Moja kwa moja, Hatua za mwisho kuelekea makubaliano, Marekani na Iran wasubiri kutia saini hati ya maelewano

Trump ameonya kuwa iwapo makubaliano hayo hayataanza kutekelezwa haraka na kikamilifu, kuna uwezekano wa kurejelewa kwa matumizi ya nguvu za kijeshi.

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. FIFA kumlipa Omar Artan licha ya kukosa kushiriki Kombe la Dunia

    Omar Artan amekuwa mwamuzi wa FIFA tangu 2018.

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Omar Artan amekuwa mwamuzi wa FIFA tangu 2018.

    Mwamuzi Omar Artan, ambaye alinyimwa ruhusa ya kuingia nchini Marekani kwa ajili ya kuchezesha mechi za Kombe la Dunia, atalipwa ada yake yote ya mashindano hayo.

    Vyanzo vimeiambia BBC Sport kuwa ingawa Omar Artan hatashiriki katika Kombe la Dunia, FIFA imeahidi kumlipa mshahara wake kikamilifu.

    Waamuzi kwa kawaida hawajui kiwango halisi cha fedha watakacholipwa kwa kuchezesha mechi za Kombe la Dunia, kwani malipo hayo hutolewa baada ya mashindano kukamilika.

  2. New York Knicks watwaa ubingwa wa NBA baada ya miaka 50

    h

    Chanzo cha picha, Dustin Safranek-Imagn Images TPX IMAGES OF THE DAY

    Klabu ya mpira wa kikapu ya New York Knicks wameandika historia baada ya kushinda ubingwa wa mwaka huu wa ligi kuu ya NBA kwa mara ya kwanza baada ya zaidi ya miaka 50, baada ya kuilaza San Antonio Spurs kwa vikapu 94-90 katika mchezo wa tano wa fainali za 7 bora.

    Ingawa mchezo huo ulifanyika Texas katika ukumbi wa Frost, mashabiki wa New York walifurika mitaani kusherehekea ushindi huo.

    Shabiki mmoja Max alisema haijalishi kuwa ubingwa umepatikana Texas badala ya Madison Square Garden kwa sababu “New York yote kwa sasa inasherehekea.”

    Ushindi huo umeonekana kama mabadiliko makubwa kwa Knicks baada ya miaka mingi ya kufanya vibaya kwenye ligi.

    Mara ya mwisho timu hiyo kucheza fainali ilikuwa mwaka 1999 dhidi ya Spurs, lakini ilishindwa. Ubingwa wao wa mwisho ulikuwa mwaka 1973.

    Rais wa Marekani Donald Trump pia aliipongeza Knicks pamoja na mmiliki wake Jim Dolan.

    “Umekuwa mwaka wa kipekee sana lakini zaidi ya yote, tumeshuhudia ushindi wa ajabu katika hatua ya muondoano, hasa michezo minne ya mwisho huenda ndiyo michezo bora zaidi kuwahi kutokea katika historia ya mpira wa kikapu.” Trump

    G

    Chanzo cha picha, Geoff Burke-Pool Photo via Imagn Images

  3. Rais wa Somaliland Irrawaddy afanya ziara yake ya kwanza nchini Israel

    G

    Chanzo cha picha, X

    Rais wa Somaliland, Abdirahman Mohamed Abdullahi almaarufu Irro, ametua katika Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion mjini Tel Aviv kwa ziara ya kwanza rasmi kabisa ya kiongozi wa Somaliland nchini Israel.

    Ziara hiyo imekuja miezi michache baada ya Israel kuwa taifa la kwanza mwanachama wa Umoja wa Mataifa kutambua rasmi uhuru wa Somaliland mnamo Desemba 2025.

    Kwa mujibu wa Balozi wa Somaliland nchini Israel, Mohammed Hagi, Rais Irro anatarajiwa kufanya mazungumzo rasmi na Rais wa Israel, Isaac Herzog, pamoja na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.

    Mazungumzo hayo yatahusisha ushirikiano katika siasa, usalama, biashara, uwekezaji, teknolojia na maendeleo ya uchumi.

    Rais huyo pia anatarajiwa kukutana na zaidi ya wawekezaji na wafanyabiashara 200 wa Israel, kutembelea vituo vya teknolojia na maeneo muhimu ya kihistoria.

