya wanawake hao warudi nyuma zaidi.
Kabla ya kuvamiwa, Glory alikuwa mwanafunzi na Mercy alikuwa akiwahudumia watoto wake wawili wadogo, akiwasaidia kazi za nyumbani na kwenda kanisani. Lakini baada ya shambulio hilo wanawake wote wawili walilazimika kukimbilia mji tofauti ambapo wanaishi mafichoni.
Wanakaa ndani sasa. Akiwa amezuiliwa kwenye kuta za nyumba yao ya muda, Mercy haendi tena kanisani au kuwapeleka watoto wake shuleni yeye mwenyewe.
"Sidhani kama nitaweza kuishi kama nilivyoishi hapo awali," anasema. "Ninapata ugumu kutoka nje ya nyumba, ninaogopa na kuona aibu kukutana na watu."
Glory anahisi vivyo hivyo na ananiambia yeye pia bado yuko "katika kiwewe", anaogopa kukutana na watu na anaogopa umati.
Huduma za ushauri zimewasaidia lakini hasira na chuki vimeingia ndani sana. Wameamua kuongea ili kuhakikisha hakuna mwanamke mwingine atakayetendewa hivi tena.
Miezi sita iliyopita, Glory alikuwa akisoma katika darasa mchanganyiko la wanafunzi wa Meitei na Kuki chuoni ambako alikuwa na marafiki wengi, lakini sasa anasema hataki kuonana na mtu mwingine wa Meitei tena.
"Sitarudi tena kijijini kwangu. Nilikulia huko, ilikuwa nyumbani kwangu, lakini kuishi huko kutamaanisha kutangamana na Meitei ambao ndio majirani na sitataka kamwe kukutana nao tena," anasema. Mercy anakunja mikono na kugonga meza huku akikubaliana naye.
Kijiji chao kiliposhambuliwa na kila mtu akakimbia kuokoa maisha yake, babake Glory na mdogo wake walivutwa na kundi la watu na kuuawa.
"Niliwaona wakifa mbele ya macho yangu," anasema kwa upole. Anaeleza jinsi ilimbidi kuiacha miili yao uwanjani alipokuwa akijaribu kujiokoa.
Ananiambia hawezi hata kwenda kuwatafuta sasa. Tangu ghasia kuzuka, hakuna maelewano kati ya jamii za Meitei na Kuki-Zomi huko Manipur. Watu wamegawanywa na mpaka wa ulio na vituo vya ukaguzi vinavyosimamiwa na polisi, jeshi na watu wa kujitolea wa jamii hizo mbili.
"Sijui hata miili yao imehifadhiwa katika chumba gani cha maiti na siwezi kwenda kuangalia," anasema. "Serikali inapaswa kutukabidhi."
Ni nini kilitokea huko Manipur?
· Zaidi ya nusu ya watu milioni tatu wa Manipur ni wa jamii ya Meiteis, ambapo karibu 43% ni Kukis na Nagas.
· Mapigano mapya yalizuka mwezi wa Mei wakati Kukis walipoandamana dhidi ya madai ya Meitei ya kuwa na hadhi ya kikabila - Kukis walihofia kuwa hii ingeimarisha ushawishi wa Meitei na kuwaruhusu kununua ardhi au kuishi katika maeneo ya Kuki.
· Serikali ya jimbo, inayoongozwa na N Biren Singh, Meitei, imeshutumu vikundi vya waasi wa Kuki kwa kuchochea jamii.
· Zaidi ya watu 200 wamekufa kufikia sasa, wengi wao kutoka kwa jamii ya Kuki, na maelfu wamekimbia kutoka pande zote mbili.
Wanawake wa Meitei pia wanasema wameshambuliwa, na angalau lalamiko moja la polisi liliwasilishwa lakini, kama wanawake kote India, wengi wanaona ni aibu sana kujadili unyanyasaji wa kingono kutokana na unyanyapaa .
Mume wa Mercy anaelezea jinsi nyumba na kanisa la kijiji zilivyochomwa moto katika shambulio hilo.
