Maafisa wa Polisi kupisha uchunguzi kuhusu mauaji ya Mtwara, Kilindi Tanzania

Iliyochapishwa

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameunda timu maalumu ya watu tisa ambayo imepewa jukumu la kuchuguza mauaji yaliyofanyika Mtwara na Kilindi Tanga.

''Kamati hiyo inapaswa kuanza kazi yake kesho na inatakiwa iwe imekamilisha ripoti yake ndani ya siku 14,'' amesema Waziri Mkuu ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alilolitoa leo akiwa mjini Magu, Mwanza.

Rais Samia amesema anatambua Jeshi la Polisi limeunda kamati ya uchunguzi lakini ameagiza iundwe kamati iliyo huru ili ikafanye uchunguzi wa mauaji ya Mtwara yaliyofanywa na polisi.

Mauaji ya Mtwara yalitokea Januari 5 na mauaji ya Kilindi yalitokea Januari 30 mwaka huu.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, Kamati hiyo ina maafisa wenye dhamana kutoka mamlaka tofauti za serikali ikiwemo Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Rais, TAKUKURU, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Katika hatua nyingine Bw. Majaliwa amuemuagiza Inspekta Jenerali wa Polisi Simon Sirro awasimamishe kazi maafisa wa Polisi wa Mtwara na Kilindi ili kupisha uchunguzi wakati timualiyoiunda ikifanya kazi yake.

''Viongozi hawa wanapaswa wake pembeni, watahojiwa na hii timu wakiwa nje ya ofisi,'' amesema Waziri Mkuu na kuwataja maafisa hao kuwa ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara (RPC), Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Mtwara (RCO) na Mkuu wa kituo cha Polisi Mtwara cha eneo alilofia mfayabiashara Mussa Hamisi Hamisi na Mrakibu Msaidizi wa Polisi Greysona Mahenge anayedaiwa kujinyonga.

Pia ameagiza Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Kilindi na Afisa wa Upelelezi wa wilaya nao wakae pembeni kupisha uchunguzi.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amekemea matukio ya mauaji ambayo yamekua yakiripotiwa katika siku za hivi karibuni nchini Tanzania, amesema kuwa kamati maaulum itachunguza chanzo cha mauaji hayo.

Hivi karibuni Tanzania imerekodi idadi ya mauaji katika mikoa kadhaa ikiwemo Mtwara, Mbeya, Mwanza, Moshi na Dodoma.

"Nimemuelekeza Waziri Mkuu, aunde kamati nyingine iende ikafanye uchunguzi wa mauaji yaliyofanywa na Jeshi la Polisi alafu watuletee taarifaa, lakini wakati huo huo, nataka Jeshi lako lijitafakari waone kinachotokea ni misingi ya jeshi la polisi''. Alisema Rais Samia.