Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Monkeypox: Chanjo dhidi ya ugonjwa huo na mambo mengine ambayo hufanya mlipuko wa sasa usitie watu wasiwasi
Virusi vingine vimesababisha tena wasiwasi ulimwenguni ambao bado haujaibuka kutoka na janga la corona.
Ugonjwa wa Monkeypox, ambao umewaathiri Waafrika kwa karne nyingi, umeanza kuripotiwa katika mataifa kadhaa duniani, ikiwa ni pamoja na Marekani, Canada na mataifa kadhaa ya Ulaya.
Ingawa milipuko hiyo kwa sasa imedhibitiwa, ripoti za visa vipya katika nchi tofauti zimezua wasiwasi katika maeneo mengi.
Hata hivyo, ingawa mamlaka za matibabu zinasema kuwa bado hakuna habari nyingi juu ya mlipuko mpya na njia zinazowezekana za maambukizi, kwa sasa wanahakikisha kwamba hakuna sababu ya hofu au hatari kubwa kwa umma kwa ujumla.
''Ni muhimu kusisitiza kwamba ugonjwa wa monkeypox hausambai kwa urahisi kati ya watu na hatari kwa umma ni ndogo sana,'' Nick Phin, naibu mkurugenzi wa Huduma ya Kitaifa ya Maambukizi katika ofisi ya afya ya umma ya Uingereza alisema.
Michael Head, mtafiti mkuu katika masuala ya afya duniani katika Chuo Kikuu cha Southampton, anasema kwamba ingawa bado kuna mapungufu katika ufahamu kuhusu mlipuko wa sasa, hafikirii watu wanahitaji kuogopa viwango vya maambukizi kama vile vinavyoonekana kwenye janga la corona.
''Nadhani itakuwa nadra sana kwetu kuona zaidi ya visa vichache katika kila mlipuko. Na hakika hatutaona viwango vya maambukizi ya mtindo wa Covid,'' aliambia Kituo cha Vyombo vya Habari vya Sayansi.
Na ni kwamba, tofauti na kesi za kwanza za ugonjwa wa Covid-19 ziliripotiwa, ambayo hakuna chochote kilichojulikana, monkeypox ni ugonjwa unaojulikana, ambao kuna hata chanjo, matibabu na uzoefu wa hapo awali kutoka kwa milipuko ya hapo awali.
Inapaswa pia kukumbushwa katika akili kwamba mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa sasa pia ni ya kisasa zaidi na sasa ni rahisi kutambua na kubaini virusi, ambayo inaweza kumaanisha kuwa pia kuna habari zaidi kuhusu matatizo, magonjwa ya kuambukiza au aina mbalimbali za virusi.
Mamlaka za afya zinaonya, hata hivyo, kwamba hii haimaanishi kuwa tahadhari na hatua hazipaswi kuchukuliwa ili kuzuia kuenea kwa visa zaidi vya ugonjwa huu wa sasa: kwasababu virusi hubadilika mara kwa mara na hakuna kitu kinachohakikishia kuwa mlipuko mmoja utakuwa sawa na mwingine.
Hizi hapa ni baadhi ya sababu kwa nini wataalam wa afya wanaamini kuwa visa vilivyoripotiwa kufikia sasa havina tishio kubwa kwa umma.
1. Ni virusi vinavyojulikana
Wakati kisa cha kwanza cha covid-19 kilipoanza kuripotiwa duniani, moja ya swali kubwa lilikuwa ni aina gani ya viini ilisababisha na nini asili yake.
Ingawa SARS-Cov-2 ilitambuliwa kwa muda mfupi na nadharia kadhaa zinaonyesha kwamba ilipitishwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa wanadamu, bado inajadiliwa ni mnyama gani na jinsi ilipitishwa kwa watu hapo awali.
Tofauti na hali hiyo, virusi vinavyosababisha monkeypox vimejulikana kwa zaidi ya nusu karne, hivyo inajulikana jinsi vinavyofanya kazi na jinsi vinavyoambukizwa.
