Uchaguzia Kenya 2022:Shauku ya wapiga kura,nia ya kufungua ukurasa mpya na ushawishi kwa majirani

    • Author, Mohammed Abdulrahman
    • Nafasi, Mchambuzi
  • Iliyochapishwa

Kenya itakuwa na uchaguzi wake mkuu Agosti 9 mwaka huu, uchaguzi ambao unafuatiliwa kwa karibu na majirani zake.

Uchaguzi huu utakuwa wa aina yake kwa sababu moja kubwa. Kwa mtazamo wa misukosuko ya ilionza miaka 3 baada ya uhuru na kuendelea takriban miongo minne chini ya utawala wa chama cha Kenya African National Union (KANU ) uchaguzi wa Agosti utakuwa kipimo cha kukomaa kwa demokrasia, kujaribu kuondokana na siasa za ukabila na hivyo kufungua ukurasa mpya.

Vuguvugu la kudai demokrasia lilivyoanza

Hatua ya kwanza ya mabadiliko ilikuwa ni ile ya 1991, wakati vuguvugu la kudai kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi lililoongozwa na wanasiasa kadhaa maarufu lilipoilazimisha serikali ya Rais Daniel Arap Moi kubadili kifungu cha katiba na kuachana na mfumo wa utawala wa chama kimoja cha KANU.

Miongoni mwa walioongoza vuguvugu hilo ni pamoja na wale waliopigania uhuru Jaramogi Oginga Odinga na Martin Shikuku ( kwa kuwataja wachache ). Moi ndiye aliyemridhi Rais wa kwanza Mzee Jomo Kenyatta aliyefariki dunia 1978.

Uchaguzi wa kwanza 1992 ulioitishwa na Moi baada ya kutumia mbinu kulivunja bunge ulimpa ushindi. Sababu ilikuwa ni uchanga wa upinzani. Moi akashinda tena 1997 kutokana na kugawika kwa wapinzani.

Rais huyo wa pili wa Jamhuri ya Kenya alipoamua kustaafu 2002 ikiwa hatua ya pili ya ukurasa wa mabadiliko pale wapinzani walipoweza kuungana na kuwa na mgombea mmoja wa kiti cha Urais.

Walimteuwa Mwai Kibaki wa chama cha Democratic (DP) baada ya mvutano baina yao hatimaye kuzimwa kwa ushawishi wa Raila Odinga kwa usemi wake maarufu "Kibaki Rosha."

Kibaki akamshinda aliyekuwa mgombea wa KANU Uhuru Kenyatta aliyesimamishwa kwa ushawishi wa Moi mwenyewe .

Moja ya mafanikio yaliofuata ni kupatikana kwa katiba mpya 2004.

Mabadiliko yaliporudi nyuma

Hata hivyo Gurudumu la mabadiliko lilirudi nyuma ulipofanyika uchaguzi mkuu 2007.

Kiu cha madaraka na tafauti za kimkoa na kikabila kikasababisha machafuko na mapigano ambapo karibu watu 1.100 waliuwawa.

Matumaini ya Wakenya ya kuwa na siasa mpya yakatoweka. Jumuiya ya Kimataifa ililazimika kati kuleta suluhu, iliopatikana kwa kuundwa serikali ya Umoja wa Kitaifa huku Kibaki akibakia kuwa Rais.

Juhudi hizo ziliongozwa na aliyekuwa Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Kofi Anna.

Vurumai nyengine ilizuka 2013, mzizi wa fitna ukiwa Tume Huru ya Uchaguzi iliodaiwa kushindwa kuwajibika.

Ushindi wa kumpa muhula wa pili Uhuru Kenyatta ukacheleweshwa kutokana na uamuzi wa mahakama kwamba uchaguzi ulikuwa na dosari. Uhuru uchaguzi wa marudio uliosusiwa na upinzani na sasa anamaliza muhula wa pili na wa mwisho.

Uhuru ameigeuza karata katika uchaguzi huu.

Chama chake cha Jubilee kimempitisha kiongozi wa ODM Raila Odinga kuwa mgombea wake chini ya jukwaa la Azimio la Umoja.

Wanasiasa hao waliamua kuondoa tafauti zao kwa kile walichosema ni kwa maslahi ya taifa ili kuleta Umoja.

Uchaguzi Kenya 2022:Unaweza pia kusoma

Vigogo kutoka vyama wameungana na ushirika huo unaoitwa Azimio la Umoja na kumuidhinisha Odinga aliyevishwa lakabu ya '"BaBa", nao sasa wakija na kauli mbiu ya Baba Tosha.

Hali hii inafuatia kuhasimiana kwa Uhuru na naibu wake wa Urais William Ruto.

Ruto amekuwa akilalamika kwamba mwenzake amekiuka mapatano yao kwamba atakapomaliza muhula wake wa pili amuunge mkono Ruto kuwa mrithi wake.

Kutokana na uhasama huu Ruto ,wanasiasa na wakenya wamegawika.

Ruto naye anaongoza muungano na wanasiasa wengine wakiwemo Musalia Mudavadi na Moses Watangula unaojulikana kama Kenya Kwanza, uliomtea awe mgombea wao wa kiti cha Urais.