    Aidha, atazindua ubalozi wa kwanza wa Somaliland mjini Jerusalem, ikiwa ni ubalozi wa kwanza kufunguliwa katika taifa lililotambua rasmi uhuru wa Somaliland.

    Ziara hiyo inafuatia safari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Gideon Sa’ar, mjini Hargeisa mapema mwaka 2026 pamoja na kuwasilishwa rasmi kwa balozi wa kwanza wa Somaliland nchini Israel.

    Rais Irro ameielezea Israel kama mshirika muhimu, huku akionyesha nia ya kushirikiana katika sekta mbalimbali ikiwemo uwekezaji wa madini na teknolojia.

    Kwa upande wa Israel, ushirikiano huo unaipa mshirika mpya katika eneo muhimu la upeembe wa Afrika na Bahari ya Shamu.

    Kwa Somaliland, ambayo ilijitangazia uhuru kutoka Somalia mwaka 1991 lakini bado haijatambuliwa na mataifa mengi duniani, hatua hiyo inaonekana kama fursa ya kuimarisha uhalali wa kidiplomasia na kupata manufaa ya kiuchumi.

    Hata hivyo, Somalia imepinga vikali uhusiano huo kwa kuungwa mkono na Umoja wa Afrika, Shirikisho la mataifa ya kiarabu (Arab League) na Muungano wa mataifa ya kiislamu Organisation of Islamic Cooperation.

    Soma zaidi:

  4. Israel yafanya mashambulizi ya anga katika maeneo kadhaa kusini mwa Lebanon

    h

    Chanzo cha picha, Reuters

    Lebanon imesema Israel imefanya mashambulizi ya angani katika maeneo kadhaa kusini mwa nchi hiyo leo, baada ya jeshi la Israel kutoa onyo la kuhamishwa kwa wakazi wa mji wa Nabatieh na zaidi ya makazi 20 mengine kusini mwa Lebanon.

    Shirika la Habari la Lebanon liliripoti kuwa mashambulizi hayo yalilenga maeneo mbalimbali, hususan maeneo yanayozunguka mji wa Nabatieh.

    Mpiga picha wa AFP aliyekuwa eneo la Nabatieh alisema alisikia milipuko kadhaa katika eneo la Kafr Raman na kuona moshi ukifuka kutoka eneo la Kafr Benit.

    Jeshi la Lebanon pia lilitangaza kuwa mmoja wa wanajeshi wake alijeruhiwa vibaya katika shambulio la ndege isiyo na rubani ya Israel kwenye barabara inayounganisha Kafr Raman na Nabatieh.

    Shirika hilo la habari liliongeza kuwa shambulio jingine lilimuua afisa mmoja wa serikali za mitaa katika eneo la Rayhan kusini mwa Lebanon.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Morocco yajiondoa kuwania uenyeji wa mashindano yoyote ya Afrika

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Morocco imetangaza kuwa haitawasilisha tena maombi ya kuandaa mashindano ya soka ya Afrika kwa sasa, badala yake ikielekeza juhudi zake katika maandalizi ya matukio makubwa ya soka duniani yanayotarajiwa kufanyika katika miaka ijayo.

    Akizungumza kwenye jukwaa la Al Jazeera 360, Rais wa Royal Moroccan Football Federation, Fouzi Lekjaa, amesema kuwa azma ya Morocco ya kuandaa mashindano katika siku zijazo itajikita kwenye michuano ya FIFA, ikiwemo Kombe la Dunia na Kombe la Dunia la Klabu, badala ya mashindano ya bara la Afrika.

    “Morocco haitawasilisha tena maombi ya kuandaa mashindano yoyote ya Afrika. Mataifa mengine yakitaka kuyaandaa, yako huru kufanya hivyo,” alisema Lekjaa.

    Morocco itakuwa mwenyeji mwenza wa Kombe la Dunia la 2030 pamoja na Spain na Portugal, hatua itakayoifanya kuwa taifa la kwanza la Afrika Kaskazini kuandaa mashindano hayo makubwa ya soka duniani.

