Mauaji ya kimbari Rwanda: Mwanaume afunga ndoa na binti ya aliyemuua baba yake

- Author, Yves Bucyana
- Nafasi, BBC News, Kigali
- Iliyochapishwa
Ili kupata uponyaji wa moyo ni lazima upende - ndivyo anavyoamini mwanamke ambaye sio tu kwamba alimsamehe mtu aliyemuua mumewe miaka 28 iliyopita wakati wa mauaji ya kimbari ya Rwanda, lakini alimruhusu binti yake kuolewa na mwanawe.
Bernadette Mukakabera amekuwa akisimulia hadithi yake kama sehemu ya kuendeleza juhudi za Kanisa Katoliki kuleta upatanisho kwa jamii iliyosambaratika mwaka 1994 wakati takriban watu 800,000 walichinjwa katika siku 100.
''Watoto wetu hawakuwa na uhusiano wowote na kile kilichotokea. Walipendana tu na hakuna kinachofaa kuwazuia watu kupendana,'' Bernadette aliambia BBC.
Yeye na mumewe Kabera Vedaste walitoka katika jamii ya Watutsi, ambao walilengwa baada ya ndege iliyokuwa imembeba rais wa Rwanda wa kabila la Mhutu kutunguliwa tarehe 6 Aprili 1994.
Ndani ya saa chache, maelfu ya Wahutu, wakiwa wamefundishwa na miongo kadhaa ya propaganda za chuki, walianza mauaji yaliyopangwa vyema - kuwageukia majirani zao Watutsi kote nchini humo.
Mmoja wao alikuwa Gratien Nyaminani, ambaye familia yake iliishi karibu na ya Bernadette huko Mushaka magharibi mwa Rwanda.
Wote wawili walikuwa wakulima.
Baada ya mauaji hayo kuisha, huku kundi la waasi la Kitutsi likichukua mamlaka, mamia ya maelfu ya watu wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji hayo walitiwa mbaroni.
Gratien aliwekwa chini ya ulinzi na hatimaye kuhukumiwa na mahakama moja ya jamii, inayojulikana kama gacaca, iliyoundwa kushughulikia washukiwa wa mauaji ya kimbari.
Katika vikao hivi vya kila wiki, jumuiya zilipewa nafasi ya kuwakabili washtakiwa na kusikiliza na kutoa ushahidi kuhusu kile hasa kilifanyika - na jinsi kilivyotokea.

Chanzo cha picha, AFP
Mnamo mwaka 2004, Gratien alimwambia Bernadette jinsi alivyomuua mumewe na kuomba msamaha - na wakati huo huo akachagua kumsamehe.
Hii ilimaanisha kwamba hakulazimika kutumikia kifungo cha miaka 19 jela, lakini kifungo cha miaka miwili katika huduma ya jamii badala yake.
'Nilitaka kusaidia'
Katika muda wa miaka 10 aliyokuwa kizuizini kabla ya kuomba msamaha hadharani, familia yake ilikuwa imejaribu kurekebishana na Bernadette na mwanawe Alfred, ambaye alikuwa na umri wa miaka 14 babake alipouawa.

Chanzo cha picha, BBC
Binti ya Gratien Yankurije Donata, ambaye alikuwa na umri wa miaka tisa hivi wakati wa mauaji ya halaiki, alianza kwenda kwa Bernadette na kusaidia kazi za nyumba hiyo.
''Niliamua kwenda kumsaidia mama Alfred kufanya kazi za nyumbani na hata shambani kwa sababu hakuwa na mtu mwingine wa kumsaidia ikizingatiwa kuwa babangu alihusika na mauaji ya mumewe,'' aliambia BBC.
''Nadhani Alfred alinipenda nilipokuwa nikimsaidia mama yake.''
Bernadette aliguswa moyo na chaguo lake: ''Alinisaidia licha ya kujua vizuri kwamba baba yake alimuua mume wangu, alijua kwamba sikuwa na msaada wowote kwa sababu mwanangu alikuwa katika shule ya bweni.
''Nilipenda moyo wake na tabia zake - hii ndiyo sababu sikumpinga hatua ya yeye kuwa mke wa mwanangu.''
Lakini kwa Gratien haikuwa rahisi sana - mwanzoni alikuwa na shaka alipoambiwa juu ya pendekezo la ndoa.
''Aliendelea kuuliza jinsi na kwa nini familia aliyokosea sana ingetaka chochote kufanya na binti yake,'' Yankurije alisema.

Hatimaye alishawishiwa na kutoa baraka zake kwani Bernadette alisisitiza kwamba hakuwa na nia mbaya juu ya Yankurije.
''Sikuwa na kinyongo chochote kwa binti-mkwe wangu kwa vitendo vya baba yake,'' Bernadette anasema.
''Nilihisi angeweza kuwa binti-mkwe bora kwa sababu alinielewa kuliko mtu mwingine yeyote. Nilimshawishi mwanangu kumuoa.''
Wenzi hao walioana katika Kanisa Katoliki la eneo hilo mwaka wa 2008. Hapa ndipo Gratien aliungama mbele ya kutaniko baada ya kumaliza huduma yake ya kijamii miaka miwili iliyopita - akiomba msamaha.
'Hakuna upatanisho, hakuna ushirika mtakatifu'
Kanisa limekuwa kitovu cha juhudi za kuunganisha jamii katika eneo hilo.
Padre Ngoboka Theogene kutoka Dayosisi ya Cyangugu anasema watu wamepokea mpango wake wa upatanisho.
Madhehebu mengine kadhaa yamewezesha mipango kama hiyo.
Makanisa yanatambua kwamba watu hawana chaguo ila kuishi pamoja, bora zaidi wafanye hivyo kwa amani na uelewano.
"Wale wanaotuhumiwa kwa uhalifu wa mauaji ya kimbari hawaruhusiwi kushiriki sakramenti hadi watakapopatana na familia ya wahasiriwa wao," Padre Ngoboka anaeleza.
Upatanisho wa mwisho hutokea hadharani ambapo mtuhumiwa na mhasiriwa husimama pamoja.
''Mhasiriwa ananyoosha mikono yake kwa mshtakiwa kama ishara ya msamaha,'' anasema.
Watu walihudhuria hafla ya hivi majuzi huko Mushaka kuadhimisha miaka 28 tangu mauaji ya halaiki ili kujifunza njia za kuishi pamoja, muda mfupi baada ya Gratien kufariki.
"Tunapozungumzia mabadiliko sio kubadili rangi ya ngozi bali ni kubadilisha tabia yako mbaya," alisema mwezeshaji wa tukio hilo, Apiane Nangwahabo kutoka parokia ya Mushaka.
''Mabadiliko ya moyo ni muhimu kabla ya kuamua kuishi maisha matakatifu.''
Ilikuwa hapa ambapo Bernadette alizungumza juu ya ndoa ya mwanawe na binti wa muuaji wa mumewe.
''Nampenda sana binti-mkwe wangu na sijui ningeishi vipi ikiwa hangekuwa hapa kunisaidia baada ya mume wangu kufariki dunia.''
Anasema ametiwa moyo kuona kwamba simulizi ya mapenzi ya Alfred na Yankurije imehamasisha wengine wengi kutafuta na kutoa msamaha.














