Uchaguzi Kenya 2022: Je gharama kubwa ya kuendesha uchaguzi Kenya ni ya haki?.....

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, Joseph Kioko
- Nafasi, Mchambuzi wa Siasa
- Iliyochapishwa
Mazingira ya uchaguzi nchini Kenya yamebadilika sana kutoka kwa njia ya upigaji kura ya foleni ambayo ilipitishwa katika uchaguzi mkuu wa 1988 hadi hali ya sasa ambapo kituo cha kupigia kura ndicho kitovu cha uchaguzi.
Katika chaguzi zilizopita (1992/1997/2002/2007) kituo kikuu cha kupigia ndicho ambacho masanduku yote ya majimbo yangesafirishwa, kuhesabiwa na kutangazwa kwa matokeo.
Mchakato huu ulikumbwa na matukio mengi ya udanganyifu, kwa mfano kujazwa kwa masanduku ya kupigia kura, kutoweka kwa kura hali imayofanya matokeo ya uchaguzi kukosa uaminifu.
Kwa upande wa urais, baada ya kura kuhesabiwa katika kituo kikuu cha kijimbo, matokeo yangesafirishwa hadi kwenye kituo cha kitaifa cha kuhesabia kura, ambapo Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ingetangaza matokeo. Utaratibu huu ulikuwa mrefu na usio wazi na kukabiliwa na udanganyifu.
Uchaguzi Kenya 2022:Unaweza pia kusoma
UNAYOFAA KUJUA:Uchaguzi Kenya 2022: Je Naibu wa rais wa Kenya William Ruto anakabiliwa na changamoto gani katika kumteua naibu wake wa rais?
1.Je Katiba ya kenya inasemaje kuhusu uchaguzi?
Kupatikana kwa Katiba Mpya, kulifungua njia ya kupitishwa kwa mageuzi ya kimaendeleo ya uchaguzi, ambayo yalihusu uhuru wa raia kutumia haki zao za kisiasa bila woga wala vitisho, usawa wa kura, uchaguzi huru na wa haki, ambao unafanywa kwa kura ya siri katika njia ya uwazi, isiyopendelea upande wowote, yenye ufanisi, sahihi na ya uwajibikaji.
Katiba inasema kwamba uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge wa Bunge la Kitaifa na lile la Seneti, Mwanachama wa Bunge la Kaunti, Gavana na mwakilishi wa wanawake wa Kaunti utafanywa siku moja ambayo ni Jumanne ya pili ya mwezi Agosti katika kila mwaka wa tano.
Ingawa rais anachaguliwa moja kwa moja na wapiga kura wote waliosajiliwa nchini, gavana wa kaunti, Seneta na mwakilishi wa wanawake wa Kaunti watachaguliwa na wapiga kura waliosajiliwa katika kaunti mahususi.

Chanzo cha picha, AFP
Kwa hivyo nafasi sita zinazogombaniwa wakati wa Uchaguzi Mkuu ni ile ya Urais (1), Gavana (47), Seneta (47), Mjumbe wa Bunge la Kitaifa (290), mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti (47), na Mjumbe wa Bunge la kaunti ( 1450).
Kwa hivyo katika kila uchaguzi, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ina jukumu la kuhakikisha kuwa njia yoyote ya upigaji kura inayotumiwa, ni rahisi, sahihi, inayoweza kuthibitishwa, salama, ilio na uwajibikaji na wazi.
Kura zilizopigwa uhesabiwa, kuorodheshwa na matokeo kutangazwa mara moja na msimamizi katika kila kituo cha kupigia kura; matokeo kutoka kwa vituo vya kupigia kura yanakusanywa kwa uwazi na kwa usahihi na kutangazwa mara moja na msimamizi wa uchaguzi; na miundo na mifumo ifaayo ya kuondoa dosari katika uchaguzi imewekwa, ikijumuisha uhifadhi salama wa nyenzo za uchaguzi.
2.Gharama ya uchaguzi Kenya
Katika maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2022, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati alisema kwamba watahitaji Sh40.329 bilioni ili kuendesha Uchaguzi Mkuu wa 2022 ipasavyo pamoja na Sh588 milioni za ziada ili kupata vifaa muhimu za kukabiliana na maradhi ya Covid-19. Vifaa hivi ni pamoja na bunduki za kupima joto, sanitizer, sabuni na sehemu za kunawia.