    Hata hivyo, viongozi wa soka nchini humo wanaamini kuwa maandalizi ya mashindano hayo makubwa ya kimataifa yanahitaji umakini na rasilimali nyingi ili kuhakikisha yanafanyika kwa mafanikio.

    Tangazo hilo linaashiria mabadiliko makubwa kwa Morocco, taifa ambalo limekuwa miongoni mwa waandaaji wakuu wa mashindano ya soka barani Afrika katika miaka ya karibuni.

    Morocco iliandaa kwa mafanikio 2025 Africa Cup of Nations baada ya kutunukiwa uenyeji na shirikisho la soka barani Afrika CAF.

  6. Fars: Uamuzi wa mwisho kuhusu hati ya maelewano bado haujafikiwa

    t

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Shirika la Habari la Fars limemnukuu “chanzo chenye taarifa za ndani kilicho karibu na timu ya mazungumzo” kikisema kuwa Iran bado haijatangaza uamuzi wake wa mwisho kuhusu rasimu ya hati ya maelewano iliyopendekezwa.

    Kwa mujibu wa ripoti hiyo, “uchambuzi wa vipengele vya kisiasa, kisheria na kiufundi vya mapendekezo bado unaendelea.”

    Shirika hilo, ambalo linaelezwa kuwa karibu na taasisi za kijeshi na usalama, limesema kuwa “uchambuzi wa pande mbalimbali za mapendekezo yaliyowasilishwa bado unaendelea katika ngazi ya wataalamu na maamuzi, na taasisi husika zinaendelea kuyapitia kwa makini vipengele vya kisiasa, kisheria na kiufundi vya suala hilo.”

    Wakati huo huo, saa moja iliyopita, ujumbe kutoka Qatar uliwasili Tehran kuendeleza mchakato wa kubadilishana ujumbe kati ya Iran na Marekani.

    Soma zaidi:

  7. Uingereza yakamata meli ya mafuta ya Urusi iliyokuwa ikipita katika Mfereji wake

    G

    Chanzo cha picha, Reuters

    Uingereza imesema vikosi vyake vya kijeshi vimeikamata meli ya mafuta inayodaiwa kuwa sehemu ya mtandao wa “meli za kivuli” za Urusi katika Mfereji wa Uingereza mapema ya leo.

    Katika operesheni iliyochukua takribani saa sita, makomandoo wa Jeshi la Majini la Kifalme na maafisa wa utekelezaji wa sheria waliobobea kutoka Shirika la Kitaifa la Uhalifu waliipanda meli hiyo, kwa msaada wa Jeshi la Anga la Kifalme.

    Meli hiyo, Smyrtos, itashikiliwa na kufuatiliwa karibu na pwani ya kusini ya Uingereza wakati uchunguzi ukiendelea, Wizara ya Ulinzi ilisema katika taarifa.

    Waziri Mkuu Keir Starmer amesema:

    “Operesheni hii yenye mafanikio imeipiga tena Urusi pigo jingine na kuwakumbusha wanaofadhili vita vya Putin nchini Ukraine kwamba hatutawaacha wajifiche.”

    Urusi imekuwa ikiendesha mtandao wa “meli za kivuli” ili kukwepa vikwazo vya kimataifa vilivyowekwa dhidi ya mauzo yake ya mafuta.

    Wizara ya Ulinzi ya Uingereza imesema mtandao huo unao zaidi ya meli 700 unahusika na kusafirisha takribani asilimia 75 ya mafuta ya Urusi yaliyo chini ya vikwazo, na hivyo kuwa njia muhimu ya kuiwezesha Kremlin.

    Waziri mkuu alitangaza mwezi Machi kwamba vikosi vya Uingereza sasa vina uwezo wa kupanda meli zilizowekewa vikwazo zinazopita katika maji ya nchi hiyo.

    Wizara ya Ulinzi pia ilisema Uingereza tayari imeziwekea vikwazo zaidi ya meli 500.

  8. Korea Kaskazini yawajibu Marekani, Japan na Korea Kusini kuhusu kuharibu silaha za nyuklia

    f

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Korea Kaskazini imesema hadhi yake kama taifa lenye silaha za nyuklia ni "isiyoweza kubadilishwa" na imekataa wito mpya wa kuachana na ghala lake la silaha za nyuklia.

