Uchaguzi Kenya 2022: Je wanamuziki wana ushawishi gani katika siasa za Kenya?

    • Author, Dinah Gahamanyi
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Kinyume na siasa za miaka iliyopita, wanasiasa katika uchaguzi wa mwaka wa 2022, wanaonekana kwenda na wakati, hususan inapokuja katika kuchagua  nyimbo wanazozitumia katika kampeni zao ili kuwavutia wafuasi wao,hasa wale wa umri mdogo .

Kwa mfano Wagombea wakuu wa Urais Raila Odinga na Naibu Rais William Ruto , katika nyakati fofauti wameonekana kutumia wimbo uliovuma al Maarufu ''Sipangwingwi'. 

''Sipagwingwi''ulioimbwa kwa Lugha ya Sheng, na kijana mwenye umri wa miaka 17- Mario TJ Kasela, aliyekuwa shule ya upili, akimshirikisha Exray Taniua, imevuma sana kwenye redio mbali mbali nchini Kenya na sasa hutumiwa kwenye mikutano ya  kambi kuu mbili pinzani za kisiasa katika kampeni za uchaguzi wa  2022.

Wakati wa Kongamano la kitaifa la   Azimio La Umoja katika uwanja wa  Kasarani, mwanamuziki huyu aligonga vichwa vya habari wakati alipoonekana moja kwa moja kwenye Vituo vyote vya Televisheni katika matangazo ya kutoka kwenye kongamano hilo mbele ya umati uliokuwa ukisherehekea kuundwa kwa Muungano wa Azimio la Umoja.

Awali Mwenzake Exray Taniua  pia alionekana akiipiga 'mgoma' hiyo katika Kampeni za Naibu Rais William Ruto mwaka  2021.Mara baada  kukutana,  Naibu Rais aligeuza jina la wimbo, kulingana na ujumbe aliotaka kuufikisha kwa wapinzani wake na kuuita ''Hatupangwingwi'' katika mkutano wake wa kampeni.  Jina jipya la wimbo lililenga kuwaasa wapiga kura kutowaruhusu watu binafsi kuwaamlia kwa niaba yao ni nani atakayekuwa rais ajaye. 

 Sauti Sol - 'Tano Tena' wakiwashirikisha Nviiri The Storyteller na Bensoul

Katika kibao chao hivi karibuni  kabisa  ''Miaka tano tena'' Sauti Soul wakimshirikisha Nviiri The Storyteller na  Bensoul,   kilichopigwa kwa mtindo wa  R &B  ni  ''ngoma'', ambayo pia huenda haitasahaulika  katika uchaguzi wa wa Kenya kutokana na maudhui yaliyomo. ''Miaka tano tena''  ambao tayari umekwishatazamwa na watu zaidi ya laki mbili tangu  kuwekwa kwenye mtandao wa You Tube baada ya video yao kupakuliwa  tarehe 2 Agosti,  una maneno kama ''sikufi miaka tano tena'', na ''sikupi miaka tano tena'' unaonekana kutuma ujumbe unaolenga kuwashauri Wakenya waache kuwapigia kura viongozi walioshindwa kutekeleza ahadi za maendeleo kwa wananchi  au kutowahuduamia wapiga kura baada ya kuwachagua, miaka mitano iliyopita.  Haijulikani iwapo Wakenya watatekeleza maudhui yaliyomo ndani ya wimbo  ''Miaka Tano Tena''

 Mbali na kampeni za urais, katika kampeni za wagombea wa viti  vya Ubunge, ugavana, Useneta na madiwani(MCA), wagombea wamekuwa wakitumia tunzi za wasanii wa nyimbo za lugha za jamii zao kunadi sera zao na kuwashawishi wapiga kura kuwapigia kura katika uchaguzi mkuu.

Kubadilika kwa ''ladha'' za muziki kulingana na nyakati

'Ladha' za muziki unaotumika katika siasa za uchaguzi wa Kenya zimekuwa zikibadilika  kulingana na nyakati na mtindo wa muziki uliopo wakati huo na unaopendelewa na jamii hususan vijana.

Katika uchaguzi wa sasa ladha ya ''muziki wa Genge'',inatumiwa zaidi,  uchaguzi Mkuu uliopita kulikuwa na mapambano ya lugha katika matumizi ya nyimbo na kila wimbo uliimbwa kwa manufaa ya  wagombea.

