Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Waridi wa BBC: Jinsi saratani ilivyomfanya mwanamke huyu kupoteza ujauzito mara tisa
Ni simulizi ya Caroline Gathoni , mwanamke wa miaka 28 raia wa Kenya ,Kwa miaka ya utu uzima wake anasema kwamba kwa muda mrefu amezongwa na uchungu mwingi.
Je mahangaiko yake yalianza vipi?
"Natamani ningekuwa na jibu la jinsi nilipata saratani lakini, kwa kweli, sina , Mume wangu na mimi tumekuwa tukijaribu kupata mtoto kwa muda mrefu. sio eti kwamba mimi ni tasa .Ila nilipata mimba, mara tisa, na majaribio yote tisa ya kushika mimba yaliishia kuharibika kwa mimba hizo . Nilijifungua mtoto wangu wa kwanza wa kiume mnamo 2013."anasema Caroline
Wakati huo Caroline anasema kwamba maisha ya ndoa yalikuwa sawa , wakati anajaaliwa mwanae wa kwanza , walijitahidi yeye na mume wake kumlea mwana wao kwa njia bora zaidi .Kabla ya mwaka wa 2018 ulikuwa mwaka mmoja kabla hajajifungua mtoto wao wa pili anasema kwamba aligundua alikua anavuja damu iliyokuwa na harufu kutoka sehemu zake za siri .
Anasema kwamba kipindi hicho alikuwa na ujauzito hivyobasi akaamua kwenda hospitalini kwa uangalizi .
"Kwanza, madaktari waligundua ugonjwa wa candidiasis, ugonjwa wa kuvu unaojulikana kama maambukizi ya uchachu. wakati huo walinipa dawa za kuua viini ili kutibu nakumbuka wakati huo damu ilinitoka kama maji ya bomba. Ningeweza kutumia pakiti moja ya taulo za hedhi kwa siku, hata hivyo, nilikuwa mjamzito. Baadaye, niliambiwa kwamba nilikuwa na ugonjwa wa uvimbe kwenye fupanyonga(pelvic inflammatory disease). Iliathiri safari yangu ya ujauzito na mtoto wangu alizaliwa kabla ya wakati, katika wiki 28"anasema Caroline "
Mwanadada huyu anasema kwamba shinikizo la mtoto wake kuzaliwa kabla ya wakati , ni kwa sababu alipata maambukizi ya bakteria yanayofahamika kwa lugha ya kimatibabu kama chorioamnionitis, ambayo hufanya maji anayoelea mtoto akiwa tumboni kubadiika na kuwa rangi ya kijani .
Hali hio ilikuwa inaashiria mstari mwekundu ikimaanisha kwamba alihitaji upasuaji wa dharura.
Katika chumba cha upasuaji, madaktari waligundua uvimbe mwengine ambao walikata sehemu kidogo ili kufanyia vipimo , wakati huo walidhani ni kitu kama saratani, ila ilibidi wafanyie uchunguzi zaidi .Ila kilichokua akilini mwake ni jinsi mtoto wake aliyekuwa na wiki 28 ataishi licha ya kuzaliwa kabla ya wakati?
" Nilimtazama mtoto wangu ambaye alikuwa kwenye kifaa maalum cha kumsaidia kupumua (incubator) akipigania maisha yake kupitia mashine. Mawazo mengi yalikuwa yanapita akilini mwangu na uwezekano wa kupata saratani uliniogopesha sana. Sikutaka ukweli huo. Licha ya kuwa katika nyanja ya utabibu, sikuamini kuwa siku moja daktari angeniita, na kupasua mbarika kwamba nimegundulika kuwa na saratani katika mlango wa kizazi changu . "anakumbuka Caroline
Caroline anasema kwamba alishtuka kwa habari hizo , ilibidi apige moyo konde kuendelea na maisha yake na hasa kuona kwamba mtoto wake aliyekuwa bado kwenye mashine angeishi.
