Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Uchaguzi wa Kenya 2022: Nyuso zilizotawala siasa za Kenya tangu ipate uhuru
Kenya inajitayarisha kwa uchaguzi wake mkuu wa Agosi tarehe 9 mwaka huu na jambo moja kubwa ambalo limejitokeza wazi na ambalo linazidi kuzungumziwa ni kujipata kwa familia tatu kubwa za kisiasa katika mrengo mmoja kwenye uchaguzi huo.Familia hizo zimekuwa nyuso zinazotambulika katika siasa za Kenya tangu ijinyakulie uhuru na yamkini vizazi vya wanasiasa hao watangulizi bado vipo kati kati ya uchaguzi wa mwaka huu .
Siasa za Kenya kwa miaka mingi tangu nchi hiyo ipate uhuru wake mwaka wa 1963 zimeegemea familia za Mzee Jomo Kenyatta na Jaramogi Oginga Odinga, mashujaa wawili wa vita vya ukombozi, ambao miaka miwili baada ya uhuru walitofautiana na kuwa mahasimu wakuu wa kisiasa.
Ijapokuwa Daniel arap Moi, alikuwa rais wa pili wa Kenya aliyekaa mamlakani kwa muda mrefu zaidi - miaka 24, na rais wa tatu, Mwai Kibaki ambaye alikuwa madarakani kati ya 2002-2013, unapofuatilia hisia na siasa za Kenya, taswira inayotawala ni kati ya familia mbili- ya Kenyatta na ile ya Odinga.Maajuzi mtoto wa rais wa pili Daniel Moi ,Gideon Moi naye amejipata katika muungano wa Azimio la Umoja ambao unamuunga mkono Raila Odinga kumrithi rais Uhuru Kenyatta.
Mzee Jomo Kenyatta na Jaramogi Oginga Odinga
Mzee Jomo Kenyatta na Jaramogi Oginga Odinga walianza kutawala siasa za Kenya hata kabla ya nchi ya Kenya kupata uhuru.Taifa lilipopata uhuru ,Oginga ndiye aliyekuwa makamu wa rais wa kwanza wa nchi huku Mzee Kenyatta akichukua hatamu kama rais wa kwanza .
Kulingana na historia tofauti kati ya viongozi hao wawili ilikuwa chanzo cha uhasama wa kikabila ambao ulipelekea jamii mbili nchini, Wakikuyu na Wajaluo kutokurubiana kisiasa.
Kutokana na uhasama huo wa jadi makabila mengine yaliunga mkono moja kati ya jamii hizo, jambo ambalo limekuwa likigawanya nchi ya Kenya katika mirengo miwili mikubwa ya kisiasa.Lakini hilo sasa litakuwa katika kipimo katika uchaguzi wa mwaka huu baada ya Rais Kenyatta kuamua kumuunga mkono Odinga katika kinachoonekana na wadadisi kama hatua ya kujaribu kupunguza joto kali la uhusiano wa kisiasa kati ya jamii zao .
Uhasama huo ulijitokeza bayana mwaka 2013 wakati mtoto wa Bw Oginga, Raila Odinga na mwenzake wa Mzee Kenyatta, Uhuru Kenyatta walipokabiliana kwenye uchaguzi mkuu wa 2017 na Rais Uhuru Kenyatta kuibuka mshinda.
Matokeo ya uchaguzi huo yalipingwa mahakamani na Bw. Odinga na hatimaye kubatilishwa kutokana na dosari na kufanya uchaguzi wa urais kurudiwa. Hali ilichukua mkondo hatari wakati Bw Odinga na wafuasi wake walipokataa matokeo ya ushindi wa Rais Kenyatta na hata kujiapisha kama ''rais wa watu''.
Ili kutatua mzozo huo viongozi hao wawili waliammua kuchukua hatua ambayo haikutarajiwa na wengi na kuamua kufanya kazi pamoja kuunganisha nchi maarufu ''Hand shake''.
Wazazi wa viongozi hao wawili walikutana mapema miaka ya hamsini, wakati huo, Bw Oginga akiwa mfanyabiashara mashuhuri kutoka eneo la Nyanza na ni Mzee Kenyatta aliyemshawishi kujiunga na siasa.
Baadaye Bw. Oginga alimsaidia Kenyatta kuwa waziri mkuu wa kwanza wa Kenya na kisha Rais kwenye uchaguzi mkuu wa 1963. Hata hivyo, tofauti zao zilianza Bw Oginga alipoanza kukumbatia usosholisti, jambo ambalo halikumfurahisha Mzee Kenyatta na nchi za Uingereza na Marekani zilizounga mfumo wa utawala wa upebari.
Kulingana na ripoti za Shirika la Ujasusi la Marekani CIA wakati huo , Bw Oginga alidaiwa kuanza kununua silaha kutoka Urusi na China kwa lengo la kupindua serikali ya Mzee Kenyatta.
Akiungwa na Urusi na China, Bw Oginga alianza kukosoa serikali ya Mzee Kenyatta. Mnamo 1966, alijizulu kama makamu wa rais na waziri wa masuala ya ndani na akaanza kukosoa vikali serikali ya Mzee Kenyatta.
