Siku ya Bajeti Afrika Mashariki: Bajeti ‘ya kipekee’ Tanzania
Peter Mwangangi
BBC Swahili, Nairobi
Mawaziri wa fedha kutoka nchi za Afrika Mashariki wanatarajiwa kuwasilisha makadirio ya bajeti ya mwaka ujao wa fedha wa 2026/2027 leo Alhamisi (Juni 11), wakiangazia mipango ya matumizi na mapato ya nchi zao, pamoja na vipaumbele vya kila taifa katika juhudi za kukuza uchumi na kuimarisha maisha ya wananchi.Wananchi watarajie nini? Haya ni mambo matano yanayojitokeza kufikia sasa.
Tanzania imeahidi kuwa hii itakuwa bajeti ya ‘kipekee’, ikiwa ya kwanza katika awamu ya pili ya rais Samia Suluhu Hassan madarakani kufuatia uchaguzi wa mwaka uliopita.Waziri wa fedha Khamis Mussa Omar amesema kuwa bajeti ya $23.8 bilioni (Tsh 62.3 trilioni) itakayosomwa bungeni Dodoma itafadhiliwa zaidi na mapato ya ndani zaidi, huku serikali ikipunguza utegemezi wa misaada ya nje."
Kwa bajeti ya mwaka unaofuata, sehemu ya matumizi ambayo itagharamiwa na mapato ya ndani itakuwa ni asilimia 70% ambayo ni kiwango cha juu zaidi ya kiwango cha mwaka wa sasa wa kifedha unaomalizika.
Nayo misaada kutoka nje haitafika hata Tsh trilioni moja kwenye bajeti hiyo ya Tsh 62.3 trilioni," alisema Waziri Khamis Mussa katika kikao na waandishi wa habari jijini Dodoma, siku moja kabla ya kuwasilishwa kwa makadirio ya bajeti bungeni.
Maeneo makuu ya kipaumbele mwaka huu nchini humo yatakuwa miradi ya maendeleo ya kimkakati kama kuendeleza mradi wa reli ya kisasa (SGR), barabara, uwekezaji katika sekta za nishati na sekta nyinginezo ili kuchochea ukuaji wa uchumi.