Nigeria yakumbwa na mshtuko kufuatia vifo katika kiwanda haramu cha kusafisha mafuta - Rais Buhari

Burned-out vehicle

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Picha kutoka eneo la mlipuko inaonyesha magari yaliyoteketea
Iliyochapishwa

Rais wa Nigeria amesema nchi hiyo iko katika "mshtuko na kiwewe" kufuatia vifo vya takriban watu 100 kutokana na mlipuko katika kiwanda haramu cha kusafisha mafuta kinyume cha sheria.

Rais Muhammadu Buhari alielezea tukio hilo katika jimbo la Imo, kusini mwa Nigeria kama "janga na janga la kitaifa".

Wahasiriwa wengi waliteketea kiasi chakutoweza kutambulika.

Polisi sasa wanamsaka mmiliki wa kiwanda hicho kisicho halali cha kusafisha mafuta.

Uharibifu unaokumba uvuvi na kilimo unaosababishwa na sekta ya mafuta kwa miongo kadhaa iliyopita na umetokana na nchi hiyo kushindwa kugawana mali yake. Hali ambayo kumesababisha baadhi ya watu kutafuta njia nyingine za kupata pesa.

Usafishaji haramu wa mafuta unavutia sana katika sehemu za Delta yenye mafuta mengi ya Niger kwasababu inaoonekana kuwa rahisi kuepuka mkono washeria, licha ya juhudi za kukomesha mwenendo huo.

Makumi ya watu wanadhaniwa walikuwa wakifanya kazi katika kiwanda hicho wakati kilipokumbwa na moto

Idadi ya vifo imeongezeka kulingana na wafanyakazi wa kutoa huduma za dharura. Ifeanyi Nnaji wa Shirika la Kitaifa la Usimamizi wa Dharura aliambia BBC Igbo kwamba idadi ya waliouawa sasa imefikia 109.

"Tuligundua miili mingi iko kwenye vichaka na misitu iliyo karibu huku baadhi ya waendeshaji haramu wa kiwanda hicho na wateja wao wakitoroka kutafuta usalama," awali aliliambia shirika la habari la AFP.

Katika taarifa yake Jumapili, Bw Buhari alitoa rambirambi zake kwa familia za waathiriwa na kusema waliohusika na milipuko hiyo lazima wakamatwe na kufikishwa mahakamani.

Mamlaka zimekuwa zikijitahidi kuzuia kuenea kwa mitambo haramu ambapo mafuta machafu yaliyoibwa husafishwa. Rais aliviamuru vikosi vya usalama kuzidisha juhudi za kufunga mitambo hii ya kusafisha mafuta.

Bado haijabainika ni nini kilisababisha mlipuko huo uliotokea usiku wa kuamkia Jumamosi, lakini ajali zimekuwa za kawaida siku zilizopita katika maeneo hatari sawa na hatua za usalama hazijatekelezwa.

Kumekuwa na wasiwasi juu ya ukosefu wa tahadhari katika vituo hivyo na pia juu ya uchafuzi wa mazingira unaosababisha.

Lakini viwanda rasmi vya kusafishia mafuta vya Nigeria havifanyi kazi kwa uwezo wake, na kusababisha uhaba wa mafuta mara kwa mara na kuongezeka kwa bei nchini kote.

Map
1px transparent line