Urusi na Ukraine: Hujui kinachokuja - Joe Biden amwambia Putin

Iliyochapishwa

Rais wa Marekani Joe Biden ameliambia bunge la Congress kwamba rais wa Urusi Vladimir Putin alikosea kimtazamo kuhusu namna nchi za Magharibi zingejibu mapigo wakati alipoivamia Ukraine.

Katika hotuba yake hiyo, Bwana Biden aliapa "uamuzi usioyumba kwamba daima uhuru utashinda dhidi ya udhalimu".

Hotuba hiyo inakuja wakati Wamarekani wanaonekana kuchoshwa na janga linalowafanya kukabiliana na mfumuko wa bei.

Rais huyo wa chama cha Democratic aliwaambia wabunge Jumanne usiku: "Vita vya Putin vilipangwa na havina sababu. Alikataa juhudi za mara kwa mara katika diplomasia.

"Alidhani nchi za Magharibi na NATO zisingechukua hatua. Na, alidhani angeweza kutugawanya hapa nyumbani.

"Putin alikosea. Tulikuwa tayari."

Bwana Biden alitangaza kuwa Marekani itapiga marufuku ndege za Urusi katika anga yake, kama zilivyofanya mamlaka za Canada na Ulaya.

Akisisitiza vikwazo zaidi vya kiuchumi dhidi ya Urusi, rais wa Marekani alisema kuhusu Putin: "Hajui nini kinakuja."

Rais huyo wa Marekani pia alimkaribisha balozi wa Ukraine Oksana Markarova, ambaye alikuwa amekaa katika sehemu ya VIP ya mke wa rais wa Marekani, Jill Biden kwa ajili ya tukio hilo.

Hotuba hiyo ya rais kuhusu taifa, tukio la kila mwaka linalotumika kuzungumzia masuala muhimu kwa taifa na linalosukuma ajenda ya rais. Tukio hili linakuja wakati umaarufu wake binafsi ukishuka katika.

Ni asilimia 40.6 tu ya Wamarekani wanafurahishwa na kazi anayoifanya, kwa mujibu wa kura za maoni za RealClearPolitics. Ingawa kiwango cha ukosefu wa ajira cha Marekani kimepungua hadi 4%, mfumuko wa bei umefikia kiwango cha juu katika miaka 40.

Kiwango cha mauaji ya taifa kimeongezeka hadi kiwango cha juu katika miaka 25.

Kura za maoni zinaonyesha Wamarekani kutofurahishwa na jinsi Biden anavyolishughulikia janga la virusi vya corona na hatua ya Marekani kujiondoa kutoka Afghanistan mwaka jana.

Rais huyo alionyesha huruma huruma kwa familia zinazofanya kazi kwa bidii, akisema: "Mfumuko wa bei unaathiri kipato chao. Nafahamu."

Aliahidi mpango wa "kuijenga Marekani bora".

Bwana Biden alisema njia bora ya kukabiliana na kupanda kwa bei za walaji ni kuongeza uzalishaji wa ndani wa magari na kujenga upya barabara na madaraja ya taifa hilo.

Lakini kilichotawala zaidi ufunguzi wa hotuba yake ni mgogoro wake mkubwa wa sera za kigeni na uvamizi wa Ukraine.

Saa chache kabla ya hotuba yake, Bwana Biden alizungumza na rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kujadili ni msaada gani wa Marekani ambao anaweza kuipatia nchi yake baada ya siku sita za mashambulizi ya Urusi.

Urusi yaishambulia Ukraine:Mengi zaidi