Kwa mfano Ben Githae aliimba wimbo kwa ajili ya Muungano wa Jubilee  "Wembe Ni Ule Ule" kuashiria utayari wa Uhuru Kenyatta na Ruto  kuwania uongozi katika muhula wa pili , huku Muungano wa  Nasa ukiwa na wimbo  "Bindu Bichenjanga", ulioimbwa na Amos Barasa ulilenga kuonyesha kwamba mabadiliko  yanakuja katika ardhi ya ahadi , Canaan.

Wimbo mwingine uliovuma katika uchaguzi uliopita ni pamoja na  "Nasa (Tibim)" ulioimbwa na Onyi Jalamo, "Tano Tena" wa Ben Githae, "Jubilee Emet" wa Florence Chepng'etich, na  "Jubilee Tosha" ulioimbwa na Marion Cherotich.

'Ushawishi wa wanamuziki wa Kenya katika siasa sio wa sasa'

Katika kampeni za mwaka  2017, wasanii wawili   waling'aa. Emma Jalamo aliyeimba 'ngoma' iliyovuma NASA  ambapo wimbo wake uliimbwa kwa lugha ya  Luo, wimbo wake ulichezwa katika matukio yote ya kumuunga  mkono Raila na Muungano wake wakati huo -National Super Alliance (NASA). 

 Mwaka  2002, GidiGidi MajiMaji,  wimbo wa bendi yao maarufu ya Hip hop  iliimba kibao kilichoitwa "Unbwogable" kilichovuma na kupendwa wakati Mwai Kibaki wa NARC alipokabiliana na  Uhuru Kenyatta wa KANU katika mbio za kuingia ikulu

 "Hamu ya nchi ya mabadiliko ililetwa kwa njia ya muziki na wasanii .  Wanamuziki wawili, Joseph Ogidi na Jahd Adonija, chini ya jina Gidi Gidi Maji Maji, waliimba  kibao Ting Badi Malo na  I am Unbwogable , kilichokonga mioyo ya wapiga kura'', inasema taarifa ya tathmini ya utafiti uliofanywa na Gordon Omenya na kuchapishwa katika  Tathmini ya gazeti la East African.   

"Unbwogable ukawa wimbo uliotumiwa kuwahamasisha wapiga kura katika kuunga mkono  Muungano wa  -National Rainbow Coalition (NARC). Na tangu wakati huo, wanasiasa wamekuwa mara kwa mara wakiwakodi wasanii kuimba sifa zao na kwenye majukwaa yao ya kisiasa." , anasema Gordon Omenya.

Pia ''Ngoma'' ya DNA na P-Unit  "Una" ilitamba katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2007. 

Je wanamuziki wameweza kuwashawishi Wakenya kupiga kura?

Licha ya umaarufu wa kazi hizi za muziki wa wasanii kwenye majukwa ya wanasiasa wanaowania nyadhifa  mbalimbali za uongozi, kuna dalili ndogo sana za kuonyesha  kwamba wakenya hususan vijana wanashawishika kupiga kura. 

Katika ripoti yake ya ukaguzi ya Juni 2022, Tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) ilionyesha kuwa asilimia ya vijana, wenye umri wa kati ya miaka 18  hadi 34, walijisajili kupiga kura katika uchaguzi wa mwaka  2022  idadi hiyo ikipungua kwa asilimia 5.27 ikilinganishwa na uchaguzi wa mwaka 2017 - ambao ulibatilishwa na kurudiwa .

Inaaminika kuwa kazi za usanii hatahivyo zilichangia pakubwa katika kampeni za kuelekea uchaguzi , na kuwashawishi vijana kushiriki upigaji kura.

Mwaka huu kwa upande mwingine Roots Party, chama cha  George Wajackoyah - mmoja wa wagombea wanne wa urais, kimevutia ushawishi na hisia kubwa miongoni mwa vijana  katika uchaguzi wa mwaka huu hususan wale ambao awali hawakujali kuhusu mamsuala ya uchaguzi. Wasanii wameanza kubuni muziki unaozungumzia vitu anavyovitetea Bw. Wajackoyah  katika kampeni zake.

''Baadhi ya vijana wameanza kuimba nyimbo zenye ujumbe wa kuunga mkono -bangi na kutokana na kwamba mtindo  wake wenyewe wa kampeni unaendana na aina ya muziki   maarufu wa vijana, anasema   mkazi wa mtaa wa mabanda wa Kibera.'' Wamaitha Kariuki.,"Ujumbe wake wa  kubuni ajira umechangia pakubwa katika kuikumbusha hadhira kwamba kuna hali  mustakabali mzuri baada ya uchaguzi huu ," aliongeza

Unaweza pia kusoma: