Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Vita vya Ukraine: Jinsi wanawake wanavyopata nafasi katika jeshi la Ukraine
- Author, Halyna Korba
- Nafasi, ВВС News Ukrainian
- Iliyochapishwa
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, idadi ya wanawake katika jeshi la Ukraine imekaribia mara mbili. Wadunguaji wa kike, wapiga risasi na wafanyakazi wa vifaru si jambo la ajabu tena katika jeshi la Ukraine, lakini wanawake bado wanapaswa kupigania nafasi yao katika sekta hii ya wanaume wengi.
"Wanawake wanatendewa kwa tahadhari zaidi, wakati mwanaume aliye katika vita anapata heshima moja kwa moja," Maryna Moloshna anasema. "Mwanamke analazimishwa mara kwa mara kuthibitisha kwamba anastahili kufanya kitu, kwamba hatawaangusha wanaume, kwamba anaweza kuaminiwa na kutegemewa."
Wakati Moloshna alipozungumza na BBC, alikuwa akifanya misheni ya kivita katika eneo la Kharkiv kama anayehudumu kwenye Vikosi vya Wanajeshi vya Ukraine.
Anahisi kujiamini katika jukumu lake jipya, ingawa anakiri kwamba kuwa mwanajeshi wa kike katika jeshi la Ukraine bado si rahisi.
Baada ya uvamizi, Moloshna alienda mstari wa mbele kama mtu wa kujitolea. Anasema alitaka kufanya zaidi kulinda nchi yake na alijisikia hatia kuhusu kuondoka Mariupol, ambako alifanya kazi kama mwandishi wa habari kabla ya vita.
Mji wa pwani kusini-mashariki mwa Ukraine ulikuwa eneo la mapigano makali ya miezi kadhaa kabla ya kuangukia kwa Warusi.
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, idadi ya wanawake katika jeshi la Ukraine imekaribia kuongezeka maradufu hadi 40,000 - zaidi ya 5,000 kati yao wakiwa mstari wa mbele - kulingana na vyanzo vya kijeshi.
Wanawake katika jeshi bado wanaripoti matatizo mengi - kutokana na vifaa vya kijeshi vilivyoundwa ambavyo wanaume pekee wanamudu hadi ubaguzi wa kijinsia wa kawaida - lakini jukumu la wanawake katika jeshi linazidi kuonekana na kukubalika na jamii ya Ukraine.
"Hapo zamani lilikuwa jeshi la baada ya Usovieti, gumu na la kiume, lakini sasa jeshi linakuwa linafaa zaidi na sawa,sasa wanaweza kujithibitisha," anasema Oksana Grygoryeva, mshauri wa masuala ya jinsia kwa kamanda wa vikosi vya ardhini vya Ukraine.
Maafisa, kikosi cha vifaru na bunduki
Nafasi ya wanawake katika jeshi la Ukraine imebadilika kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha miaka 15 iliyopita, sio tu kwa wingi, lakini pia katika ubora, anasema Oleksiy Melnyk wa Kituo cha Razumkov, taasisi isiyo ya kiserikali ya Kiukraine.
Hapo awali, wanawake walitumiwa hasa katika nafasi zisizo za kupigana - watu wa mawasiliano ya simu, waandishi wa habari, wapishi, madaktari, nk.
Hii ilibadilika na kuanza kwa vita huko Donbas mnamo 2014, wakati wanawake walienda kupigana katika vikosi vya kujitolea kwa idadi kubwa kwa mara ya kwanza. Huko, hakuna mtu aliyezingatia taratibu za ukiritimba.
"Kulikuwa na visa vingine wakati mwanamke alipigana kama mpiga risasi, lakini aliorodheshwa kama mpishi au mpiga chapa katika makao makuu," Melnyk anakumbuka.
Lakini mwaka 2018 vizuizi fulani kwa wanawake vilikomeshwa kisheria, waliweza kuchukua majukumu kisheria na kupokea mafunzo kwa usawa na wanaume.
Sasa wanawake wanapigana kama makamanda wa vikosi, betri za mizinga na vitengo vya anga visivyo na rubani, alisema kamanda wa vikosi vya Umoja wa Vikosi vya Wanajeshi wa Ukraine, Luteni Jenerali Serhiy Naev.
