Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Somalia nchi ambayo watu 329 pekee wanapiga kura kumchagua rais
- Author, Mohamud Ali
- Nafasi, BBC News
- Iliyochapishwa
Mwishoni mwa Jumapili, Wasomali wanapaswa kujua rais wao ajaye ni nani, lakini kura hii iliyocheleweshwa kwa muda mrefu inahusisha tu wabunge 329 wa nchi hiyo na inafanyika katika eneo lenye ngome nyingi.
Mazingira yasiyo ya kawaida yanaangazia masuala ya usalama wa Somalia, pamoja na ukosefu wa uwajibikaji wa kidemokrasia.
Mji mkuu, Mogadishu, uko katika kizuizi kamili hadi Jumatatu asubuhi.
Mshindi kati ya wagombea 39 pia atalazimika kukabiliana na athari za ukame unaoendelea.
Lakini kazi kubwa ni kunyakua udhibiti wa sehemu kubwa ya Somalia kutoka kwa al-Shabab.
Kundi la wapiganaji wa Kiislamu lenye uhusiano na al-Qaeda linaendelea kutawala sehemu kubwa za nchi na kufanya mashambulizi ya mara kwa mara mjini Mogadishu, na kwingineko.
Serikali ya shirikisho inaungwa mkono katika mapambano yake dhidi ya al-Shabab na Umoja wa Afrika, wenye takribani wanajeshi 18,000, na Umoja wa Mataifa.
Somalia haijawahi kuwa na uchaguzi wa kidemokrasia wa mtu mmoja kwa kura moja tangu mwaka 1969.
Kura hiyo ilifuatiwa na mapinduzi, udikteta na mzozo uliohusisha wanamgambo wa koo na Waislam wenye msimamo mkali.
Kukosekana kwa utulivu ni sababu mojawapo iliyoifanya Somalia kushindwa kufanya uchaguzi wa moja kwa moja.
Hii ni mara ya tatu tu kwa uchaguzi usio wa moja kwa moja wa rais kufanyika nchini Somalia kwenyewe. Zilizotangulia zilifanyika katika nchi jirani za Kenya na Djibouti.
Ni nani anayewania urais?
Miongoni mwa wagombea 39 ni Rais wa sasa, Mohamed Abdullahi "Farmajo", marais wawili wa zamani, Sharif Sheikh Ahmed na Hassan Sheikh Mohamud, na Waziri Mkuu wa zamani, Hassan Ali Kheyre.
Hawa wanne, pamoja na Rais wa eneo la Puntland la Somalia, Sa'id Abdullahi Deni, wanachukuliwa kuwa mstari wa mbele.
Ilani zao zilizingatia utulivu wa kisiasa, kuboresha usalama na mageuzi ya kiuchumi.
Fawzia Yusuf Adam, waziri wa zamani wa mambo ya nje, ndiye mwanamke pekee kati ya wale wanaotaka kazi hiyo ya ngazya juu.
Je, kura itafanyika vipi?
Kura hii ilipaswa kufanyika mwaka jana wakati muhula wa Bw Farmajo wa miaka minne ulipokamilika. Lakini tofauti za kisiasa na ukosefu wa utulivu vilichelewesha uchaguzi na rais akabaki madarakani.
Wabunge ambao watamchagua rais ajaye siku ya Jumapili walichaguliwa wenyewe na wajumbe waliopendekezwa na koo zenye nguvu nchini humo.
Watakusanyika katika hangar kubwa ya uwanja wa ndege katika Kambi ya Halane inayolindwa vyema. Hiki ndicho kituo kikuu cha kijeshi cha ujumbe wa AU nchini Somalia (Atmis), pamoja na makao ya ujumbe wa kidiplomasia na mashirika ya misaada.
Upigaji kura utakuwa kwa kura ya siri na inatarajiwa kuwa kutakuwa na duru kadhaa kabla ya mgombea mmoja kuibuka mshindi.
Wale wanaoacha katika kila duru wanaweza kuwahimiza wafuasi wao kumuunga mkono mgombea mwingine.
Chaguzi zilizopita zilikumbwa na madai ya ununuzi wa kura huku wagombea wakiripotiwa kutoa pesa ili kuungwa mkono.
Je, al-Shabab wamesema nini?
Katika chaguzi zilizopita, al-Shabab waliwatishia na hata kuwateka nyara wazee wa koo baada ya kuwashutumu kwa kushiriki katika kile walichokiona kuwa uchaguzi usio wa Kiislamu.
Safari hii mwitikio wake kwa uchaguzi umekuwa kimya zaidi, huku kukiwa na hofu kwamba huenda wanachama au wafuasi wake walitafuta viti vya ubunge kwa siri kwa nia ya kuhujumu mfumo huo kutoka ndani.
Hofu hiyo ilioneshwa hadharani na Rais wa nchi jirani ya Djibouti Omar Guelleh mwaka wa 2020, aliponukuliwa akisema: "Ninahofia tutaishia kuwa na bunge linalodhibitiwa kwa njia isiyo ya moja kwa moja na al-Shabab kwa sababu watakuwa wamenunua kuungwa mkono na baadhi ya wabunge. ."
Baadhi ya wachambuzi walihisi Bw Guelleh alikuwa akitia chumvi uwezekano wa al-Shabab kupata udhibiti bungeni, lakini hakuna shaka kwamba ni nguvu kuu ya kisiasa nchini Somalia.
Je, ni changamoto gani zinazomkabili rais ajaye?
Juu ya tishio linaloendelea kutoka kwa al-Shabab na hitaji la kuwatimua wanamgambo hao, Somalia inakabiliwa na ukame ambao umezikumba nchi katika eneo zima.
Imezua mzozo wa kibinadamu ambapo Wasomali milioni 3.5 wako katika hatari ya njaa kali, kulingana na UN. Wafugaji ambao wamepoteza mifugo yao wanakwenda mijini kutafuta njia ya kuishi.
Nchi hiyo pia inaathiriwa na mfumuko wa bei wa vyakula na mafuta uliosababishwa na vita nchini Ukraine.
Kuna shinikizo la kukamilisha mchakato wa katiba na kuhakikisha kuwa nchi inakuwa na uchaguzi wa kidemokrasia katika miaka minne ijayo.
Hata hivyo, wapenda madaraka wa Somalia walikubali muda mrefu uliopita kwamba uchaguzi wa kura ya mtu mmoja ungefanyika ifikapo mwaka huu, na walishindwa kutimiza ahadi hiyo.