Mauaji ya kimbari Rwanda:Jinsi picha iliyomuita ‘muuaji’ ilivyoharibu maisha yake na familia yake

Mauaji ya kimbari Rwanda:Jinsi picha iliyomuita 'muuaji' ilivyoharibu maisha yake na familia yake

Chanzo cha picha, BBC & AFP

Iliyochapishwa

Mzee Apollinaire Hitimana, na familia yake wanalalamika kwamba maisha yao yaliharibika kwa karibu miaka 20 kwa sababu ya picha ambayo ilisambaa duniani kote ikimuonyesha kama mhusika wa mauaji ya kimbari ya 1994.

Ni picha ambayo imekuwa ikitumika katika magazeti nchini Rwanda na nje ya nchi, na pia kwenye nyumba za kumbukumbu ya mauaji ya kimbari nchini Rwanda.

Yeye anakana kuhusika katika mauaji ya kimbari na anataka ahakikishiwe kuondolewa picha hiyo sehemu zote iliko. Wizara ya sheria inasema imeanza kushughulikia suala hilo.

Picha yake ilitumiwa katika filamu na vyombo mbalimbali vya habari vya Rwanda na vya kimataifa na imewekwa katika majumba yote ya kumbukumbu ya mauaji ya kimbari kote nchini Rwanda.

Maeneo mengi ilipowekwa picha ya Hitimana imeandikwa chini kwamba alikua miongoni mwa wajumbe wa kikundi kilichoendesha mauaji na ukatili wakati wa mauaji hayo kilichojulikana kama Interahamwe , lakini majina yake hayajaandikwa kwenye picha yake.

Baada ya miaka mingi ni hivi karibuni tu Bw Hitimana aliondokewa na hofu na kujitokeza kuzungumza kuhusu picha yake iliyosambaa.

Hitimana aliiambia BBC kwamba ni kweli mtu anayeonekana katika picha hiyo ni yeye, lakini hakupigwa picha akifanya mauaji na hakuhusika kwa namna yoyote ile na mauaji ya kimbari yaliyotokea Rwanda.

Anasema ombi lake ni kwamba angependa picha yake iondolewe kote iliko.

Aliyepiga picha hiyo aliiambia BBC kuwa kweli hakumpiga picha hiyo akifanya mauaji, ingawa anasema kuwa hakumbuki matukio yote ya wakati huo alipopiga picha ya Hitimana kwani tangu alipoipijga imepita miaka 26 sasa.

Maafisa nchini Rwanda wanasema hilo ni suala linalowahusu Hitimana na na mpiga picha.

Picha ilipigwa vipi? Na wapi?

Bwana Hitimana anaishi katika wilaya ya Muhanga katika mkoa wa Kusini, ambako alizaliwa .

Anasema picha hiyo ilipigwa mwaka 1994 alipokuwa ametoka katika kambi ya wakimbizi alikokuwa amekimbilia alipokuwa amerudi nyumbani kiwake kutafutia familia yake chakula.

Mahala pengi ilipo picha hii inaonesha kuwa mwenye picha hii kulia ni mmoja wa wajumbe wa kikundi cha Iterahamwe kilichowachinja watu.

Chanzo cha picha, AFP

"Nilipofika pale katika eneo la Cyakabiri, kilomita chache nikamuona mwanajeshi aliyekuwa na bunduki akaniambia hivi 'unatoka wapi na unaelekea wapi?'

Nikasema 'nimetoka kambini hapa chini narudi nyumbani kidogo kutafuta kitu cha kula kwa ajili ya familia yangu ", anasema Hitimana.

Anasema kuwa aliambiwa afungue mkoba aliokuwa nao wakaona mpanga ndani yake kisaha wanajeshi wakamlazimisha kuushikilia vizuri na anasema kuwa alimuona mtu akimpiga picha lakini anasema:"Sikujua kuwa nilipigwa picha ".

Alexander Joe aliyepiga picha hii kwa ajili ya Shirika la habari AFPmwezi Juni 1994, ,anasema kuwa walikuwa ndani ya gari na walipofika katika kundi la watu wengi akawaomba askari kupiga picha.

"Picha hii niliipiga katika eneo ambalo ungedhania ni baa au duka, niliwaomba wanajeshi waliokuwepo kama ninaweza kupiga picha kwasababu usingeweza kupiga picha mahala penye watu wenye silaha bila kuomba ruhusa.