Kwamujibu wa data yake, zaidi ya wanawake 8,000 wanashikilia nyadhifa za afisa, akiwemo Brigedia-Jenerali Tetyana Ostashchenko, kamanda wa vikosi vya matibabu, ambaye alikua jenerali wa kwanza wa kike nchini mnamo 2021.
"Kuna wanawake wengi wenye nguvu," Grygoryeva anathibitisha. "Kuna makamanda wa bunduki, makamanda wa kikosi, wadunguaji wengi. Kuna hata mwalimu wa kupiga mbizi kwenye kina kirefu cha bahari."
"Kuna wanawake wengi kati ya wafanyakazi wa vifaru, ni wepesi na wadogo kuliko wanaume na inaweza kuwa rahisi kwao kuwa kwenye kifaru," anasema.
Wanawake katika majukumu ya mapigano mara nyingi huwa na utulivu zaidi wa kisaikolojia kuliko wanaume na wenye huruma zaidi linapokuja suala la uhusiano wa timu na kusaidia askari wenzao, Grygoryeva anaongeza.
Mtazamo wa jamii
Mtazamo wa wanawake wanaojiunga na jeshi pia umebadilika katika jamii. Tamara Martsenyuk, mwanasosholojia na mtafiti wa jinsia katika Chuo cha Kyiv-Mohyla, analinganisha tafiti mbili za kisosholojia kuhusu mada hii.
Mnamo mwaka wa 2018, utafiti wa Taasisi ya Kimataifa ya Sosholojia ya Kyiv (KMIS) uligundua kuwa wazo la haki sawa na fursa kwa wanaume na wanawake katika Jeshi liliungwa mkono na karibu 53% ya Waukraine.
Miaka minne baadaye, wakala wa utafiti "InfoSapiens" uligundua kuwa kiashiria hiki kimeongezeka hadi 80%.
Martsenyuk anaamini kwamba miaka minane ya uhasama nchini Ukraine imekuza taswira nzuri ya wanawake wa kijeshi, ambayo imeongezwa mwaka huu na uvamizi wa Urusi na hitaji la kuhamasisha watu zaidi.
Huduma za kijeshi 'si jambo linalotolewa na kila mtu'
Wazo la ushiriki wa wanawake wengi katika jeshi lilianza kabla ya uvamizi wa Urusi, hata hivyo.
Mwishoni mwa 2021, Wizara ya Ulinzi ilichapisha orodha ya taaluma ambazo zingehitaji wanawake kujiandikisha kwa huduma ya jeshi.
Orodha hiyo ilikosolewa mara moja kwa sababu ilihitaji kuandikishwa kwa taaluma za kawaida kama vile wataalamu wa IT, waandishi wa habari, wanamuziki, wafanyakazi wa ukarimu na watangazaji.
Kuna ushahidi kwamba baadhi ya Waukraine hawakurejea nchini kutoka nje kwa sababu ya hatua hiyo.
Anna, mwanasaikolojia kutoka Kyiv, ambaye ameishi na binti yake mdogo huko Austria tangu uvamizi huo, anakiri kwamba amechelewa kurudi Ukraine kwa sababu ya hatari ya kuandikishwa ghafla.
"Siyo kwamba niliogopa kujiunga na jeshi, lakini nilitaka uhakika, taratibu zilizo wazi," anafafanua.
"Ikiwa tutawaondoa akina mama kutoka kwa watoto wao wadogo, hatutakuza kizazi cha kawaida," Anna anaamini. taifa linategemea wanawake ambao wanapitisha utamaduni kwa watoto wao.
Kujibu ukosoaji huo, Wizara ya Ulinzi iliahirisha usajili wa wanawake hadi 1 Oktoba 2022, na kupunguza kwa kiasi kikubwa orodha ya taaluma.
Majira haya ya vuli usajili uliahirishwa kwa mwaka mwingine, na ukawa wa hiyari pekee, isipokuwa kwa madaktari wa kike.
Wanasiasa wengine hawakukubaliana na wanawake kutendewa tofauti na wanaume, hata hivyo. Maryana Bezugla, naibu mkuu wa kamati ya usalama wa taifa, ulinzi na ujasusi, anasema kwamba hakupigia kura sheria mpya, za hiyari za kuandikisha wanawake.
