Rais Samia,Lukuvi,Kabudi na 'mbinu za kisiasa'

Chanzo cha picha, Ikulu Tanzania
- Author, Ezekiel Kamwaga
- Nafasi, Mchambuzi
- Iliyochapishwa
Hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania kutangaza majukumu mapya kwa mawaziri wawili aliowaondoa katika baraza lake jipya aliloliteua na kutangazwa Januari 8, 2022 mwezi huu imeibua maswali kuhusu 'mbinu'ambayo anataka kuitumia katika suala hilo.
Ingawa ni jambo la kawaida kwa Rais wa Tanzania kupanga na kupangua mawaziri wake kadiri anavyotaka, hatua ya Rais Samia hivi karibuni ni miongoni mwa mara chache ambazo uteuzi wa Rais unatazamwa katika namna ambayo hakuna jibu moja linaloweza kuwekwa bayana.
Katika baraza jipya la mawaziri lililotangazwa na Rais Samia Januari 8, mawaziri wawili; William Lukuvi na Profesa Palamagamba Kabudi, walikuwa ni miongoni mwa mawaziri ambao hawakurudi katika baraza na tayari maswali yalianza kuulizwa kuhusu sababu hasa za wawili hao kuondoshwa katika baraza hilo.
Rais Samia mwenyewe tayari amezungumza hadharani kueleza nini hasa ilikuwa sababu ya uamuzi wake. Siku ya kuwaapisha mawaziri wapya na waliobadilishwa wizara Januari 10 Ikuku Chamwino Dodoma, alisema; "Nataka niseme jambo moja tu nina kaka zangu, Lukuvi na Kabudi. Kaka zangu wawili hawa nimewavuta waje kwangu wanisaidie ili waje kunisimamia ninyi, kwa hiyo kuwaacha kwangu kwenye hiyo listi watakuja kwangu tuwasimamie ninyi".
Katika ufafanuzi wake, Rais alisema Lukuvi atasaidia katika shughuli za uratibu wa majukumu ya mawaziri na manaibu wao wakati Kabudi atakuwa akitoa ushauri katika masuala ya kisheria.
Kwa kawaida, hatua hiyo ya Samia ingetosha kabisa kumaliza minong'ono yote kuhusu sababu hasa za kuwaondoa vigogo hao kwenye baraza la mawaziri. Hata hivyo, kuna mambo machache ambayo yanafanya minong'ono na dhana mbalimbali ziendelee kujadiliwa. Mosi ikiwa kwamba, kimsingi, Rais hatakiwi wala hana sababu ya kutoa maelezo kwa umma kuhusu kwanini kamteua fulani kuchukua nafasi fulani. Kwamba Rais mwenyewe kaamua kutoa ufafanuzi, inaweza kumaanisha kwamba kunaweza kuwa na sababu zaidi ya ile aliyoitoa hadharani.
Kuhusu Kabudi na Lukuvi
Wawili hao ni wanasiasa wenye sifa na historia tofauti katika siasa za Tanzania. Lukuvi ni mwanasiasa aliyelelewa na kukulia katika siasa za Chama Cha Mapinduzi (CCM) - kuanzia kwenye Umoja wa Vijana (UVCCM) alikotumikia kufikia hatua ya Naibu Katibu Mkuu na kuingia bungeni mwaka 1995. Katika Bunge la sasa, yeye ndiye mbunge wa muda mrefu kuliko wengine wote akiwakilisha jimbo la Isimani mkoni Iringa. Amekuwa Waziri na pia kushika nyadhifa nyingine kubwa serikalini kama vile kuwa Mkuu wa Mkoa katika mikoa nyeti ya Dodoma na Dar es Salaam bila mashaka juu ya utendaji kazi wake.
Kabudi ni mwanasiasa ambaye alijulikana zaidi kama mmoja wa wahadhiri nguli wa sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alikojipambanua kama mmoja wa wasomi mashuhuri nchini. Aliingia katika siasa kupitia uteuzi wa hayati Rais John Magufuli katika awali yake ya kwanza na kisha yeye mwenyewe akajitosa kuwania ubunge na kushinda katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 katika Jimbo la Kilosa mkoani Morogoro.

