Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Tulia Ackson: Je, ni zipi changamoto na matarajio kwa Spika huyu wa Tanzania?
- Author, Markus Mpangala
- Nafasi, Mchambuzi, Tanzania
- Iliyochapishwa
Tulia Ackson Mwanasasu, amechaguliwa kuwa Spika wa saba na sasa ni mwanamke wa pili kuliongoza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu ilipopata uhuru mwaka 1961. Tulia ametanguliwa na Chifu Adam Sapi Mkwawa, Chifu Erasto Mang'enya, Pius Msekwa, Samwel Sitta, Anne Makinda na Job Ndugai. Lakini kiongozi huyu mpya anakabiliwa na changamoto nyingi na matarajio toka kwa wabunge na wananchi, namna gani anaweza kuendesha Bunge lenye ushawishi, kusimamia serikali, kurejesha heshima machoni mwa wananchi na demokrasia licha ya kuwa na Wabunge wa chama kimoja.
Duru za kisiasa zinasema miongoni mwa changamoto kubwa inayomkabili Spika huyo ni namna atakavyoweza kuweka uwiano wa kulinda maslahi ya Bunge, wabunge, wananchi na serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake kwa kipindi cha miaka mitano 2015-2021.
Pia imeelezwa changamoto nyingine kwa Spika huyo ambaye amewahi kuwa Naibu Spika ni kuegemea siasa za chama tawala CCM. Wengi wanatarajia kuona nini atakachokifanya baada ya kukachukua madaraka haya kwa kipindi cha 2022-2025.
Ushindi aliopata katika kinyang'anyiro cha Uspika unadhihirisha namna Bunge la Tanzania lilivyogota kwenye kona ya chama kimoja na kwamba Wabunge kwa kura 376 wametoa msimamo wa kulinda maslahi ya chama chao kwanza kuliko kuweka demokrasia ya aina yoyote kwa kuwapa kura angalau chache wagombea wa vyama vidogo na visivyo na nguvu ambavyo viliweka wagombea wao.
Ni mambo gani yanayotarajiwa kwa Spika mpya?
Mojawapo ya maswali yanayoulizwa ni hili; Je kwa kiasi gani wananchi wana imani na yapi matarajio kwa Spika huyo? Madhumuni yanalenga kupata mtazamo wa taswira binafsi ya Spika na Bunge analokwenda kuliongoza kwa sababu rekodi zinaonesha amekuwa akizua mivutano mara kwa mara kwa kuikingia kifua serikali wakati akiendesha vikao vya Bunge alipokuwa Naibu Spika.
Mosi, asilimia 99 ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaundwa na Wabunge wa chama tawala CCM. Hivyo inatarajiwa angalau kidogo huenda uongozi wake ukulifufua Bunge kurejesha utamaduni wa kuhoji na kusimama kidete dhidi ya mipango mibovu ya maendeleo inayowasilishwa na serikali.
Pili, kudumisha demokrasia ni jambo ambalo linaangaliwa kwa umakini ikizingatiwa kuwa hata wabunge wakosoaji toka ndani ya CCM wamekuwa wakinyimwa nafasi ya kufurukuta tangu zama za Job Ndugai, huku Naibu huyo katika nafasi alizopata kuongoza vikao vya Bunge amewahi kulalamikiwa kwa kutowapa nafasi.
Tatu, suala la haki na usalama, Spika ndiye mlinzi wa kwanza wa Bunge na Wabunge, lakini katika kipindi cha Unaibu wake baadhi ya wabunge wamepitia wakati mgumu katika shughuli zao. Akiwa Naibu Spika, ndicho kipindi ambacho aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alishambuliwakwa rasasi na watu wasiojulikana mnamo Septemba 7 mwaka 2017, kisha akafukuzwa ubunge kwa madai ya utoro.
Pengine wakati yanatokea hayo angejitetea kukosa mamlaka kisheria, lakini sasa anamamlaka kamili na anatakiwa kusafisha taswira hasi iliyolizingira Bunge, na kwamba atakuwa mstari wa mbele kufikia matarajio ya wananchi ikiwemo kushughulikia masuala tata yaliyotia toa bunge.
Nne, kuondoa uhusuiano mbaya ama mgongano wa mihimili. Ni sababu hii Spika na Rais walipishana kauli hadharani kwa kile ambacho Mkuu wa serikali na mhimili mmoja unaamini unaweza kudhibiti mwingine. Kwamba Rais anaweza kudhibiti Bunge na hivyo likawa linakwenda vile serikali yake inavyotaka. Malumbano hayo ndio yalikuwa kiini cha Spika Ndugai kuachia ngazi na kuzua mjadala ikiwa Bunge la nchi hiyo linao uhuru wa kutosha kusimamia serikali. Inategemewa kuwa spika mpya ataimarisha uhusiano huo baina ya mihimili lakini pia kuondoa mivutano.
Tano, suala la wabunge ambao wanadaiwa kuwa si wanachama wa chama chochote, ni jambo linalotarajiwa kuangaliwa kwa umakini na spika huyu. Tulia Akson anatoka chama tawala je ataweza kufanya uamuzi mzito wa kuwaondoa au kuwabakiza bungeni kwa maslahi ya chama tawala kama ilivyofanywa na Ndugai.
