Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
WARIDI WA BBC: Mama asimulia machungu ya kuuawa kwa wanawe wa kipekee
- Author, Anne Ngugi
- Nafasi, BBC Swahili
- Iliyochapishwa
Siku ambayo Lucy Wanjiru raia wa Kenya anayeishi nchini Uingereza hatawahi kuisahau maishani mwake ni ile siku alipokea taarifa ya vifo vya wanawe wawili wa kiume waliouawa katika mazingira ya kutatanisha.
Vijana hao wawili walikuwa pamoja na marafiki zao wawili wa kiume waliposhambuliwa na kuuawa na wanakijiji katika Kaunti ya Kajiado nchini Kenya katika kile kilichotajwa kushukiwa kuwa wahalifu.
Bi Wanjiru anasema alisafiri nje ya nchi mnamo mwaka 2018 kwa lengo la kuwatafutia riziki wanawe wawili wa kiume huko Uingereza.
Hakujua kwamba miaka mitatu baadaye atarejea nyumbani kwa uchungu mwingi atakaosalia nao maishani mwake.
Agosti 15 mwaka 2021, aliporejea Kenya kutoka Uingereza baada ya kupokea taarifa kwamba wanawe wawili wameuawa wimbi la simanzi lilimghubika mama huyu , taswira ambayo iliangaziwa katika vyombo vikuu vya habari nchini humo.
Jamaa na marafiki ambao walikusanyika katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi hawakuweza pia kuficha hisia zao wakati Wanjiru alipoangua kilio.
"Nililia kwa uchungu Eh Mungu! Mungu wangu eh nimefanya nini oh Mola Wangu hadi kustahili haya. Nimekukosea nini eh Mungu hadi kuchukua wanawangu niwapendao, na mimi napiga magoti kila siku kukushukuru kwa mengi ulionifanyia,"anakumbuka Lucy
Anasema kwamba alizimia mara kadhaa wakati ambapo alikuwa anaelekea kwenye gari ambalo lilitumiwa kumsafirisha kutoka uwanja wa ndege hadi nyumbani kwake.
Mama huyu alikabiliwa na wakati mgumu sana hasa wakati gari hilo lilipoelekea mtaa wa Syokimau anakoishi katika jimbo la Machakos viungani mwa mji wa Nairobi.
Anakumbuka akimuomba kaka yake ageuze gari na kurudi walikotoka kwani hana nguvu ya kuingia nyumbani kwake kutokana na kumbukumbu nzito za kukubali kwamba wanawe wawili wamemtoka.
Bi Lucy anasema kwamba ilibidi kaka yake amtafutie sehemu nyingine ya kukaa kabla ya kwenda hadi makafani ya Kenyatta ambapo miili ya wanawe ilikuwa imehifadhiwa.
Fredrick Mureithi angekuwa hai leo hii angekuwa na miaka 27 na kaka yake mdogo Victor mwangi angekuwa na miaka 22.
Mazingira ya kuuawa kwa vijana hao
Karibu mwaka mmoja uliopita ndugu hao wawili waliuawa eneo la Kitengela baada ya kundi la watu kuwadhania kuwa majambazi waliokuwa wakihangaisha wenyeji eneo hilo. Mauaji hayo yalifanyika mnamo agosti tarehe 7 mwaka uliopita wa 2021.
Vijana hawa walifariki katika njia ya kuhofisha baada ya watu wasiojulikana kutoka kijiji hicho kuwashambulia kwa mapanga na silaha nyengine butu.
Mama yao anasema kwamba vijana hao waliuawa wakati alikuwa wamezuru eneo hilo kujivinjari kwa pikipiki zao kama sehemu ya sherehe za siku ya kuzaliwa kwa mmoja wao.
Mpango uliokuwa uwe wa furaha uligeuka ghafla na kuwa msiba ambao umemuacha mama huyu na maswali mengi kuliko majibu .
Sherehe ya kuzaliwa kwa Victor ilikuwa imepangiwa kufanyika eneo mmoja huko kabla ya kifo hicho cha kikatili kuwakuta.
Japo kuna washukiwa waliokamatwa na kesi inaendelea mahakamani hadi sasa na mama huyu akitumai kwamba haki kwa upande wake itatendekea
Mama huyu anasema habari alizoelezwa na ambazo ziko katika baadhi ya vyombo vya habari nchini Kenya ni kwamba Wanne hao walipigwa hadi kufariki kwasababu wakaazi waliwadhania walikuwa wezi wa mifugo, nyaraka zao pamoja na pikipiki walizokuwa nazo wakati waliponaswa ziliteketezwa moto.
Miili yao ilipatikana siku mbili baadaye ikiwa na mikuki vichwani mwao, mifupa mingi ilikuwa imevunjika pia .Ripoti za uchunguzi pia zilisema kwamba walikuwa wameteswa kabla ya mauaji hayo.
"Nakumbuka siku mbili kabla ya kifo cha wanangu nilizungumza na wao nikiwa Uingereza, na ni mimi niliwatumia pesa za kuandaa sherehe hio ya kuzaliwa kwa mwanangu wa mwisho Victor , nisijue kwamba ilikuwa siku ya mwisho kuwasikia tena.
Baada ya hapo juhudi za kuwapigia simu kuwasiliana nao ikawa shida nisijue kwamba walikuwa wameuawa "Lucy anakumbuka
Kukabiliana na hofu ya vifo vya wanawe
Haijakuwa rahisi kwa Lucy kukubali kwamba hatawahi kuwaona wanawe tena. Lucy anasema kwamba amekuwa mzazi wa kipekee kwa wanawe hawa baada ya ndoa kati yake na baba ya wanawe kukumbwa na changamoto zilizosababisha iwe vigumu kwa wao kuishi pamoja .
Lucy anasema kwamba kila siku anawafikiria wanawe na wakati mwengine anajipata akilia kwa masikitiko.
Kwa sasa anapokea ushauri kutoka kwa mwanasaikolojia na hali kadhalika mtoa nasaha, lakini anasema kwamba licha ya kuwa na ukakamavu bado moyo unakuwa mzito sana kukubali hali hali ya kuondokewa na wanawe.
Anachofanya zaidi ni kuhakikisha kwamba mawazo haya hayamkoseshi amani ni kujipa shughuli chanya kwa mfano alikuwa hafugi kuku ila kwa sasa ameanza kuwafuga, ukulima kidogo na pia kuhakikisha kwamba anakaa karibu na marafiki ambao wamemsaidia kukubali hali yake na kuendeleza maisha yake.
Mama huyu anasema hakuna kitu kigumu kama mzazi kuwapoteza watoto wake wote akiwa hai.
"Kwangu mimi kuna wakati naona maisha hayana maana kabisa, yaani jitihada zangu nchini Kenya na hata Uingereza, ili niwasomeshe wanangu ni kama ziliambulia patupu "anasema Lucy.