    Pyongyang ilitoa kauli hiyo katika taarifa iliyojibu mkutano wa maafisa wa Korea Kusini, Japan na Marekani uliofanyika Ijumaa, ambapo washirika hao walithibitisha tena dhamira yao ya kuifanya Rasi ya Korea kuwa eneo lisilo na silaha za nyuklia.

    Korea Kaskazini imezitaja kauli hizo kuwa "mazungumzo yasiyo na mantiki" na "ndoto zisizoweza kutimia."

    Katika taarifa hiyo, Pyongyang pia ilitaja mauzo ya mifumo ya silaha ya Washington kwa Seoul na Tokyo kuwa sababu mojawapo ya kuendelea na mpango wake wa nyuklia.

    Korea Kaskazini imeongeza kasi ya maendeleo ya silaha zake za nyuklia katika miaka ya karibuni baada ya mazungumzo kati yake na Marekani kuvunjika mwaka 2019.

    Soma zaidi:

  9. Guyana yampendekeza balozi wake kuwania ukatibu mkuu wa Umoja wa Mataifa

    Carolyn Rodrigues-Birkett amekuwa mwakilishi wa Guyana katika Umoja wa Mataifa tangu mwaka 2020.

    Chanzo cha picha, Wizara ya mambo ya kigeni ya Guyana

    Maelezo ya picha, Carolyn Rodrigues-Birkett amekuwa mwakilishi wa Guyana katika Umoja wa Mataifa tangu mwaka 2020.

    Guyana imemteua balozi wake katika Umoja wa Mataifa kugombea wadhifa wa Katibu Mkuu wa Umoja huo wa kimataifa, jambo lililotangazwa na Rais wa taifa hilo la Amerika Kusini, Irfaan Ali, usiku wa Ijumaa.

    Katibu Mkuu wa sasa wa Umoja wa Mataifa, António Guterres wa Ureno, anatarajiwa kuondoka madarakani mwishoni mwa mwaka huu baada ya kuhudumu kwa mihula miwili tangu mwaka 2017.

    Carolyn Rodrigues-Birkett amekuwa mwakilishi wa Guyana katika Umoja wa Mataifa tangu mwaka 2020.

    Guyana ni taifa la pwani ya Bahari ya Atlantiki lililopo kati ya Venezuela na Brazil, lenye idadi ya watu isiyofikia milioni moja.

    Akizungumza katika hotuba yake, Rais Ali alisema maono ya Rodrigues Birkett kwa Umoja wa Mataifa yanajikita katika kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, kuongeza ufanisi na mwitikio wa taasisi hiyo, kukuza utawala jumuishi wa dunia na kuhakikisha Umoja wa Mataifa una uwezo wa kukabiliana na changamoto za kisasa.

    Ali pia alisifu uongozi wa balozi huyo mwenye umri wa miaka 52 wakati Guyana ilipohudumu kwa muhula wa miaka miwili kama mwanachama asiye wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kati ya mwaka 2024 na 2025.

    “Uchaguzi wetu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na utekelezaji wenye mafanikio wa muhula wetu wa 2024 hadi 2025 umeonyesha kwa dunia kuwa Guyana inaweza kutoa uongozi katika ngazi mbalimbali za mfumo wa kimataifa,” alisema Ali.

    Rodrigues Birkett aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Guyana kati ya mwaka 2008 na 2015 kabla ya kujiunga na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kama Mratibu Maalumu wa Ushirikiano na Mabunge.

    Mwaka 2017 aliteuliwa kuwa mkuu wa Ofisi ya Mawasiliano ya FAO mjini Geneva, Uswisi, ambako alihudumu hadi mwaka 2020.

    Hadi sasa, hakuna mwanamke aliyewahi kushika wadhifa wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

    Mataifa mengi yanaendelea kushinikiza mwanamke achaguliwe kwa mara ya kwanza kuongoza taasisi hiyo, huku nchi za Amerika ya Kusini zikidai ni zamu yao kwa kuzingatia utamaduni wa mzunguko wa kijiografia katika uteuzi wa nafasi hiyo, ingawa si mara zote kanuni hiyo imekuwa ikifuatwa kikamilifu.

