Sudan yashtushwa na kurejea kwa wafuasi wa Bashir na NCP

Chanzo cha picha, AFP
Miaka mitatu baada ya Rais wa Sudan Omar al-Bashir kuondolewa madarakani kupitia maandamano ya umma, wanachama wa zamani wa chama chake cha National Congress Party (NCP) wanapewa nyadhifa zenye ushawishi mkubwa na utawala wa kijeshi, jambo linalozua hofu kwamba wanarejea kisiasa.
Serikali dhaifu ya mpito ilivunjsa mwaka jana baada ya Jenerali Abdel-Fattah Burhan kufanya mapinduzi dhidi ya washirika wake wa kiraia, ambao walikuwa na jukumu muhimu katika maandamano makubwa ya kupinga utawala wa kimabavu wa Bashir.
Wengi wanaona majenerali wakuu - wajumbe wote wa kamati ya usalama iliyoteuliwa na Bashir katika siku za mwisho za utawala wake - kuwa wanapendelea NCP, ambayo iliweka Sharia kali (sheria za Kiislamu) wakati wa utawala wake.
Hamza Balol - mwanachama mkuu wa vugu vugu la Forces for Freedom and Change (FFC) linalounga mkono demokrasia, ambalo liligawana madaraka na majenerali hadi wakati wa mapinduzi- anaamini kuwa jeshi limeharibu mpito kwa kulinda NCP.
Amesema kiongozi wa mapinduzi amekuwa "akishirikiana kwa karibu na viongozi wa utawala uliopita ili kupata msingi wa kisiasa".
"Majeshi yaliyochochea mapinduzi lazima yaungane ili kuyashinda mapinduzi," Bw Balol aliambia BBC.
Zaidi ya watu 100 wameuawa tangu mapinduzi ya Oktoba mwaka jana katika maandamano ya mara kwa mara ya kutaka kurejeshwa kwa utawala wa kiraia.
Mojawapo ya maagizo ya kwanza yaliyotolewa na Jenerali Burhan kufuatia mapinduzi hayo ni kusimamisha kazi ya kamati iliyoundwa "kusambaratisha" utawala wa zamani wa kung'ang'ania madaraka, na kubadili maamuzi yake yote.
Kamati hiyo - inayoongozwa na wakili Wajdi Saleh, ambaye alizuiliwa baada ya kuchukua mamlaka ya kijeshi - ilisaidia sana kufichua ufisadi uliokuwa umekithiri chini ya Bashir.
Ilitaja maafisa wafisadi na wafanyabiashara, iliwafuta kazi watumishi wa umma, ikatangaza kukamata mali, ilitoa hati za kukamatwa, kufungia akaunti za benki, na ilikuwa ikichunguza shughuli kati ya uongozi wa NCP na majenerali wa jeshi wakati mapinduzi yalipofanywa.
Kamati hiyo ilikuwa na wakosoaji wake - wengine walisema ilifanya kazi kinyume cha sheria, huku wengine wakisema imekuwa chombo cha kutoa adhabu zisizo za haki.