Mnamo Oktoba 25, 1969, Mzee Kenyatta alienda Kisumu kufungua hospitali iliyofahamika kama Russia Hospital (sasa hospitali ya eneo la Nyanza) ambapo wafuasi wa Jaramogi walishambulia msafara wake.
Uchaguzi Kenya 2022:Unaweza pia kusoma
UNAYOFAA KUJUA:Uchaguzi Kenya 2022: Je Naibu wa rais wa Kenya William Ruto anakabiliwa na changamoto gani katika kumteua naibu wake wa rais?
Mwaka huo, Bw Oginga na washirika wake walitiwa mbaroni na chama chake cha Kenya Peoples Union kikapigwa marufuku.
Katika uchaguzi mkuu wa 1974, Be Oginga aliamua kugombea kiti cha eneo bunge la Bondo lakini hakuruhusiwa. Kenyatta hakuwa akimwamini.
Watoto wa viongozi hao wawili walikutana tena katika serikali ya muungano chini ya Rais Mwai Kibaki 2007, Raila akiwa Waziri Mkuu naye Uhuru akiwa Naibu wake.
Walishindana kwenye uchaguzi mkuu wa 2013 ambapo Uhuru alimshinda Raila na historia ikajirudia 2017.
Daniel Moi
Yeye alikuwa mwanasiasa aliyetaka kupendwa zaidi na wananchi kuliko alivyokuwa mtangulizi wake, rais wa kwanza wa Jamhuri ya Kenya Mzee Jomo Kenyatta.
Hata hivyo alishindwa kumaliza baadhi ya mambo yaliyoonekana kuitia dosari serikali ya mtangulizi wake Jomo Kenyatta na badala yake yeye mwenyewe akajikuta katika hali ya kuwadhulumu wapinzani wake wa kisiasa.
Moi alikuwa mmoja wa wanasiasa wachache mashuhuri waliofanikiwa, ambaye hakutoka katika mojawapo ya makabila mawili makubwa nchini Kenya.
Machi 1957 Moi alikuwa mmoja wa watu weusi wanane waliochaguliwa kuwa wanachama wa Bunge la Ukoloni kwa Kiingereza Legislative Council ambalo kwa kifupi lilifahamika kama LegCo.
Mapema mwaka 1960 alikuwa mmoja wa wajumbe walioteuliwa kuhudhuria mkutano katika Lancaster House jijini London, ambapo Katiba mpya iliandaliwa na kuwapa Waafrika viti vingi katika Bunge.
Kenyatta alipofariki Agosti mwaka 1978, Moi aliyekuwa makamu wa Rais alichukua wadhifa wa kaimu Rais. Mara tu alipotwaa madaraka hayo alisema kuwa ataendelea na uongozi wa Kenyatta ulioegemea uongozi wa mataifa ya Magharibi, angefuata nyayo.
Mnamo Oktoba alichaguliwa kwa wingi wa kura kuongoza chama cha kisiasa cha pekee nchini Kenya wakati huo(KANU) ambapo alichaguliwa pia kuwa Rais wa Pili wa Kenya.
Raila Odinga
Kama hayati babake, Jaramogi Oginga Odinga, Raila aliishi kukamatwa na kuachiliwa mara kwa mara tangu mwaka 1982 hadi 1991 kwa harakati zake za kupigania mageuzi wakati wa muhula wa pili wa utawala wa rais Daniel arap Moi.
Kufuatia kuidhinishwa kwa katiba mpya, mwezi Agosti, mwaka 2010, amekuwa akisema kwenye kampeni zake kuwa nia yake ni kuleta mageuzi ya kisiasa na pia kumaliza ufisadi.
Bw Odinga ni mwanasiasa anayesifika sana kwa ushawishi wake kisiasa na amekuwa katika msitari wa mbele kuunda vyama vya miungano na wanasiasa ambao ni mahasimu wake.
Baada ya uchaguzi wa mwaka 1997 ambapo Raila alishikilia nafasi ya tatu, kufuatia kuundwa kwa muungano wa chama chake (NDP) na chama cha rais wa zamani Daniel Moi (KANU), aliteuliwa kama waziri wa kawi katika serikali ya muhula wa mwisho wa Moi.
Mwaka 2002, baada ya Moi kumuunga mkono Uhuru Kenyatta, kama mrithi wake, Raila na maafisa wengine wa KANU ikiwemo Kalonzo Musyoka na wafuasi wengine, walipinga ungwaji mkono wa Kenyatta kugombea Urais.
Waliungana na kiongozi wa upinzani Mwai Kibaki na kuunda muungano wa National Rainbow Coalition (Narc) ambao baadaye ulishinda uchaguzi wa mwaka 2002.
Raila aliungana na Rais Mwai Kibaki kuunda serikali ya Muungano ya NARC baada ya kumuondoa mamlakani rais mstaafu Daniel Moi.Miaka kadhaa baadaye Raila sasa anajipata katika hali ya kipekee,anaungwa mkono na rais Uhuru Kenyatta na Seneta Gideon Moi ,viongozi wawili ambao familia zao zina historia ndefu pamoja katika mchakato wa siasa za Kenya na huenda simulizi ya ushirikiano huo itazidi kuwa sehemu ya mijadala na historia hata baada ya uchaguzi wa mwaka huu.