    Miongoni mwa wanaotajwa kuwania nafasi hiyo ni Michelle Bachelet, aliyewahi kuwa Rais wa Chile na Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Rebeca Grynspan wa Costa Rica, pamoja na María Fernanda Espinosa.

    Wagombea wengine waliotangaza nia ni Rafael Grossi kutoka Argentina na aliyekuwa rais wa Senegal Macky Sall.

    Soma zaidi:

  10. Siku ya kuzaliwa ya Trump yaambatana na kutiwa saini kwa makubaliano ya Iran na Marekani

    d

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Marekani, Donald Trump, anatimiza miaka 80 Jumapili ya leo Juni 14, siku ambayo amesema pia itashuhudia kutiwa saini kwa makubaliano yaliyosubiriwa kwa muda mrefu kati ya Marekani na Iran.

    Trump amesema kutiwa saini kwa makubaliano hayo kunaweza kufungua kwa haraka Mlango wa Bahari wa Hormuz na kuanzisha mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, ingawa viongozi wa Iran wameendelea kuonyesha tahadhari na mashaka kuhusu muda wa kutiwa saini kwake.

    Kwa majuma kadhaa, Trump amekuwa akisema kuwa makubaliano hayo yako karibu kufikiwa.

    Wakati huo huo, anasherehekea siku yake ya kuzaliwa kwa hafla kubwa ya mashindano ya UFC katika ikulu ya White House.

    Pia unaweza kusoma:

  11. Tunachojua kuhusu makubaliano yatakayotiwa saini na Marekani na Iran

    f

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Marekani na Iran, kwa upatanishi wa Pakistan, Qatar na mataifa mengine kadhaa, zinatarajiwa kutia saini hati ya maelewano leo.

    Chini ya makubaliano hayo, usitishaji wa mapigano utaongezwa kwa siku 60, Mlango wa Bahari wa Hormuz utafunguliwa tena, na mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran yataanzishwa.

    Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, amesema pande hizo mbili zimekaribia kufikia makubaliano ambayo hayajawahi kushuhudiwa hapo awali, huku maandalizi ya kutiwa saini kwa njia ya kielektroniki yakiendelea.

    Rais wa Marekani, Donald Trump, pia amesema kuwa makubaliano hayo yatatiwa saini leo na kwamba Mlango wa Bahari wa Hormuz utafunguliwa mara moja kwa meli zote za biashara na usafirishaji.

    Aidha, Trump ameonya kuwa iwapo makubaliano hayo hayataanza kutekelezwa haraka na kikamilifu, kuna uwezekano wa kurejelewa kwa matumizi ya nguvu za kijeshi.

    Pia unaweza kusoma:

  12. Uingereza yaunga mkono juhudi za Trump kumaliza mzozo wa Iran

    f

    Chanzo cha picha, Reuters

    Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza imetangaza kuwa Waziri Mkuu Keir Starmer amejadili juhudi za kumaliza mzozo unaohusisha Iran katika mazungumzo ya simu na Rais wa Marekani, Donald Trump.

    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Starmer amekaribisha hatua iliyofikiwa katika mazungumzo hayo na kusisitiza kuwa Uingereza iko tayari kuunga mkono utekelezaji wa makubaliano yoyote ya amani yatakayofikiwa, pamoja na kushirikiana na washirika wa kimataifa kuhakikisha yanafanikiwa.

    Viongozi hao wawili pia wamekubaliana kuhusu umuhimu wa kurejesha uhuru wa usafiri na usafirishaji ili kupunguza athari hasi za mkwamo wa kiuchumi duniani.

    Katika maendeleo mengine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan, Muhammad Ishaq Dar, na mwenzake wa Saudi Arabia, Faisal bin Farhan Al Saud, walifanya mazungumzo kwa njia ya simu kuhusu mwafaka unaojadiliwa kati ya Marekani na Iran.

    Pakistan inaendelea na juhudi za upatanishi kati ya Iran na Marekani, ikisaidia kufanikisha usitishaji wa mapigano na kuwezesha mazungumzo yanayolenga kufikiwa kwa makubaliano ya amani kati ya mataifa hayo mawili.

