Mahakama ya Haki Afrika Mashariki yaitaka serikali ya Tanzania kurekebisha sheria ya vyama vya siasa

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 2

Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) imeiamuru serikali ya Tanzania kurekebisha Sheria ya vyama vya siasa, ili iondoe vifungu vinavyokiuka makataba ulioianzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), hukumu iliyotolewa kuhusu kesi iliyofunguliwa na wanasiasa wapinzani.

Hukumu ya EACJ ilisema kuwa sheria hiyo inakiuka vifungu vya mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Vyama vinne vya upinzani nchini Tanzania viliishtaki serikali katika mahakama ya Afrika mashariki kuhusu haki EACJ.

Sheria hiyo ambayo ilitiwa saini na aliyekuwa rais wa taifa hilo , John Pombe Magufuli mwezi Februari mwaka 2019 na kuchapishwa katika gazeti la serikali siku 10 baadaye ilizua mjadala mkubwa nchini humo.

Malengo ya kesi hiyo

Lengo la kesi hiyo kulingana na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Freeman Mbowe ni kwamba sheria hiyo mpya iliwekwa kupitia kubadili na kuongeza baadhi ya vifungu ambavyo vinakiuka lengo la kuanzisha ushirikiano wa jumuiya ya Afrika mashariki.

Malalamishi ya vyama vya kisiasa

Sheria mpya ya Vyama vya kisiasa ilikumbana na upinzani mkali toka muswada wake ulipowasilishwa kwa mara ya kwanza Bungeni.

Vyama vya upinzani na asasi za kiraia vimekuwa vikilalamikia sheria hiyo wakidai inafanya shughuli za siasa kuwa kosa la jinai.

Bunge lilipitisha muswada huo mwezi Januari mwaka 2019 na hatimaye kusainiwa kuwa sheria na rais Magufuli.

Wakati wa kupitishwa kwake wakati huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama alilieleza Bunge kuwa muswada huo ni kiboko.

"Lengo ni kuhakikisha chama cha siasa kinakuwa na sifa za usajili muda wote wa uhai wake na kueleza bayana mamlaka ya msajili wa vyama vya siasa kuhakiki muda wowote utekelezaji wa sheria ya vyama vya siasa ili kuhakikisha chama cha siasa kinazingatia na kutekeleza masharti ya usajili," amenukuliwa na Mwananchi akisema.

Baadhi ya yale yanayolalamikiwa kwenye sheria hiyo ni pamoja na msajili wa vyama vya siasa kupewa mamlaka ya kuingilia mfumo wa uchaguzi ndani ya vyama.

Malalamiko mengine ya 'uonevu' kwa mujibu wa upinzani ni masharti ya namna ya utoaji wa elimu ya uraia kwa kuzuia vyama rafiki kutoka nje kushiriki.

Moja ya kifungu kilichopingwa ni cha Kifungu cha 19 ambacho kinasema msajili anaweza kukisimamisha usajili wa chama kwa sababu atakazozitaja na kwa muda atakaouweka mpaka ili chama hicho kiweze kujirekebisha.

Chama ambacho kimesimamishiwa usajili hakitaweza kufanya shughuli zote za kisiasa.

Na iwapo msajili ataona chama hicho hakijajirekebisha anaweza kukifutia usajili.

Kifungu hiki, wapinzani walidai kinaweza kutumika kuzuia vyama kushiriki uchaguzi kwa kusimamishiwa usajili kabla ya uchaguzi na kurudishiwa usajili baada ya uchaguzi kupita.

Uamuzi wa Mahakama umepokelewa vipi?

Miongoni mwa waliopokea kwa mikono miwili ni chama cha ACT-Wazalendo wakisema kuwa ''Msimamo wa ACT-Wazalendo siku zote ni kuwa marekebisho ya Sheria ya vyama vya siasa yaliyofanyika mwaka 2019 hayakubaliki kwenye jamii ya misingi ya Kidemokrasia kwa sababu yanajinaisha siasa na kuipa madaraka makubwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa. Ilisema sehemu ya taarifa yake.

Chama hicho kimetoa wito wa sheria kuandikwa upya ili kuhakikisha Siasa nchini humo zinaendeshwa kwa misingi ya haki na usawa.

Hukumu hii imetolewa jana kwenye kesi iliyofunguliwa mwaka 2019 na aliyekuwa Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad, Kiongozi wa chama hicho Zitto Kabwe, Mwenyekiti wa chama cha CHADEMA, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa chama cha CHAUMMA, Hashim Rungwe na Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Salum Mwalim kwa niaba ya vyama 10 vya upinzani.