Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Moto Uchina: Jumba refu lateketezwa na moto mkubwa China
Moto mkubwa umeteketeza jengo kubwa katika mji wa Changsha nchini China, vyombo vya habari vya serikali vimeripoti.
Kanda za video zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha miali mikubwa ya moto ikitanda kwenye upande wa jengo hilo la ghorofa 42 huku wafanyakazi wa ofisi wakikimbilia usalama wao nje ya jengo.
Mawingu mazito ya moshi mweusi yalitanda nje ya jengo hilo, ambalo ni ofisi ya eneo la China Telecom.
Mamlaka ilisema moto huo umezimwa na kwamba hakuna majeruhi ambao wameripotiwa kufikia sasa.
Picha zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha wazima moto wakilenga ndege za maji kwenye uso wa jengo lenye urefu wa mita 218 (futi 715) katika harakati za kuzima moto huo.
Upande mzima wa jumba hilo kubwa ulionekana kumezwa na miali ya moto wakati mmoja. Moto mkubwa ulipanda upande wa jengo huku moshi ukifuka kwenye video nyingine, watu kadhaa walionekana wakikimbia eneo la tukio huku vifusi vinavyowaka moto vikishuka kutoka kwenye sakafu ya juu ya jengo hilo.
BBC bado haijaweza kuthibitisha kanda hiyo na haijabainika kwa sasa ni nini kilisababisha moto huo.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali, jengo hilo lilikamilika mwaka wa 2000 na liko karibu na barabara kuu ya mzunguko katika mji wa Changsha, mji mkuu wa watu milioni 10 wa mkoa wa Hunan, kusini ya kati mwa China.
Katika taarifa iliyoripotiwa na shirika la habari la AFP, kampuni ya mawasiliano inayomilikiwa na serikali ya China Telecom ilithibitisha kisa hicho, ikisema kwamba ulizimwa ''majira ya 16:30 (saa za ndani)''.
''Bado hakuna majeruhi ambao wamegunduliwa na mawasiliano hayajakatika,'' msemaji wa kampuni alisema.
Moto mkubwa ni jambo la kawaida nchini China, ambapo mapema mwaka huu kampuni kubwa ya kemikali huko Shanghai ulilipuka kwa moto.