    Pia unaweza kusoma:

  13. Trump asema makubaliano ya Marekani na Iran kutiwa saini leo, lakini Tehran yatilia shaka muda uliopangwa

    h

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuwa makubaliano ya kumaliza mapigano kati ya Marekani na Iran yanatarajiwa kutiwa saini Jumapili, baada ya Tehran kuonyesha mashaka kuhusu muda wa kufikiwa kwa makubaliano hayo.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii, Trump alisema kuwa Mlango wa Bahari wa Hormuz, njia muhimu ya usafirishaji wa bidhaa kwa meli, utakuwa "wazi kwa wote" mara tu makubaliano hayo yatakapokubaliwa.

    Pakistan, ambayo imekuwa mpatanishi muhimu katika mazungumzo hayo, pia ilisema makubaliano hayo yanatarajiwa kukamilishwa ndani ya saa 24 zijazo na kwamba maandalizi ya kutiwa saini kwa njia ya kielektroniki yanaendelea.

    Kabla ya matamshi ya Trump, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, alionyesha tahadhari kuhusu ratiba hiyo akisema:

    "Tutalazimika kusubiri na kuona tarehe kamili ya kutiwa saini kwa hati ya maelewano, ingawa haitakuwa kesho."

    Katika ujumbe wake kwenye mtandao wa Truth Social, Trump aliandika:

    "Makubaliano hayo yamepangwa kutiwa saini kesho(akirejelea leo), na mara tu yatakapotiwa saini, Mlango wa Hormuz utakuwa WAZI KWA WOTE."

    Akirejelea kile kinachoaminika kuwa akiba ya urani iliyoboreshwa ya Iran, Trump alisema kwamba "wakati mwafaka, hali ikiwa imetulia kabisa, tutaingia na kuchukua mabaki ya nyuklia," akiongeza kuwa baadaye yataharibiwa.

    Kwa miongo kadhaa, Iran imekuwa ikituhumiwa na mataifa ya Magharibi kwa kujaribu kutengeneza silaha za nyuklia. Tehran imekuwa ikikanusha madai hayo na kusisitiza kuwa mpango wake wa nyuklia ni wa matumizi ya amani, ikiwemo uzalishaji wa umeme na shughuli za utafiti.

    Trump pia alionya kwamba iwapo mambo hayataenda "haraka, kwa urahisi na kwa utulivu", Washington ina "njia mbadala ya mwisho kabisa", ambayo alieleza kuwa anatumaini haitalazimika kutumiwa tena.

    Mapema Jumamosi, Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, alisema kuwa "tuko karibu zaidi kuliko wakati wowote kufikia makubaliano ya amani."

    "Tukiwa na matarajio ya kukamilisha makubaliano hayo ndani ya saa 24 zijazo, Pakistan inajiandaa kwa kutiwa saini kwa njia ya kielektroniki mara tu yatakapokamilika, kabla ya mazungumzo ya kiufundi kuanza wiki ijayo," Sharif aliandika kwenye mtandao wa X.

    Ijumaa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Seyed Abbas Araghchi, alisema kuwa makubaliano kati ya Iran na Marekani yako karibu kufikiwa.

    Alisema makubaliano hayo yanatarajiwa kujumuisha kusitishwa kwa mzozo kati ya Israel na kundi la Hezbollah nchini Lebanon.

    Araghchi aliiambia televisheni ya taifa ya Iran kuwa makubaliano hayo pia yanajumuisha kufunguliwa tena kwa Mlango wa Hormuz pamoja na kuondolewa kwa vizuizi vya Marekani dhidi ya bandari za Iran.

    Hata hivyo, alisema mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran yataanza katika hatua ya baadaye.

    Maafisa wa Marekani wamethibitisha baadhi ya vipengele vya makubaliano hayo, wakisema kuwa manufaa ya kiuchumi kwa Iran yatategemea uwezo wa Tehran kutekeleza wajibu wake chini ya makubaliano hayo.

    Ripoti za awali kutoka Marekani zilidokeza kuwa Lebanon huenda isiwe sehemu ya makubaliano hayo, huku Iran ikiripotiwa kusisitiza suala hilo lijumuishwe katika mazungumzo.

    Pia unaweza kusoma:

  14. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya taarifa zinazochipuka. Tutakuletea matukio ya mkataba wa makubaliano ya Iran na Marekani unaotiwa saini Jumapili ya tarehe 14 Juni 2026.