Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Uislamu ni sababu ya kufutwa kwangu kazi, anasema waziri wa zamani
Mbunge Muislamu anasema Kiranja mkuu alisema imani yake ilikuwa sababu iliyochangia afutwe kama waziri mnamo 2020.
Kwa mujibu wa gazeti la Sunday Times, Tory Nusrat Ghani alisema kwamba alipotaka maelezo aliambiwa kuwa "Uislamu ndio ulikuwa sababu".
Kiranja Mkuu wa chama cha Conservative Mark Spencer alisema Bi Ghani alikuwa akimrejelea na kuongeza kuwa madai yake ni ya uwongo mtupu.
Ofisi ya waziri mkuu ilisema Waziri Mkuu hapo awali alikutana na Bi Ghani kujadili madai yake.
Msemaji alisema Boris Johnson kisha alimwandikia barua akielezea wasiwasi wake na kumtaka kuanza mchakato rasmi wa malalamiko lakini hakufanya hivyo .
Akijibu, Bi Ghani alisema Bw Johnson alimuandikia kwamba hangeweza kuhusika na kupendekeza atumie mchakato wa malalamiko wa ndani wa Chama cha Conservative.
Alisema hakufanya hivi kwa sababu "haikuwa sawa kwa jambo lililotokea kwenye shughuli za serikali".
"Nilichotaka kutaka ni kwamba serikali yake ilichukulie hili kwa uzito, ichunguze ipasavyo na kuhakikisha hakuna mwingine atakumbwa na hili."
Bi Ghani aliteuliwa kushika wadhifa katika Idara ya Uchukuzi mnamo 2018, na kuwa waziri wa kwanza wa kike Mwislamu kuzungumza katika Bunge la Commons.
Alipoteza kazi hiyo katika mabadiliko madogo ya serikali ya Bw Johnson mnamo Februari 2020.
Akizungumza na gazeti la Sunday Times, Bi Ghani alisema kwamba alipotaka maelezo, kiranja wa serikali alimwambia kwamba "Uislamu ulitolewa kama sababu"
Mbunge huyo wa Wealden amenukuliwa akisema aliachana na suala hilo baada ya kuambiwa kwamba angeendelea kuuliza kuhusu hilo "taaluma yake na sifa vingeharibiwa".
Akizungumza na kipindi cha BBC waziri wa haki Dominic Raab alisema madai yake ni "mazito sana" lakini hakutakuwa na uchunguzi rasmi isipokuwa Bi Ghani atoe malalamiko rasmi.
Siku ya Jumamosi , Bw Spencer, katika ujumbe wa twitter, alijitambulisha kama mtu ambaye madai ya Bi Ghani yalitolewa juu yake.
Alisema shutuma hizo "ni za uwongo kabisa na za kukashifu" na akakana kuwahi kutumia maneno ambayo Bi Ghani alidai.
Bwana Spencer aliendelea kusema "ilivunja moyo" kwamba wakati huo alikuwa amekataa kupeleka suala hilo kwa uchunguzi rasmi wa Chama cha Conservative.
Alisema hapo awali alikuwa ametoa ushahidi kwa uchunguzi wa Singh - ambao ulichunguza jinsi Chama cha Conservative kilishughulikia malalamiko ya ubaguzi.
Waziri wa Afya Sajid Javid pia alisema suala hilo linahitaji "uchunguzi ufaao" na kwamba atamuunga mkono Bi Ghani "kutoa malalamiko rasmi". "Lazima asikilizwe," aliongeza.
Lord Sheikh, rais wa Conservative Muslim Forum, alisema "amesikitishwa sana" na kile Bi Ghani alisema.
"Kuna mtu hasemi ukweli. Ningependa kupata undani wa hili. Ningependa uchunguzi ufanywe na mtu huru," aliongeza.
Mwandishi wa masuala ya kisiasa wa BBC Damian Grammaticas alisema kuwekwa hadharani kwa mzozo huu ni ishara ya mvutano mkubwa kabla ya wiki muhimu kwa Boris Johnson.
Mtumishi wa umma Sue Gray anatarajiwa kukamilisha uchunguzi wake kuhusu karamu zilizoandaliwa katika majengo ya serikali wakati wa kufungwa kufuatia janga la corona.
Imeripotiwa kuwa Bi Grey sasa pia anaangalia mikusanyiko inayofanyika katika jumba la kibinafsi la Bw Johnson huko Downing Street.
Bw Raab alisema matokeo yatachapishwa lakini hakuweza kusema ikiwa ripoti kamili itawekwa wazi.
Baadhi ya wabunge wa chama cha Conservative wamemtaka Bw Johnson kujiuzulu kutokana na ufichuzi huo, na mjumbe mmoja, William Wragg, alilalamikia mbinu za serikali zilizotumiwa dhidi ya wabunge wanaotaka kumtimua waziri mkuu.