"Siwezi kujua kama mwanaume huyo alilazimishwa na wanajeshi kupiga picha na upanga, siwezi kuthibitisha hilo au kulikana, siwezi kukumbuka kwani ni matukio yaliyotokea miaka 26 iliyopita ."

Bwana Hitimana alichaguliwa miongoni mwa wazee wenye busara ambao walikuwa na jukumu la kuendesha kesi hizo.

Chanzo cha picha, BBC GAHUZA

Alitengwa na wazee

Mwaka 2001 wakati mahakama za kijadi zilipoanza kwa ajili ya kushughulikia kesi za mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 Bwana Hitimana alichaguliwa miongoni mwa wazee wenye busara ambao walikuwa na jukumu la kuendesha kesi hizo.

Hatahivyo anasema: "Alikuja mtu mmoja akasema 'mimi nilimuona huyu mwanaume katika jumba la kumbukumbu ya mauaji ya kimbari la Kigali akiwa ameshikilia mpanga ', mwingine akasema 'hata mimi nilikua sitaki kusema tu, lakini pia nilimuona '.

"Wakaniuliza unasema nini juu ya hayo yanayozungumzwa juu yako?' Hapo ndipo nilipokumbuka jinsi nilivyoshurutishwa, nikasema 'ndugu zangu hiyo picha lazima ni yangu, nikasema 'sikilizeni niwaambie ilivyopigwa na mahala waliponipigia ".

Bwana Hitimana anasema kuwa hakuwahi kuhusika wala kushitakiwa kwa kuhusika katika mauaji ya kimbari ya Rwanda. Lakini picha hiyo ilinifanya niondoshwe miongoni mwa wazee wa mahakama za Gacaca.

"Baadaye tulivyorudi kwenye mikutano kuzungumzia suala la picha yangu, afisa liyekuja kusuluhisha aliniuliza kuhusu picha yangu nikajieleza tena babisubiramo,

"Katika uamuzi walisema 'wewe hautaketi tena kwenye baraza la wazee wa mahakama '.

"Hapo hakuna maelezo mengine yaliyotolewa licha ya kusema kuwa eti mtu akiniona, akapata mtu ambaye picha yake iko kwenye kumbukumbu za mauaji ya kimbari si anaweza kusema baraza ni la Interahamwe ?...Ndio maelezo waliyonipa ."

Mke wake Mukamana anasema kuwa picha hii imewaachia kidonda

Chanzo cha picha, BBC GAHUZA

"Ninachoweza kusema ni kwamba hakuna nilichoandika kwenye picha kinachoonesha jinsi alivyooneshwa mwanaume huyo, sikupiga picha watu wakiuliwa, kama ningepiga picha za mauaji ningeelezea kwenye maenelo ya picha ."

'Tumeachwa na kidonda' -

Mke wake Hitimana- Annnonciata Mukamana anasema kuwa hata watoto wao shuleni walikabiliwa na kipindi kigumu ambapo walikuwa wakiambiwa na wenzao kuwa walimuona baba yao kwenye televisheni akioneshwa kama Interahamwe.

Hitimana anasema kuwa amekuwa akiepuka kwenda mahala walipo watu , na aliamua kuacha baadhi ya shughuli kwasababu ya kuitwa Interahamwe kila anakoenda, kwasababu ya picha yake iliyosambaa hadi mbali.

Mke wake Bi Mukamana anasema: "Tunafikiria Rais wa Jamuhuri ndiye anayeweza kutuondolea aibu hii kwani tumesikitika, tuna jeraha la rohoni".

Bwana Hitimana anasema: "Napendekeza picha hii ishushwe, nioneshwe dhihirisho kuwa picha hii imeshushwa kutoka kila mahali ilipowekwa ."

Faustin Nteziryayo, rais wa mahakama ya juu zaidi nchini Rwanda, hivi karibuni aliwaambia waandishi wa habari kuwa watachunguza ukweli kuhusu madai ya Hirikmana .

Alisema: "…Suala hili nitalizungumza na waziri wa sheria tujue ukweli juu yake halafu ngazi husika zitachukua hatua ."

Hitimana na mkewe wakiwa nyumbani kwao katika kata Shyogwe

Chanzo cha picha, BBC GAHUZA