Uchaguzi kenya 2022: Mcheshi pamoja na mgombea anayepigania kuhalalishwa kwa bangi kuwania urais Kenya

Chanzo cha picha, @glwajackoyah
- Author, Abdalla Seif Dzungu
- Nafasi, BBC Swahili
- Iliyochapishwa
Mwanasiasa anayefanya kampeni ya kuhalalisha bangi nchini Kenya ameruhusiwa kugombea urais katika uchaguzi mkuu ujao wa Agosti.
George Wajackoyah, wakili na profesa wa sheria, amejaribu kugombea kiti hicho bila mafanikio makubwa.
Lakini wakati huu, ujumbe wake wa kuunga mkono bangi umegonga vichwa vya habari tangu alipofanya hili jukwaa lake mwezi Februari.
Ameanzisha chama cha kisiasa kwa jina Roots ambacho kinaitaka Kenya kuruhusu kukuza bangi ili kusaidia kulipa deni kubwa la nchi.
Mapema wiki hii, usajili wake wa kugombea urais ulikataliwa na tume ya uchaguzi IEBC kwa kukosa sahihi za kutosha.
Hata hivyo siku ya Alhamisi, aliwasilisha tena makaratasi yake huku tume ya uchaguzi ya IEBC ikimuhidhinisha kuwania wadhfa huo.
Harakati za kuwania urais zimekuwa zikionekana kuwa kati ya farasi wawili naibu rais William Ruto na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga.
Hata hivyo, mgombea wa chama cha Roots, ambaye ana hadithi ya ajabu ya Maisha yake - akitoka kuishi katika mitaa ya mji mkuu, Nairobi, aalipokuwa mtoto hadi kuwa wakili anayeheshimika na angalau digrii sita - anachangamsha kampeni na kufungua mjadala juu ya bangi.
Wakati huohuo aliyekuwa mcheshi Walter Mong'are maarufu Nyambane ameruhusiwa kuwania urais na Tume ya uchaguzi nchini Kenya IEBC.
Huku baadhi ya wagombea akiwemo gavana mmoja wa eneo la mkoa wa kati akilalamika kufungiwa nje katika kinyang'anyiro hicho, Bwana Mongare alikuwa akitabasamu alipoondoka katika ukumbi wa Bomas of Kenya na hata akapata muda wa kumuigiza aliyekuwa rais wa Kenya rais Daniel Moi muda mfupi baadaye.
Bwana Mongare alianzisha ucheshi wake kupitia kuigiza sauti ya rais huyo wa awamu ya pili wa Kenya mapema miaka ya 2000. Alikuwa miongoni mwa wachekeshaji wa kundi la Reddykyulas , kundi la watu watatu ambalo lilichangamsha Wakenya kupitia ucheshi katika siasa.
Wachekeshaji wengine wawili waliokuwa katika kundi hilo walikuwa Bwana Tony Njuguna na bwana John Kiarie, ambaye kwasasa ni mbunge wa eneo bunge la Dagoretti Kusini .

UNAYOFAA KUJUA:Uchaguzi Kenya 2022: Je Naibu wa rais wa Kenya William Ruto anakabiliwa na changamoto gani katika kumteua naibu wake wa rais?

Katika kipindi cha miaka mitano iliopita bwana Mong'are amekuwa akifanya kazi katika ofisi ya rais akiwa mshauri.
''Nataka kumwambia rais Uhuru Kenyatta kwamba uchaguzi huu sio mashindano kati yangu na yeye , najaribu kuwa kiongozi bora kama alivyotufunza ili kuweza kurudi katika Ikulu ya Rais'', alinukuliwa akisema na gazeti la the standard.
Mfahamu Mcheshi Walter Mong'are

Chanzo cha picha, Walter Mong'are facebook
Kabla ya kufanya kazi katika ofisi ya rais, bwana Mong'are alihudumu katika shirika la matangazo nchini Kenya KBC akiwa mkuu wa vipindi kabla ya kufanyakazi katika serikali ya kaunti ya Kisii kama mkuu wa mawasiliano. Pia amewahi kufanya kazi katika redio ya Kiss Fm akiwa mtangazaji.
Bwana Mongare vilevile amewahi kuwa msanii ambapo aliweza kutoa vibao kama vile 'Sweet banana' na 'baby J nyamba' akishirikiana na Talia Oyando.
Mchekeshaji huyo atawania urais kupitia tiketi ya chama cha Umoja Summit party chenye nembo ya chungu.
Anasema kwamba uwaniaji wake umeshawishiwa na rais wa Ukraine anayepigana vita dhidi ya Urusi Volodymyr Zelensky , ambaye pia aliwahi kuwa mcheshi.
''Zelensky alikuwa akiigiza jinsi rais alivyokuwa akizungumza na kufanikiwa kuwa rais'', alisema Mong'are akinukuliwa na gazeti la The Standard.












