Kiwanda cha vyuma Mariupol : Tuna waliojeruhiwa na waliokufa ndani ya mahandaki'

Iliyochapishwa

Moja ya wanajeshi wanaotetea mji wa Mariupol ameambia BBC kwamba eneo la juu la kiwanda cha vyuma kilichozungukwa limeharibiwa huku raia wengi wakiwa wamekwama chini ya vifusi ya nyumba zilizoshambuliwa .

Akizungumza kutoka kwa kiwanda cha Azovstal - eneo la mwisho la Mariupol ambalo bado halijadhibitiwa na Urusi - Svyatoslav Palamar kutoka kwa wapiganaji wa kitengo cha jeshi cha Azov alisema kwamba wanajeshi wa Ukraine wameweza kukabili mashambulizi ya Urusi.

''Kila mara mimi husema kwamba iwapo tutasalia kuwa hapa , Mariupol itasalia katika udhibiti wa Ukraine'', alisema.

Mapema rais wa Urusi Vladmir Putin alifutilia mbali mpango wa wanajeshi wa Urusi kushambulia kiwanda hicho na badala yake akawataka wanajeshi wake kukizingira ili hata nzi wasitoroke.

"Kizibeni kiwanda hicho ili hata 'nzi asitoroke''', alisema.

Eneo kubwa la Mariupol limeharibiwa katika wiki ya mashambulizi makali kutoka kwa Urusi na mapigano ya barabarani.

Utekaji wa mji huo ulio na bandari ni muhimu na Urusi itapeleka wanajeshi zaidi kujiunga na wenzao katika eneo la mashariki la Donbas.

Kapteni Palamar alisema kwamba Urusi imeshambulia kiwanda hicho kutoka kwa meli na kukiangushia mabomu ya kuvunja mahandaki.

BBC haijaweza kuthibitisha madai hayo. Lakini yanaongeza Ushahidi mapema wiki hii kutoka kwa kamnada wa jeshi la wanamaji wa Ukraine aliyepo katika kiwanda hicho , aliyesema kwamba wanajeshi wa Ukraine wamezidiwa nguvu na kwamba chakula na silaha walizonazo kimepungua.

"Majumba yote katika eneo la Azovstal yameharibiwa. Waliangusha mabomu makubwa, mabomu ya kuvunja mahandaki ambayo yamefanya uharibifu mkubwa.

Tuna watu waliofariki na wengine kujeruhiwa ndani ya mahandaki. Raia wengi wanasalia kukawama chini ya vifusi vya majumba hayo,'' alisema kapteni Palamar.

Kitengo cha Azov kilikuwa kundi la wanazi wa mrengo wa kulia ambao baadaye walishirikishwa katika jeshi la kitaifa la Ukraine. Wapiganaji wake ambao ni pamoja na wanamaji , walinzi wa mpakani na maafisa wa polisi ndio maafisa wa mwisho wanaoutetea mji huo.

Alipoulizwa ni wanajeshi wangapi wa Ukraine waliopo katika mji wa Mariupol , kapteni Palamar alisema wanatosha kukabiliana na mashambulizi.

Alisema kwamba raia walikuwa mbali na wapiganaji hao . Walikuwa katika mahandaki yalio na watu kati ya 80-100 lakini haijulikani kulikuwa na raia wangapi kwasababu majumba yalikuwa yameharibiwa na wapiganaji hawawezi kuwafikia kutokana na mashambulizi.

Maeno ya kuingia katika mahandaki hayo yalikuwa yamezibwa na vifuniko vizito ambavyo ni mashine kubwa tu ambazo zinaweza kuondoa, alisema.

Unaweza pia kusoma