Polisi wa siri wa Sudan wanaogopwa wamerejea tena

Iliyochapishwa

Katika mfululizo wa barua zetu kutoka kwa waandishi wa habari wa Afrika, mwandishi wa Sudan Zeinab Mohammed Salih anaangalia kurejeshwa kwa hatua za usalama zilizohofiwa ambazo zilikuwa zimefika kikomo baada ya kuondolewa madarakani kwa Rais Omar al-Bashir.

Polisi wa siri wa Sudan waliokuwa na sifa mbaya wamerejea kazini, wakiwateka nyara watu ambao inahofiwa hawataweza kuonekana tena.

Mwezi uliopita, katikati ya usiku wa manane, takriban watu 30 wenye silaha waliovalia mavazi ya kawaida walivamia nyumba ya Amira Osman huko Khartoum.

Mhandisi aliyefunzwa ni mwanaharakati mashuhuri wa haki za wanawake hapa.

Yeye pia ni mwanachama wa Chama cha Kikomunisti cha Sudan.

Inaaminika kuwa alikamatwa na Huduma ya Ujasusi (GIS) ambayo zamani ilijulikana kama Huduma za Kitaifa za Ujasusi na Usalama (NISS) lakini mamlaka haijatoa taarifa yoyote.

Dada mkubwa wa Bi Osman, Amani, ambaye ni wakili wa haki za binadamu, alieleza kilichotokea.

"Tulishangaa," aliniambia.

"Watoto wangu na wapwa zangu walishikwa na hofu walipowaona wanaume wakiwa na bunduki aina ya Kalashnikov, baadhi yao wakiwa wamebeba fimbo ili tu kumkamata.

"Mwanangu mwenye umri wa miaka sita sasa anapata shida ya kulala, kwasababu alichokiona kilimsababishia kumbukumbu ya kukamatwa kwangu alipokuwa na umri wa miaka mitatu tu."

"Nilitoweka kwa siku 38 bila kuwaona watoto wangu," Amani aliongeza.

"Lakini jambo la kusikitisha ni kwamba, tunapitia hayo tena.

Tulidhani kwamba baada ya kuanguka kwa utawala wa Bashir hatutakumbana tena na kitu kama hicho, lakini tuko tayari kwa hilo."

Amani alisema askari hao wa usalama hawakutishia familia yake tu, bali pia walimtishia mmiliki wa duka hilo kwenye kona ya nyumba yao na majirani zao pia.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan umetaka Amira aachiliwe huru.

Kukamatwa kwake ni moja tu kati ya kadhaa tangu Desemba, wakati GIS iliruhusiwa, kwa mara nyingine tena, kuchukua watu bila kufahamisha familia zao, au wanasheria, waliko.

Hadi sasa, mwanaharakati mwingine mashuhuri wa haki za wanawake mjini Khartoum na makumi ya kamati za upinzani za kitongoji zinazoandaa maandamano dhidi ya watawala wa kijeshi wa Sudan wamekamatwa.

Wanajeshi walionyakua mamlaka mnamo Oktoba walirejesha mamlaka ya polisi wa siri ili kuzuia wimbi la maandamano ambayo yameikumba nchi hiyo tangu wakati huo.

Waandamanaji hao wanadai kurejeshwa kwa utawala wa kiraia, wakiwashutumu viongozi wa kijeshi kuwa na uhusiano wa karibu na utawala wa Bashir, ambaye alipinduliwa baada ya ghasia za mwaka 2019.

Tangu wakati huo, nchi hiyo ilikuwa ikiongozwa na muungano usio na utulivu unaojumuisha raia na wanajeshi ambao hatimaye ndio waliomuondoa Bashir madarakani.

Mwanaharakati wa haki za wanawake, Eman Mirghani, ambaye ni mjumbe wa kamati za upinzani na mfanyakazi wa serikali ya mtaa, alichukuliwa na watu wasiojulikana kutoka karibu na sehemu yake ya kazi.

Wanahadaiwa na kukamatwa

Wale waliomchukua walikuwa wa GIS, kulingana na watu aliofanya nao kazi katika wizara ya afya ya jimbo la Khartoum.

Bi Mirghani alishawishiwa kutoka ofisini kwake kwa simu.

Ilikuwa ni mtu aliyejifanya kuwa mfanyakazi mwenzao ambaye alisema kwamba walihitaji kumuona nje.

Aliondoka ofisini na kulazimishwa kuingia kwenye gari jeupe na kupelekwa mahali pasipojulikana, walioshuhudia walisema.

Mwanawe wa kiume, Karim Ali aliniambia kuwa mama yake alikamatwa kwasababu ya kampeni yake na "kuandaa uasi wa raia kwenye wizara dhidi ya mapinduzi."

Idadi kamili ya waliokamatwa haijabainika - lakini wanaharakati wanaamini kuwa watu 70 wamechukuliwa na GIS na wala si familia zao wala mawakili wao wanaojua walipo.

GIS ilibadilishwa jina baada ya kuondolewa kwa Bashir. Pamoja na jina jipya, mamlaka yake ya kukamatwa yalipunguzwa.

Katika muundo wa awali - kama NISS - ilipata umaarufu katika miaka ya 1990 kwa kile kinachoitwa "nyumba za shetani"

Hivi vilikuwa vyumba vya mateso ambapo maelfu ya wapinzani wa rais walinyanyaswa na wakati mwingine kuuawa.

Katika tukio moja, mwalimu Ahmed el-Khair alichukuliwa kutoka kwa nyumba yake mnamo Februari 2019 na kisha kuteswa hadi kufa.

Mwaka mmoja baadaye, baada ya kuanguka kwa utawala wa Bashir na wakati wa kipindi cha mpito ambacho kilipaswa kuanzisha enzi ya kidemokrasia, wauaji wa Khair walihukumiwa kifo.

Lakini hukumu hizi hazijatekelezwa.

Mjumbe wa zamani wa tume ya haki za binadamu ya Sudan, wakili Samier Ali Maceen, anahofia kurejeshwa kwa mamlaka ya GIS "inawakilisha kurudi nyuma kwa haki za binadamu na uhuru wa kimsingi" baada ya mapinduzi ya Oktoba.

Ni ishara nyingine kwamba mambo yanarejea kama yalivyokuwa, kabla ya kupinduliwa kwa Bashir kulisababisha imani kuwa Sudan tofauti inawezekana.

Kuhusu Amira Osman, dadake anasema kuwa bado hajulikani aliko.

Familia yake inaeleza kilichotokea kama utekaji nyara.

"Hawakumruhusu hata kunywa dawa," dadake anasema.

Barua za Afrika: