Aceredo: mji wa nchini Uhispania ulioibuka kutoka majini baada ya miongo mitatu

Iliyochapishwa

Bwawa la maji la Lindoso, kwenye mpaka kati ya Uhispania na Ureno, lilizamisha mji wa Aceredo huko Galicia mnamo 1992.

Ilikuwa Januari 8 mwaka huo ambapo kampuni ya Ureno ya kuzalisha umeme kwa maji ya EDP, ambayo inasimamia bwawa hilo, iliendelea kujaza ziwa la hifadhi.

Siku hiyo Aceredo iligandishwa kwa wakati na mtindo mzima wa maisha kwa wakazi wake ulifikia mwisho.

Miongo mitatu baadaye, ukame mkali umeliribia kulimaliza ziwa, na kufichua mabaki ya nyumba zilizofurika.

Ni mandhari inayosonga, ya kuvutia na ya upweke kwa wakati mmoja, ambayo kwa sasa inavutia mamia ya watalii, Wahispania na Wareno.

"Tulitoka Vigo, tuliona mji ulioibuka na tukaamua kusimama ili kuuona. Tulikuwa tumeona kitu kwenye televisheni, lakini kukiona 'katika situ' kunavutia," mgeni aliliambia shirika la habari la Efe.

Kwa wengine, hata hivyo, mji ulioibuka ni tukio ambalo husababisha huzuni. "Ni kama ninatazama filamu. Nina hisia za huzuni," Maximino Pérez Romero aliiambia Reuters.

"Hisia zangu ni kwamba hili ndilo litakalotokea kwa miaka mingi kwa sababu ya ukame na hayo yote, na mabadiliko ya hali ya hewa."

José Álvarez, mwanzilishi wa zamani kutoka Lobios, alisema alihisi mchanganyiko wa kutamani na kufa alipokumbuka siku zake za kufanya kazi huko Aceredo. "Inatisha, lakini ndivyo ilivyo. Hayo ndiyo maisha. Wengine wanakufa na wengine wanaishi," Álvarez aliiambia Reuters.

"Walizungumza nasi vizuri sana na tukaamua kuja, inafaa kuona, ni kana kwamba ulikuwa kwenye eneo la mwezi. Lakini watu waliolazimika kuondoka pia wana huzuni sana, ilibidi wapate wakati mbaya sana. " alisema Maribel Paz, mgeni mwingine, kwa Efe.

Wakazi wa maeneo ya karibu zaidi ambao walijua kile kilichotokea Aceredo wanakosoa mabadiliko yaliyotokea Galicia kutokana na hifadhi.

"Hili ni janga, linaonesha jinsi walivyoimaliza vibaya hifadhi. Ninasikitika sana kwa uporaji waliofanya kwenye hifadhi," Francisco, mkazi wa Xinzo de Limia (Ourense), aliliambia shirika la EFE.

María del Carmen Yáñez, meya wa baraza la Mameya wa Lobios, ambalo Aceredo ni mwanachama, alilaumu hali hiyo kutokana na ukosefu wa mvua katika miezi ya hivi karibuni, haswa Januari, lakini pia kwa kile alichoelezea kama "unyonyaji mkali" na kiwanda cha kuzalisha umeme kwa maji cha EDP.

Mnamo Februari 1, serikali ya Ureno iliamuru mabwawa sita, pamoja na Lindoso, karibu kuacha kutumia maji kwa uzalishaji wa umeme na umwagiliaji, kutokana na ukame unaozidi kuwa mbaya.

EDP haikusema lolote ilipowasiliana na Reuters.

Maswali kuhusu uendelevu wa hifadhi si mapya. Mwaka jana, miji kadhaa ya Uhispania ililalamika kuhusu kampuni za huduma za Umma kwa kuchukua maji kutoka kwenye maziwa.

Takwimu kutoka Wizara ya Mazingira zinaonesha kuwa hifadhi za Uhispania ziko katika 44% ya uwezo wake, chini ya wastani wa karibu 61% katika muongo uliopita, lakini bado juu ya viwango vilivyorekodiwa katika ukame wa 2018.

Chanzo cha wizara kilisema viashiria vya ukame vinaonesha uwezekano wa kuwa mbaya zaidi katika wiki zijazo, lakini bado hawajagundua tatizo lililoenea kote nchini.