Ingawa inaaminika kuwa umeathiri watu barani Afrika kwa muda mrefu zaidi, uligunduliwa mnamo mwaka 1958 katika nyani waliohifadhiwa kwenye maabara kwa uchunguzi, na hivyo ndivyo jina la ugonjwa huo lilivyopatikana.
Hata hivyo, tafiti zilizofuata zilionyesha kuwa waenezaji wakuu wa ugonjwa huo walionekana kuwa panya na sio nyani.
''Monkeypox iligunduliwa kwa mara ya kwanza katika nyani miaka ya 1950, lakini ilipofika mwaka 1970 ulienea kwa binadamu. Pia inapatikana kwa wanyama pori wengine kama vile panya, hivyo nyani anaweza asiwe hifadhi kuu ya asili ya virusi. Maambukizi kwa binadamu inadhaniwa kuwa ni kwa sababu ya kumeza wanyama walioambukizwa,'' Simon Clarke, Profesa Mshiriki wa Cellular Microbiology katika Chuo Kikuu cha Reading, aliambia Kituo cha Vyombo vya Habari vya Sayansi.
Watafiti hao wamebaini aina mbili za virusi hivyo, moja kutoka Afrika ya Kati, ambayo husababisha ugonjwa wenye dalili zaidi, na nyingine kutoka Afrika Magharibi, ambayo husababisha ugonjwa usio na nguvu sana na hilo limegunduliwa katika kesi zilizoripotiwa hadi sasa.
Ingawa katika kesi za mlipuko mpya, mamlaka ya matibabu imeeleza kuwa baadhi ya wagonjwa wanafanana kuwa wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume wengine, kwa sasa hakuna ushahidi kwamba virusi hivyo vimebadilika na kuwa aina ya maambukizi ya ngono, ambayo hayakuwa yamejulikana hadi sasa.
2.Kuna chanjo na matibabu yanayopatikana
Kwa kuwa virusi vinavyojulikana ambavyo vimeathiri jamii kwa miongo kadhaa, kuna chanjo na matibabu yanayopatikana.
Kwa kuwa virusi vya monkeypox vinahusiana kwa karibu na kile kinachosababisha ugonjwa wa ndui, chanjo ya ndui pia imeonekana kuwa nzuri kwa magonjwa yote mawili.
Vituo vya Marekani vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) vinaeleza kwenye tovuti yake kwamba ingawa hakuna matibabu mahususi yanayopatikana kwa sasa kwa maambukizi ya ugonjwa wa monkeypox, milipuko inaweza kudhibitiwa kwa kutumia dawa.
Kuna dawa ambazo tayari ziko sokoni na zimeidhinishwa na zimeonyeshwa kuwa na ufanisi dhidi ya ugonjwa huo, kama vile cidofovir, ST-246 na vaccinia immunoglobulin.
Pia kuna chanjo iliyoidhinishwa ya mataifa mengi ya kuzuia na kutibu ugonjwa wa monkeypox, iitwayo JYNNEOSTM (pia inajulikana kama 'Imvamune au Imvanex') na inatolewa na kampuni ya dawa ya Denmark ya Bavarian Nordic.
Takwimu za awali kutoka kwa matumizi yake barani Afrika zinaonyesha kuwa ina ufanisi wa angalau 85% katika kuzuia monkeypox.
Kuna chanjo ya pili ya ndui, ACAM2000, iliyotengenezwa na Emergent Product Development, ambayo pia inaaminika na mamlaka ya matibabu kutoa kinga fulani dhidi ya monkeypox.
Kwa kweli, ni hii ambayo ilitumika katika mlipuko ulioripotiwa mnamo 2003 huko Marekani.
WHO inabainisha kuwa baadhi ya watu waliopokea chanjo ya ndui wanaweza pia kuwa na viwango fulani vya kinga, ingawa katika nchi nyingi chanjo hii ilisitishwa takriban miaka 40 iliyopita wakati ugonjwa huo ulipozingatiwa kuwa umetokomezwa.
Chanjo, katika nchi nyingi, kwa sasa zimeidhinishwa tu kwa watu walio na umri wa zaidi ya miaka 18 ambao wanachukuliwa kuwa katika hatari kubwa ya kuambukizwa ugonjwa huo.