"Suala la usawa wa kijinsia sio tu kuhusu haki na fursa sawa, bali pia wajibu. Kusiwe na mgawanyiko wa raia. Ikiwa usajili wa hiyari utatekelezwa, unapaswa kuwa wa wanaume na wanawake," alisema.
Ingawa mwanamke katika jeshi la Kiukraine sio nadra tena, hiyo haimaanishi kwamba wanatendewa kwa usawa kila wakati.
Maryna Moloshna anakiri kwamba alishangazwa sana na mtazamo wa amri yake ya kikosi kuhusu wanawake.
"Hatuzungumzii viwango vyovyote vya Nato," anasema. "Mara nyingi tunakutana na ubaguzi wa kijinsia, na wakati mwingine baadhi ya makamanda hata huwadhalilisha wanawake."
Maisha ya kila siku katika jeshi pia bado yanazingatia wanaume: wanawake huvaa sare sawa na wanaume, kutafuta buti ndogo za jeshi ni changamoto ya kweli, na wanawake hawapewi nguo za ndani za kike au za joto. Wanawake pia wanapaswa kununua bidhaa zao za usafi wa kike, kama vile pedi au tamponi, anasema Moloshna.
Maelfu ya askari wa kike huja kwetu mara kwa mara na matatizo haya, anasema Ksenia Draganyuk, mwanzilishi mwenza wa shirika la umma la "Zemlyachki", ambalo husaidia wanawake katika jeshi.
Anasema mfuko huo unawapatia wanawake nguo za ndani za kijeshi, mafuta, sare, sahani nyepesi za kujikinga, kofia, bidhaa za usafi, vifaa vya huduma ya kwanza vilivyoundwa mahususi kwa ajili ya wanawake.
"Unapoenda kwenye ukumbi wa mazoezi, unataka nguo za starehe ili iwe rahisi kukimbia na kufanya mazoezi. Inapokuwa kwenye mstari wa mbele na lazima ufanye kazi za mapigano, ni suala la usalama," anaelezea.
Mfuko huo pia unatoa msaada wa kisaikolojia - kwa wale ambao kwa sasa wako katika harakati za kijeshi, lakini pia kwa wanawake ambao wanapaswa kupambana na ubaguzi wa kijinsia.
Mamlaka zinasema zinatambua matatizo haya na kuahidi mabadiliko.
Mnamo Julai, BBC iligundua kuwa sare maalum ya kijeshi kwa wanawake ingeanzishwa, lakini haijulikani ni lini itakuwa tayari kwa huduma.
"Si nchi zote za Nato bado zina sare za wanawake; nchini Marekani zilianza kuendelezwa mwaka 2009 pekee," anabainisha Oksana Grygoryeva, ambaye anaamini kuwa Ukraine inapiga hatua za haraka katika eneo hili.
Anasema vikosi vya kijeshi vinafanya kazi kupambana na ubaguzi na kuelimisha wanajeshi, lakini anaongeza kuwa wanawake wanapaswa kuripoti matatizo kama vile unyanyasaji au ubaguzi kwa kuwasiliana na msimamizi wao wa karibu, mshauri wa jinsia au simu ya dharura ya Wizara ya Ulinzi.
Grygoryeva anasema amepokea malalamiko mawili pekee tangu achukue nafasi yake tarehe 1 Februari, moja kuhusu ubaguzi na moja kuhusu unyanyasaji. Wote wawili wamechunguzwa kwa kina.
"Nawahimiza wanawake kuzungumza, tutasaidia," anasema. "Kamanda ataogopa kunyanyasa au kubagua akijua ataadhibiwa. Inaweza kuwa kukemewa au kushushwa cheo."
Kadiri wanawake wanavyozidi kuwa katika jeshi la Ukraine, ndivyo mabadiliko yatakavyokuja haraka, anasema Moloshna.
"Kutakuwa na usawa zaidi na ubaguzi utapungua," ana uhakika. "Kwa sababu hadi sasa hatuko wengi hapa, hasa katika nafasi za mapigano. Kuna wengi wetu kuliko miaka michache iliyopita, lakini mwanamke katika jeshi bado mara nyingi anachukuliwa kwa namna ya tofauti."