Chanzo cha picha, Getty Images
Baada ya mapinduzi, uongozi wa kijeshi uligeukia NCP na wafuasi wake ili kuimarisha kwenye mamlaka.
Mamia ya wafanyikazi walioachishwa kazi walirejea kazini katika benki kuu, mahakama, idara ya mashtaka, shirika la utangazaji la serikali na wizara za serikali.
Wafuasi wa NCP walioteuliwa katika nyadhifa kuu ni pamoja na Jenerali Ahmed Mufdal, gavana wa zamani wa Kordofan Kusini na aliyekuwa kiongozi wa NCP huko.
Sasa ni mkuu wa Huduma ya Ujasusi Mkuu (GIS) - Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi na Usalama ambayo iliogopwa wakati wa utawala wa Bashir.
Katika ishara zaidi ya kurejea kwa NCP katika maisha ya umma, mamia ya akaunti za benki za wanachama wake hazijafungiwa, na baadhi ya wanachama wake wakuu wameachiliwa kutoka kizuizini.
Katika shara zaidi ya kurejea kwa NCP uongozini, mamia ya akaunti za benki za wanachama wake hazijafungiwa, na baadhi ya wanachama wake wakuu wameachiliwa kutoka kizuizini.
Miongoni mwao ni:
- Mkuu wa zamani wa NCP, na waziri wa zamani wa mambo ya nje, Ibrahim Ghandour
- Gavana wa zamani wa Darfur Mashariki Anas Omar, ambaye anatuhumiwa kwa ukiukaji wa haki za binadamu
- Mhubiri Muhammad Ali Al-Jizouli ambaye wakati mmoja aliunga mkono wanamgambo wa kundi la Islamic State (IS)
Bashir mwenyewe, hatahivyo, bado ni mfungwa kijeshi. Alipatikana na hatia ya ufisadi mwaka wa 2019, na amekuwa akishikiliwa tangu Julai 2020 kupitia mapinduzi ambayo yalimuweka madarakani kwa mara ya kwanza mwaka wa 1989. Hili ni jambo ambalo vuguvugu linalounga mkono demokrasia ilishinikiza, na kesi ilianza kabla ya Jenerali Burhan kunyakua mamlaka. .
Utawala wa kijeshi umekata kumwasilisha Bashir kwa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa jinai ICC ili afunguliwa mashataka ya uhalifu wa kivita katika mzozo wa Darfur, madai ambayo anakanusha.
Baadhi ya wachambuzi wanaamini majenerali hatimaye watamuachilia Bashir, kama vile Rais aliyepinduliwa wa Misri Hosni Mubarak aliachiliwa baada ya jeshi kuchukua madaraka mwaka 2013.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kiongozi wa NCP Ali Karti, ambaye pia ni kaimu katibu mkuu wa Vugu vugu la Kiislam la Sudan, muungano mpana wa makundi ya Kiislamu, anadhaniwa nyuma ya kufufuka kwa NCP.
Kwa sasa anaishi Uturuki, Bw Karti hivi majuzi alifanya mahojiano yake ya kwanza ya Televisheni katika zaidi ya miaka mitatu. Alitetea NCP na kusema Waislam walikuwa na haki ya kujipanga upya na kugombea uchaguzi ujao.
Waziri wa zamani wa mambo ya nje, Bw Karti pia alikuwa mmoja wa watu mashuhuri ambao walilengwa na kamati ambayo ilikandamiza wanachama wa utawala wa Bashir.
Mamia ya viwanja vilivyosajiliwa chini ya jina lake vilitwaliwa huko Khartoum Kaskazini, na kusababisha baadhi ya maeneo hayo kupaita eneo la Kartistan. Alikana kosa lolote.
Alisifika kuwa miongoni mwa mwewe katika utawala wa Bashir, na alianzisha Jeshi la Ulinzi maarufu, wanamgambo walioundwa katika kilele cha ushawishi wa serikali ya Kiislamu katika miaka ya 1990.
Ilisaidia kupigana vita dhidi ya Sudan People's Liberation Movement (SPLM), wakati ilipokuwa ikidai uhuru wa eneo ambalo hasa ni la Kikristo ambalo sasa ni Sudan Kusini.

Chanzo cha picha, Getty Images
Waziri wa zamani wa habari wa Bashir, Amin Hassan Umar, pia alifanya mahojiano hivi karibuni, na kudai kuwa vuguvugu la Kiislamu lilikuwa na wapiganaji 500,000 walio tayari kuilinda Sudan dhidi ya tishio lolote.
Hakuna uthibitisho huru wa madai yake, lakini kama Waislam wana wanaume 500,000 chini ya amri yao, watakuwa wengi zaidi ya Rapid Support Forces (RSF), kundi la wanamgambo linaloundwa na wanamgambo wa Janjaweed wanaotuhumiwa kwa ukatili ulioenea katika mzozo wa Darfur.
Makadirio ya idadi ya wapiganaji wa RSF yanatofautiana sana, kutoka 50,000 hadi 150,000.
Baadhi ya wachambuzi wanaamini kwamba viongozi wakuu wa jeshi, akiwemo Jenerali Burhan, wanawatumia Waislam kuzuia ushawishi unaoongezeka wa kamanda wa RSF Jenerali Muhammad Hamdan Dagalo, ambaye kwa sasa ni naibu wa kiongozi huyo wa mapinduzi.
Jeshi limeahidi uchaguzi mwaka ujao, na kisha kukabidhi mamlaka kwa serikali ya kiraia.
Marekani na Saudi Arabia wanafanya mazungumzo yasiyo rasmi kati ya majenerali na FFC katika jitihada za kusuluhisha tofauti, lakini kamati za upinzani - zinazoundwa na wanaharakati wa ngazi ya chini ambao wamekuwa mstari wa mbele katika maandamano dhidi ya mapinduzi - bado wanashuku jeshi na maandamano yanaendelea.
Wanahofia kwamba majenerali wakuu watatumia mazungumzo kupata uhalali wa lengo lao kuu - kuandaa uchaguzi wa uongo, ambao ungeshuhudia kambi mpya ya Kiislamu - ambayo itajumuisha NCP iliyobadilishwa jina - kuchukua mamlaka.
"Wao [NCP] wangependelea kugombea uchaguzi kwa maslahi yao. Huu ndio wasiwasi," Jonas Horner, mchambuzi mkuu wa shirika la kimataifa la kupambana na majanga International Crisis Group.
Kwa hivyo, kamati za upinzani zinataka wanajeshi kurejea kambini, na kwa serikali mpya ya mpito kuiongoza Sudan kwenye uchaguzi wa kidemokrasia.
Haijulikani iwapo watafanikisha lengo hili, lakini wana uwezekano wa kuweka shinikizo kwa FFC kutofanya makubaliano mapya ya kugawana madaraka na jeshi.
Pia unaweza kusoma :