3. Hauambukizi sana
Shirika la Usalama wa Afya la Uingereza linasema kuwa, tofauti na magonjwa mengine ya kuambukiza, monkeypox hausambai kwa urahisi kati ya watu.
Katika milipuko ya hapo awali, mtu aliyeambukizwa alisambaza virusi, kwa wastani hadi kati ya sifuri na mtu mmoja, kwa hivyo viwango vya uambukizaji vimekuwa chini sana.
''Katika hali nyingi, mtu mgonjwa haambukizi virusi kwa mtu mwingine yeyote,'' Jay Hooper, wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Kuambukiza ya Jeshi la Merika, aliiambia NPR katika ripoti ya ugonjwa huo.
Dk Head, kutoka Chuo Kikuu cha Southampton, anaeleza kwamba hii ni kwa sababu virusi vinahitaji mgusano wa karibu sana, wakati mwingine ngozi hadi ngozi, na mtu aliyeambukizwa ili kuambukizwa.
Kulingana na WHO, kiwango cha vifo kwa monkeypox imeanzia 0 hadi 11% katika idadi ya watu kwa ujumla na imekuwa juu zaidi kati ya watoto wadogo.
Kuenea kwa monkeypox kunaweza kutokea wakati mtu anapogusana kwa karibu na mnyama, binadamu au nyenzo zilizo na virusi, ambazo huingia mwilini kupitia ngozi iliyopasuka (hata kama haionekani), njia ya upumuaji, au utando wa (macho), pua au mdomo).
Shirika la Usalama wa Afya la Uingereza linaeleza kuwa kuenea kwa ugonjwa huo kutoka kwa mtu mmoja hadi kwa mwingine ''ni nadra sana'' lakini kunaweza kutokea kwa:
- kugusana na nguo zinazovaliwa na mtu aliyeambukizwa (pamoja na matandiko au taulo)
- kugusa moja kwa moja vidonda au vipele kwenye ngozi ya mgonjwa
- kukohoa au kupiga chafya kwa mtu aliyeambukizwa.
4. Kumekuwa na milipuko kadhaa hapo awali
Kisa cha kwanza cha monkeypox cha binadamu kilirekodiwa mwaka wa 1970 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na milipuko au visa vya maambukizi vimeripotiwa katika nchi kadhaa za kati na magharibi mwa Afrika kwa miongo kadhaa tangu wakati huo.
Ingawa visa vya binadamu kuwa na monkeypox nje ya Afrika ni nadra, vimeripotiwa katika miaka ya hivi majuzi nchini Marekani, Uingereza, Israel na Singapore.
Kwa kweli, huko Uingereza, ambapo kisa cha kwanza cha mlipuko wa sasa kiligunduliwa, wagonjwa walio na ugonjwa huo pia walisajiliwa mnamo 2018, 2019 na 2021.
Milipuko hii yote ambayo imegunduliwa hapo awali nje ya Afrika imekuwa kidogo sana, na watu wachache sana wameambukiz
Katika mlipuko nchini Marekani mnamo mwaka 2003, watu 47 waliugua.
Kuwepo kwa milipuko ya hapo awali huwapa mamlaka ya afya ujuzi sio tu kuhusu njia ambazo virusi vinaweza kuambukizwa, lakini pia uzoefu wa jinsi ya kuvidhibiti, kutibu wagonjwa na kupendekeza njia za kupunguza uambukizaji.
Hata hivyo, mashirika ya afya ya nchi kadhaa yalitangaza kwamba watafuatilia kwa karibu mabadiliko ya kesi mpya, ikizingatiwa kwamba hadi kuwe na data ya kutosha, haiwezi kusemwa kimsingi kuwa hali itakuwa sawa kwa sasa.
Ukweli ni kwamba, hakujawahi kuwa na visa vingi vya ugonjwa wa monkeypox hivyo kurekodiwa kwa wakati mmoja katika nchi kadhaa na bila uhusiano unaowezekana kuanzishwa kati ya watu walioambukizwa na kusafiri kwenda Afrika, kama ilivyo sasa.