Chanzo cha picha, AFP
Hii inafanya jumla ya mahitaji ya Uchaguzi Mkuu kufikia bilioni 40.917. Gharama kwa kila mpiga kura katika uchaguzi ujao kutokana na bajeti iliyopendekezwa na wapiga kura waliojiandikisha inafikia dola 17 za Marekani , ikiwa ni gharama kubwa sana.
Kazi muhimu ya IEBC ni pamoja na kuajiri wafanyikazi, kununua vifaa vya uchaguzi, kuendesha elimu ya wapigakura na mazoezi ya usajili, kando na kukusanya na kuwasilisha matokeo.
Ili uchaguzi uwe huru, wa haki, uliothibitishwa na wa uwazi inavyotakiwa kisheria, IEBC inabidi iwe na wafanyikazi waliofunzwa vilivyo kutoka kaunti 47 na maeneo bunge 290 ambao watakuwa waratibu wa uchaguzi na hatimaye maafisa wasimamizi wakati wa uchaguzi.
Mchakato na gharama ya kuajiri, mafunzo na kujenga uwezo wa maafisa hawa ni kitu muhimu lakini chenye gharama kubwa . Hii ni mojawapo ya sababu nyingi zinazoweza kuelezea gharama ya juu ya kuendesha uchaguzi nchini Kenya.
Matumizi ya teknolojia katika mchakato mzima wa uchaguzi kutoka usajili wa wapigakura, upigaji kura kwa kutumia bayometriki, utumiaji wa kielektroniki wa kujumlisha matokeo ni kipengele kingine kikuu cha matumizi ya juu.
3. Gharama ya uchaguzi wa Kenya ikilinganishwa na mataifa mengine ya Afrika
Kihistoria, chaguzi za Kenya mara zote zimekuwa zikigharimu walipa kodi pesa nyingi ikilinganishwa na nchi zingine za Kiafrika.
Wakati wa uchaguzi mkuu wa Kenya wa 2017 ambapo kulikuwa na wapiga kura milioni 19.6 waliojiandikisha kuliigharimu serikali $25.40 kwa kila mpiga kura, huku, Rwanda yenye wapiga kura milioni 6.8 waliojiandikisha ikitumia dola milioni 6.5 (chini ya dola moja kwa kila mpiga kura) kufanya uchaguzi wake wa tatu wa vyama vingi.
Uchaguzi wa 2016 nchini Ghana, ambapo watu milioni 15.7 walisajiliwa, uligharimu serikali dola 12 kwa kila mpiga kura, huku Tanzania, nchi yenye watu wengi na wapiga kura wengi kuliko Kenya, ilitumia dola milioni 300 chini ya Kenya katika uchaguzi wake wa 2015.
Kama eneo lenye nguvu kubwa ya kiuchumi na demokrasia iliyo wazi kiasi, uchaguzi wa Kenya unavutia umakini nje ya mipaka yake.
Mwaka huu uchaguzi wa urais unaonekana kuwa mchuano wa Muungano wa farasi wawili kati ya Kenya Kwanza wa Naibu Rais William Ruto na Muungano wa Azimio wa Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga.
Hata hivyo licha ya kupitishwa katiba endelevu na kupiga hatua katika demokrasia, gharama ya kuendesha uchaguzi mkuu imesalia juu sana nchini Kenya ikilinganishwa na mataifa mengine ndani ya eneo hilo.















