Allison Fluke-Ekren: Mwanamke wa Marekani anayeshikiliwa kwa kuongoza kikosi cha wanawake cha IS

Iliyochapishwa

Mwanamke Mmarekani amekamatwa na kushitakiwa kwa kupanga na kuongoza kikosi cha wanawake pekee cha kikundi cha Islamic State.

Allison Fluke-Ekren, mama ambaye aliishi katika Kansas, anadaiwa kuwa aliwapatia mafunzo wanawake na watoto ya kutumia bunduki aina ya AK-47 na fulana za vilipuzi nchini Syria.

Pia alishutumiwa kutoa mafunzi ambayo yangewezesha kufanyika kwa mashambulio katika vyuo vya Marekani siku zijazo.

Bi Fluke-Ekren anaweza kukabiliwa na kifungo cha hadi miaka 20 jela iwapo atapatikana na hatia.

Taarifa za mshukiwa huyo zilitolewa katika waraka wa mashitaka Ushahidi wa mashitaka wa FBI kuanzia mwaka 2019, ambao ulitolewa Jumamosi baada ya mshukiwa kurejeshwa nchini Marekani kukabiliana na mashitaka.

Inadaiwa kwamba katika mwaka 2016 bataliani ya wanawake pekee ya IS, inayofahamika kama Khatiba Nusaybah, iliundwa katika mji wa Raqqa, nchini Syria.

Wakati huo, mji huo ulikuwa mji mkuu wa kikundi cha Islamic State.

Kikosi hicho kinasemekana kuwa cha wajumbe wa IS wanawake pekee ambao walikuwa wameolewa na waiganaji wa kiume wa IS.

Bi Fluke-Ekren anashukiwa kuwa alikuwa kiongozi na muandaaji wa kikundi mara baada ya kujiunga na kikundi hicho.

Inadaiwa kuwa jukumu lake kubwa lilikuwa ni kuwafundisha wanawake kujilinda wenyewe dhidi ya maadui wa IS .

Inasemekana kuwa alifanikiwa katika kuwapatia mafunzo wanawake kadhaa wa IS ya kutumia bunduki ya AK-47, gurunadi na mikanda ya mabomu ya kujilipua.

Pia anashutumiwa kwa kuwafundisha watoto kutumia silaha, na katika ushahidi wa FBI mmoja wa mashahidi alinukuliwa akisema kwamba mmoja wa watoto wa kiume wa Bi Fluke-Ekren alionekana akiwa ameshikilia bunduki. Alikuwa na umri wa miaka 5 au 6 wakati huo.

Unaweza pia kusoma:

Pamoja na jukumu analoshukiwa kuwa nalo nchini Syria, Bi Fluke-Ekren pia anashukiwa kupanga mipango ya kushambulia vyuo nchini Marekani.

Pia anadaiwa kuwaambia mashahidi wake kuhusu nia yake ya kufanya shambulio kwenye duka kubwa kwa kutumia vilipuzi, na anaripotiwa kusema kuwa itakuwa ni kupoteza raslimali iwapo halitawauwa watu wengi.

Bi Fluke-Ekren inashitakiwa kwa kutoa na kula njama ya kutoa usaidizi wa vitu au raslimali kwa shirika la kigaidi la kigeni na anakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 20 jela iwapo atapatikana na hatia.