"Niliita polisi wa eneo hilo, lakini wakasema hatuwezi kusaidia, kituo chetu cha polisi pia kinashambuliwa," anasema. "Niliona gari la polisi barabarani, lakini hawakufanya chochote.
"Nina huzuni na hasira kwa kushindwa kwangu kufanya lolote. Sikuweza kumuokoa mke wangu wala wanakijiji. Hilo linanivunja moyo," anasema. "Wakati mwingine mimi hukasirika sana nikifikiria juu ya kila kitu kilichotokea, nikiwa na huzuni na hasira, nahisi kuua mtu."
Wiki mbili baada ya shambulio hilo, aliwasilisha malalamiko kwa polisi, lakini hakuna hatua iliyochukuliwa hadi video hiyo ilipoonekana Julai. Duru za polisi zimeiambia BBC kwamba kwa sasa wamemsimamisha kazi afisa anayesimamia kazi hiyo na wengine wanne kusubiri uchunguzi.
Hasira iliyoenea iliyofuatia kutolewa kwa video hiyo ilimlazimu Waziri Mkuu Narendra Modi kutoa kauli yake ya kwanza kuhusu ghasia hizo. Hayo yalifuatiwa na kukamatwa kwa wanaume saba ambao sasa wamefunguliwa mashtaka ya ubakaji na mauaji .
Glory, Mercy na mumewe wananiambia wanapata nguvu kutokana na jumbe za usaidizi ambazo zimemiminika tangu video ya shambulio hilo kuanza kusambaa mtandaoni.
"Bila video, hakuna mtu ambaye angeamini ukweli, kuelewa maumivu yetu," mume wa Mercy anasema.
Mercy bado anapata jinamizi na ana hofu ya kufikiria juu ya siku zijazo, haswa kwa watoto wake. "Inanilemea sana, mawazo kwamba hatuna cha kuwapitishia, kila kitu kimepita," anasema.
Glory anaeleza kuwa wanataka utawala tofauti kwa jamii yao. "Hiyo ndiyo njia pekee ya kuishi kwa usalama na amani," anasema.
Watu wa Kuki wamefanya matakwa haya yenye utata mara nyingi lakini yanapingwa na jamii ya Meitei. Waziri mkuu wa jimbo hilo, kutoka jamii ya Meitei, ametoa wito mara kwa mara wa kuwepo kwa umoja wa Manipur.
Glory na Mercy wana imani ndogo na serikali ya mtaa na wanaishutumu kwa kuwa na upendeleo dhidi ya jamii yao lakini serikali ya jimbo hilo imekanusha madai haya.
Waziri mkuu, N Biren Singh, hakujibu wakati BBC ilipomweleza madai hayo, lakini katika mahojiano ya hivi majuzi na Indian Express alisema: "Hakuna upendeleo moyoni mwangu au kazi yangu."
Video hiyo pia ikawa wakati ambapo Mahakama ya Juu ilizingatia mapigano ya kikabila na kupendekeza kwamba kesi zote za vurugu zikabidhiwe kwa mashirika huru ya uchunguzi, kama vile Ofisi Kuu ya Upelelezi (CBI). Mahakama kuu imeitaka serikali ya jimbo hilo kutambua miili ya watu waliouawa na kuwarejesha kwa jamaa zao wa karibu.
Akiangalia siku za usoni, Glory anatarajia kuendelea na masomo yake katika chuo tofauti ili aweze kutekeleza ndoto yake ya kuwa mwanajeshi au afisa wa polisi. "Azimio langu limeimarishwa kufanya kazi kwa kila mtu kwa njia isiyo na upendeleo," ananiambia. "Na ninataka haki, kwa gharama yoyote ile... Ndiyo maana pia ninazungumza, kwa hivyo hakuna mwanamke anayedhurika tena jinsi nilivyokuwa."
Mercy ananiambia kuwa "kama wanawake wa kabila tuna nguvu, hatukati tamaa" na tunapoamka kuondoka, anasema ana ujumbe.
"Nataka kuwaambia akina mama wote wa jamii zote kuwafundisha watoto wao, bila kujali kitakachotokea, kamwe wasidharau wanawake."
Majina ya wanawake hao wawili yamebadilishwa kwa makala hii.