Dalili za kuhitilafiana marafiki hao wawili, zilianza wakati Uhuru na Raila walipokutana chini ya mpango waliouita Building Bridges Initiative-BBI (Hatua ya kujenga daraja la kuleta maelewano ).

Lengo lao wanasema ni kuondoa tafauti za kikabila zilizoikumba Kenya tokea uhuru wake kutoka kwa Uingereza.

Pia kuondoa utamaduni uliojengeka wa kwamba nchi hiyo itawaliwe na watu wa makabila mawili tu Kikuyu na Kalenjin.Uhuru ni mkikuyu kabila la Mzee Kenyatta na Kibaki Rais watatu, Ruto ni Mkalenjin sawa na Moi aliyemrithi Mzee Kenyatta .

Azimio la Umoja, muungano ulioundwa na Uhuru na Raila ambaye ni kutoka kabila la Luo limeungwa mkono na vigogo wengine wakiwemo Makamu wa zamani wa rais Kalonzo Musyoka na Martha Karua.

Kampeni za uchaguzi zimepamba moto.

Lakin bado kuna umuhimu wa kuchukuliwa hatua za tahadhari kutokana na lugha inayotumiwa na wanasiasa. Kauli za Chuki zilichangia vurugu za 2007/2008. Safari ni kauli za mashambulizi ya binafsi na hata matusi.

Ushawishi wa siasa za Kenya kwa majirani

Kwa upande mwengine, kinachofurahisha na kuelekea kuwasisimua walioko nchi za jirani na hasa Tanzania , ni kiwango cha uhuru wa vyombo vya habari na kutoa maoni, ambapo hali katika mataifa hayo mawili imeendelea kuwa isiyofurahisha kwasababu ya vikwazo mbali mbali vya dola.

Pia katika jicho la demokrasia, Kenya inaangaliwa iliopiga hatua fulani panapohusika naUhuru wa mahakama na pia kuheshimiwa kwa Katiba, sababu ikiwa ni mahakama kutoingiliwa na mkono wa dola.

Kilio kikubwa hivi sasa nchini Tanzania ni Katiba mpya na Tume huru, licha ya kwamba vyama vya upinzani vinatafautiana kipi ni muhimu kwanza.

Wakati chama kikuu cha upinzani Chadema kinasema Katiba mpya ndiyo itakayozaa Tume huru ya uchaguzi, ACT-Wazalendo kinataka Tume huru kabla ya uchaguzi ujao 2005, Chama tawala cha mapinduzi CCM kinaendelea kulipiga chenga suala la katiba mpya na Tume huru ya uchaguzi.

Wao wanasema kwanza ni ujenzi wa taifa kwa maana ya maendeleo. Bila shaka kwa wapinzani Tanzania Kenya inaweza kuwa chachu ya mabadiliko ya kisiasa nchini Tanzania.

Nchini Uganda bado Rais Yoweri Museveni anashikilia madaraka kwa staili ya kuvikandamiza vyama vya upinzani .

Akiwa anatawala kwa miaka 36 sasa ,kuna hata tetesi kuwa anamuandaa mwanawe Luteni Jenerali Muhoozi Kainerugaba mwenye umri wa miaka 47, kuwa mrithi wake.

Itakumbukwa alipochukuwa madaraka 1986, Museveni alisema kinyume na viongozi waliotangulia, wao hawakuingia madarakani kubakia na wangeondoka mara tu baada ya kuyaweka mambo sawa.

Jitihada ya kufunika maovu yaliopita

Kukisalia miezi minne kabla ya Uchaguzi mkuu Wakenya watakuwa wanausubiri matokeo ya Agosti 9 wakitumai zoezi hilo litakuwa la amani na kufunika historia mbaya ya kisiasa katika taifa hilo.

Utawala wa Mzee Kenyatta ulikuwa wa mkono wa chuma na hakuvumilia upinzani, Katika kadhia ambazo hadi leo hazijapata jibu na sababu gani yakatokea,ni kupotea kwa wanasiasa kadhaa walioonekana kitisho kwa Mzee Kenyatta, utawala wake au hata kwa wanasiasa na wapambe waliomzunguka Kenyatta.

Mwanasiasa wa kwanza kuuwawa alikuwa mweyne asili ya Kigoa Pio Gama Pinto 1965, miaka miwili tu baada ya uhuru.

Kadhia za mauaji zikaendekea dhidi ya wanasiasa wengine maarufu . aliyekuwa Waziri wa mipango wa uchumi na maendeleo Tom Joseph Mboya (Mluo), Josiah Mwangi Kariuki (Mkikuyu) na aliyekuwa waziri wa mambo ya nchi za nje Robert Ouko (Mluo) aliyeuwawa wakati wa utawala wa Moi.

Vifo vyao hadi leo vimefunikwa. Kenya sasa inahitaji amani , umoja na kusonga mbele na kuufungua ukurasa huo wa yote yaliopita, ambayo msingi wake ni kuwania madaraka na ukabila.