Mtoto wake alipokomaa waliruhusiwa kutoka hospitalini.
Ila maisha ya ndoa waliporudi nyumbani kutoka hospitalini yalikuwa na changamoto nyingi.
"Ndoa yangu ilichukua njia ile ile ambayo afya yangu ilikuwa imeanza kuzorota, kipigo kingine ambacho sikutarajia . Kulikuwa na mabadiliko sana kwa upande wa mwenza wangu na nilihisi kana kwamba sikuwa nampendeza mume wangu kama hapo awali .Asubuhi moja, baba wa watoto wangu aliamka na kuniomba niondoke nyumbani kwetu pamoja na watoto wangu wawili. Alisema hayo bila kutetereka, nilisalimu amri na kuondoka"anasema Caroline
Asijue kwamba alikuwa tayari ameshika mimba nyengine , kutokana na hali ya saratani yake mtoto wake wa kiume alifariki akiwa tumboni .
Hapo awali mwanadada huyu anasema kwamba alipoteza pacha watatu kabla ya kujifungua na wengine wawili baada ya kujifungua vizuri.
Misukosuko ya kuishi na saratani aina tatu mwilini
Tukio jingine liligunduliwa wakati madaktari walipokuwa wakiweka njia ya kupitisha maji wakati wa upasuaji. Walishuku kwamba Caroline anaweza kuwa na saratani ya damu. Ubashiri wao ulithibitishwa , kwamba alikuwa na leukemia.
"Mnamo Desemba mwaka jana, nilipata pigo lengine la habari mbaya. Kwamba saratani ilikuwa imeenea kwenye maini yangu . Nilikuwa najiuliza , je mambo haya yote yako katika mwili mmoja?'' , anakumbuka Caroline
Licha ya kupashwa habari hizi zote ambazo bila shaka zinahofisha na kuhuzunisha Caroline anasema kwamba kwa sasa hakuna kingine ambacho madaktari wanaweza kufanya , ila kumpa huduma ya kuhakikisha kwamba mwili hauna uchungu mwingi au kile kinachofahamika kama utunzaji wa kuzuia uchungu kwa mgonjwa wa saratani.
Mfahamu Caroline Wanjiru
Caroline Gathoni Wanjiru ni mzaliwa Wa kijiji cha Kihingo, Limuru, Kaunti ya Kiambu.
Unaweza pia kusoma:
- Waridi wa BBC: 'Jinsi kimada alivyoniondoa kwenye nyumba yangu'
- Waridi wa BBC: Ulemavu ulivyompokonya ndoa yake kwa miaka 20
- 'Ndoa yangu ilidumu miezi saba tu niliona mazito ingawaje najilaumu'
- Waridi wa BBC: Kimada alilala kwangu wakati nilipokwenda kujifungua hospitalini
- Waridi wa BBC: 'Jinsi kimada alivyoniondoa kwenye nyumba yangu'
Yeye ni mtoto wa kipekee kutoka kwa mama yake , alilelewa na mzazi mmoja tu. Muda mwingi wa maisha yake aliishi na bibi yake .
Caroline kuna wakati hufikiria sana juu ya afya yake kwani utotoni mwaka alikua kama watoto wengine wenye afya:"Nilikua na afya njema na sikuwahi kuwa na matatizo yoyote ya kiafya. Nilipenda kutunza watu tangu nikiwa mdogo, si ajabu nilichukua taaluma ya uuguzi.
Kabla maisha hayajanibadilikia kwa mshangao wa magonjwa , niliwahi kufanya kazi Hospitalini kama muuguzi ".
Mnamo Aprili 28 mwezi huku mwanadada huyu , atakuwa anatimiza miaka 29 na anasema angetaka kusherehekea siku yake ya kuzaliwa na watu kama yeye, na washiriki wa kikundi chao cha msaada cha Lady Hope.