Nimezungumza na Richard Ngaya, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha SUA na mchambuzi wa siasa na utawala bora anasema, kupata Bunge lenye ufanisi chini ya Spika Tulia ni vigumu kutokana na ukweli kuwa hali ya sasa ya Bunge haionyeshi kuwa linawakilisha na kuwatumikia wananchi kwa uwiano wa kidemokrasia ipasavyo.
"Tabia mpya iliyojengwa ndani ya chama na serikali ni kuwa serikali haipaswi kukosolewa mipango yake ya maendeleo iwe kwa wabunge ama watu binafsi. Mwisho kabisa yeye binafsi alishaonesha mtizamo wake juu ya nafasi ya mhimili wa bunge siku alipoamua kuchukua fomu. Mtazamo wake ni bunge la mihuri na sio kuibua hoja nzito za kuifanya serikali ifanye kazi kwa ajili ya nchi na wananchi. Spika anaweza kutumika kuwaziba midomo wabunge wachache wanaoweza kuhoji maswali yenye tija kwa kutumia kanuni na wafuasi wao waliopo bungeni. Bunge la 2022-2025 ni mwendelezo wa kile kilicholalamikiwa na aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za serikali Profesa Musa Assad kuwa Bunge ni dhaifu. Hii si taswira nzuri."
Ni Changamoto gani zinamkabili Spika mpya?
Mratiba wa Mtandao wa Utetezi wa Haki za Binadamu, Onesmo Olengurumwa ameniambia kuwa Dkt Tulia anakabiliwa na changamoto za kulinda hadhi na heshima ya Bunge pamoja na kuweka uwiano wa maslahi ya chama na serikali kwa wakati mmoja na hiyo ni kazi ya kwanza katika kiti chake.
"Jambo kubwa ni namna ya kuweka uwiano au mizani ya maslahi ya Rais na serikali na kulinda heshima na uhuru wa Bunge na Wabunge. Hapa Spika Tulia atakuwa na wakati mgumu mno kwenye uongozi wake huu. Bunge lina hamu ya kurudishiwa ule uhuru wake wa mijadala, ushawishi na mgongano wa hoja, wakati huo pia serikali ina mategemeo ya kuendelea kupata mlinzi bungeni kama ilivyokuwa kwa Spika Job Ndugai tangu 2015 hadi 2021.
"Kama wananchi wanadhani wabunge watakosa uvumilivu ikiwa Spika ataegemea upande wa serikali, inabidi wakumbushwe wanategemea wabunge gani hao? Ni wabunge hawa walioshindwa kumtetea Spika Ndugai na kumwacha azame mwenyewe? Ni Wabunge hawa walioshindwa kumbana Spika Ndugai wakati wa uongozi wa marehemu JPM? Changamoto ni kubwa mno aendako Spika huyu mpya." Olengurumwa
Aidha, Bunge linaendeshwa 'gizani' kwa maana halioneshwi moja kwa moja kwenye runinga na kufuatiliwa na wananchi kwa kipindi cha miaka sita sasa. Hii ni changamoto kwa Spika huyu kushawishi ama kutoa maelekezo ya kurejeshwa 'Bunge Live' ama liendelee kama lilivyo sasa ikizingatiwa waziri aliyetoa tangazo la katazo amerejeshwa madarakani, Nape Nnauye. Jamii itakuwa inamtazama anakabiliana nalo vipi jambo hili.
Je ni upi mustakabali wa Bunge?
Dhahiri Bunge ni la chama kimoja, Spika wa chama tawala na hana changamoto za kisiasa kutoka kwa vyama vya upinzani na pia limejenga utamaduni wa fikra za chama cha CCM; ili kulinda heshima ya Bunge ni lazima maslahi ya rais na serikali yalindwe. Kwa maana hiyo Wabunge wa CCM wanakuwa wawakilishi wa chama tawala zaidi kuliko masuala muhimu ya wananchi wao. Hapa ilipofikia Tanzania imeleta utamaduni mpya wa kukataza Wabunge na watu binafsi kukosoa mipango mibovu ya serikali. Na pale mtu anapo kosoa hutazamwa kama adui wa Rais.
Said Arfi, Mbunge wa zamani wa Mpanda Mjini kupitia chama ch upinzani cha Chadema, ameniambia kuwa, "Tanzania tunaishi katika zama mpya, tusubiri kuona na kusikia mapya. Lakini hapa tulipofikia Dkt.Tulia Ackson Mwansasu hakupaswa kuteuliwa katika nafasi hiyo kwa kigezo cha utendaji wake, akiwa Naibu Spika wananchi wameona na uhakika uliopo ni kwamba baadhi hawakuridhishwa nikiwemo mimi. Hivyo sitegemei kama atabadilika, nasema kwa sababu amekuwa na upande wake, alishachagua upande wa chama chake sidhani kama Bunge litakuwa msaada kwa ustawi wa Taifa na Demokrasia. Kimsingi wananchi wanatakiwa kuvumilia Bunge la chama kimoja hadi litakapofikia tamati, hakuna mabadiliko." Arfi
Hata hivyo yote haya hayamzuii Tulia Akson kuamua kuishangaza Tanzania kwa kusimama kidete katika kulinda maslahi ya bunge, wabunge, nchi na wananchi bila kuhofia wajibu wake katika chama tawala. Na hii huenda ikarudisha mara dufu hadhi ya Bunge na Imani ya watanzania kwa muhimili huu muhimu katika uundwaji wa sera na kutetea maslahi ya wananchi.