Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Nimetenda dhambi': Mtawa wa Marekani afungwa jela mwaka mmoja kwa wizi wa dola 835,000
Alikuwa akificha jambo la siri kwa miaka mingi .
Mary Margaret Kreuper, mtawa mstaafu, alikiri kwamba alivunja kiapo chake cha umaskini kwa kuiba $835,000 (£616,000) kutoka shule ya California ambako alifanya kazi ili kufadhili michezo yake ya kamari .
Kreuper, 80, atatumikia kifungo cha mwaka mmoja na siku moja kwa ulaghai wa kuiba pesa kupitia njia ya elektroniki na utakatishaji fedha.
"Nimetenda dhambi, nimevunja sheria na sina visingizio," alisema katika hukumu yake huko Los Angeles.
Kwa zaidi ya muongo mmoja, Kreuper alifuja pesa kutoka kwa masomo na michango kwa Shule ya Kikatoliki ya St James ambapo alikuwa mkuu.
Kisha aliwaagiza wafanyikazi wengine wa shule "kubadilisha na kuharibu rekodi za kifedha" ili kuficha uhalifu wake.
Pesa hizo, ambazo kulingana na waendesha mashitaka zingeweza kulipia karo ya shule kwa zaidi ya wanafunzi kumi na mbili, zilitumika kwa safari za kwenda kasino na likizo kwa Kreuper na marafiki zake.
Mpango huo ulifichuliwa wakati wa ukaguzi baada ya Kreuper kustaafu mnamo 2018.
Katika kutangaza hukumu yake, Jaji wa Mahakama ya Wilaya ya Marekani, Otis D Wright II, alisema alijitahidi kupima adhabu ya kisheria dhidi ya maombi ya msamaha kutoka kwa familia za Kikatoliki ambao watoto wao walifundishwa huko St James. Alimuamuru Kreuper kutumia miezi 12 na siku moja gerezani, na kulipa shule hiyo $835,339 kama marejesho.
Kreuper alimwambia hakimu kwamba "amesikitika sana" na angetumia maisha yake yote kujaribu kufuata "kwa ukaribu zaidi katika nyayo za Kristo".
Mawakili wake walisema amekuwa akiugua ugonjwa wa akili ambao "ulififisha uamuzi wake".