Mbowe na wenzake watatu wana kesi ya kujibu-Mahakama

Mwenyekiti wa chama cha upinzani Tanzania Chadema Freeman Mbowe na wenzake watatu wana kesi ya kujibu .
Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi imesema Mbowe na wenzake watatu ambao walikuwa wanajeshi wa jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ), Mohamed Ling'wenya, Halfan Bwire na Adam Kasekwa wana kesi ya kujibu kuhusiana na tuhuma mbalimbali zikiwemo za kupanga njama za kufanya vitendo vya kigaidi.
Hatua hiyo inakuja baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wake kwa kuwaita mahakamani mashahidi 13 kati ya 24 iliokuwa imepanga kuwaita, huku ikitoa vielelezo 39.
Walipofika katika Mahakama washtakiwa hao walilakiwa na wafuasi na wanachama wao wa Chadema .Ulinzi mkali uliimarishwa pia nje ya mahakama .
Jaji Joachim Tiganga ndiye anayesikiliza kesi ya ugaidi inayomkabili Mbowe na wenzake watatu .
Tangu kesi hiyo ianze, imesikilizwa na majaji watatu; Elinaza Luvanda, Mustapher Siyani na Joachim Tiganga.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi tarehe 4 Machi 2022.
Kwa upande wa Jamhuri, mawakili ni Robert Kidando, Pius Hilla, Abdallah Chavula, Jenitreza Kitali, Nassoro Katuga, Esther Martin, Tulimanywa Majige na Ignasi Mwinuka.
Upande wa utetezi wamekuwa na jumla ya mawakili 26 wakiongozwa na Peter Kibatala, baadhi yao ni Nashon Nkungu, John Mallya, Dickson Matata, Fredrick Kihwelo, Faraji Mangula, Sisty Aloyce, Michael Mwangasa, Gaston Garubindi, Seleman Matauka, Maria Mushi, Hadija Aron, Idd Msawanga.
Jumatano, Agosti 19, 2020 Halfan Bwire Hassan, Adam Hassan Kasekwa na Mohamed Abdallah Ling'wenya walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa makosa saba waliyodaiwa kuyatenda kati ya Mei 1 na Agosti 1, 2020.
Pia, walidaiwa kukutwa na silaha, vilipuzi, sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na dawa za kulevya aina ya heroin.
Usiku wa kuamkia Julai 21 2021, polisi waliwakamata watu 11 kwenye Hoteli ya Kingdom mjini Mwanza na siku iliyofuata walithibitisha kuwakamata viongozi 15 wa Chadema akiwamo mwenyekiti wao, Mbowe.
Haya ni matukio muhimu ya kesi hii inayofuatiliwa kwa ukaribu ndani na nje ya nchi:
Julai 21, 2021: Mbowe alikamatwa
Kiongozi huyu mkuu wa Chadema alitiwa mbaroni huko jijini Mwanza usiku wa kuamkia tarehe 21 mwezi Julai, 2021. Chama chake cha Chadema, kiliwataka wafuasi wa chama hicho kuingia mtaani kumtafuta baada ya juhudi zake za kumtafuta kukwama na hawajui walipo, baada ya Mamlaka kutosema lolote kwa muda kuhusu kukamatwa kwa Mbowe. Baadae Polisi walikuja kuthibitisha kumkamatwa na kwamba amesafirshwa kutoka Mwanza kwenda Dar es Salaam na kuunganishwa kwenye kesi ya ugaidi.
Taarifa ya Msemaji wa Polisi, David Misime ilisema kuwa Mbowe hakukamatwa kwa tuhuma za kupanga na kuandaa kongamano la Katiba mpya jijini Mwanza bali alifahamu tuhuma zinazomkabili.
Julai 26, 2021: Kufikishwa mahakamani
Mbowe alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa mara ya kwanza Julai 26, 2021 na kusomewa mashtaka mawili ikiwemo la ugaidi. Baada ya kusomewa maelezo Mbowe hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka, kesi ikahairishwa hadi Agosti 5, 2021 kusubiri nyaraka ili ihamishiwe Mahakama kuu.
Agosti 6, 2021 Asomewa Mashitaka
Mbowe ambaye ni kiongozi wa zamani wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni (KUB) na wenzake watatu walisomewa mashtaka sita yakiwemo ya kufadhili vitendo vya ugaidi na kukusanya pesa kwa kufanya vitendo hivyo.
Mashtaka mengine ni kukusanya fedha kwa ajili ya kufanya vitendo vya kigaidi, kukutwa na silaha aina ya bastola na kukutwa na sare za jeshi kinyume cha sheria. Kati ya mashtaka hayo sita, Mbowe anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kula njama na kufadhili vitendo vya kigaidi.
Agosti 9, 2021: Rais Samia azungumzia Kesi ya Mbowe
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan licha ya kusema hawezi kuzungumzia zaidi kesi ya Mbowe kwa kuwa iko Mahakamani, aliiambia BBC kuwa mashtaka dhidi ya kiongozi huyo wa Upinzani hayakuchochewa kwa sababu za kisiasa.
Pamoja na mengine kauli yake hiyo iliibua mjadala mzito kwa wafuatiliaji wa kesi hiyo na siasa za Tanzania kwa ujumla.
Septemba 03, 2021: Kuanza kusikilizwa kwa kesi
Kesi hii ilianza kusikilizwa kwenye Mahakama kuu ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ikitokea Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu ambayo haikuwa na mamlaka ya kusikiliza kisheria.
Septemba 6, 2021: Jaji Luvanda ajitoa kusikiliza kesi
Jaji Elinaza Luvanda alijitoa kusikiliza kesi hiyo kufuatia maombi ya Mbowi, kwa niaba ya washitakiwa wenzake kudai kuwa hawana Imani na Jaji huyo kama atatenda haki. Nafasi yake akapangiwa Jaji Mustapha Siyani.
Oktoba 20, 2021 Jaji Siyani ajitoa kusikiliza kesi
Jaji Mustapha Siyani alikuwa jaji wa pili kujitoa kusikiliza kesi hiyo kufuatia kuteuliwa kwake kuwa Jaji kiongozi. Jaji Joachim Tiganga akachukua nafasi yake
Februari 13, 2022: Ushahidi kufungwa
Ushahidi umefungwa Wiki hii Februari 13, 2021 kwa mashahidi 13 wa upande wa mashtaka kumaliza kutoa ushahidi wao. Kinachosubiriwa sasa ni uamuzi wa Mahakama Kuu hiyo kuamua leo kama Mbowe na wenzie wana kesi ya kujibu ama la.