Chanzo cha picha, Ikulu Tanzania
Kwa sababu hiyo, wawili hawa wanawakilisha makundi mawili tofauti ya kisiasa ndani ya CCM ya sasa - mmoja akiwakilisha CCM Asili na mwingine kundi ambalo linahusishwa moja kwa moja na "CCM Mpya" iliyotaka kujengwa na Magufuli. Kwa vyovyote vile, wawili hawa hawatoki katika makundi maslahi ndani ya CCM na ni wenye mitazamo, maarifa na ngome tofauti ndani ya chama.
Ingawa katika mojawapo ya hotuba zake za Januari mwaka huu Samia alizungumzia uwepo wa kundi la wana CCM wanaokwamisha juhudi zake za kuikwamua Tanzania kiuchumi na wakiwa na homa ya Uchaguzi Mkuu wa 2025, pasi na shaka yoyote kwamba ni mmoja tu kati yao angeweza - kama kweli kundi hilo lipo, kushiriki mbinu za kumkwamisha Samia na si wote kushiriki kwa sababu kwa asili hawako katika kundi moja.
Kitabia pia, Lukuvi na Kabudi ni aina ya watu ambao hawana historia ya kugombana na mamlaka. Lukuvi alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu wakati wa Uwaziri Mkuu wa Frederick Sumaye aliyewania urais ndani ya CCM akishindana na Jakaya Kikwete mwaka 2005. Ingawa kwa nafasi yake Lukuvi alionekana kuwa mfuasi wa Sumaye, Lukuvi alikuja kuibuka kwenye baraza la Kikwete.
Mwaka 2015, Lukuvi hakuwa akijulikana kuwa katika kundi lolote miongoni mwa waliokuwa wakiwania urais kupitia CCM lakini nilimshuhudia akimsindikiza Magufuli kwenda meza kuu baada ya chama chake kumpitisha kuwa mgombea wake wa urais mjini Dodoma. Kama kuna sifa kubwa kuliko zote ya Lukuvi kama mwanasiasa, basi sifa hiyo ni uwezo wake wa kuwa kama maji - yakiwa ndani ya kikombe yatachukua mfano wa kikombe na yatachukua sura nyingine yoyote kulingana na mazingira na chombo ama kifaa yalimo.
Kabudi alikuwa miongoni mwa mawaziri waliokuwa wakionekana kama watetezi wakuu wa utawala wa Magufuli - wakati fulani akiwaambia wakosoaji wa mtangulizi huyo wa Rais Samia kwamba kama wanashindwa kumsifia bosi wake huyo, basi angalau wakae kimya badala ya kumkosoa. Msimamo huo ulikuwa tofauti na ule wa Kabudi msomi uliokuwa ukifahamika nyuma. Kama ilivyo kwa Lukuvi, ilionekana pia kwamba Kabudi alikuwa na uwezo wa kuwa kama maji - kubadilika kutokana na mazingira aliyomo.

Chanzo cha picha, Wizara ya ardhi
Kwa mujibu wa maelezo ya Rais, wawili hao sasa wamepewa majukumu ambayo hayakuwa yakijulikana kufanywa na yeyote kwenye baraza lililopita. Kwa mujibu wa Samia, kulikuwa na tatizo la uratibu miongoni mwa mawaziri na naibu mawaziri na Lukuvi sasa atafanya kazi ya kuratibu utendaji wa mawaziri. Kabudi yeye atakuwa akimsaidia Rais na nchi kwa ujumla katika masuala ya mikataba akiongoza majadiliano ya serikali na taasisi mablimbali.
Hata hivyo, nafasi hizo zina utata wake. Kwa kawaida, Ofisi ya Waziri Mkuu ndiyo ilikuwa ikifanya shughuli za uratibu na kwa vile Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, bado yupo kazini, haijulikani ni yapi hasa yatakuwa majukumu ya Lukuvi na yapi yatakuwa ya Majaliwa.
Kihalisia pia, kwa ujumla Lukuvi ni mwandamizi na mzoefu zaidi wa shughuli za serikali tangu akiwa Mkuu wa mkoa wakati wa uongozi wa Rais Benjamin Mkapa baadaye kushika uwaziri, huku Majaliwa akishika nafasi ya Ukuu wa Wilaya na baadaye Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI-Elimu) wakati wa kipindi cha pili cha Rais Jakaya Kikwete kuanzia 2010 kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu mwaka 2015 hadi sasa.
Hali hii inaweza kuonekana kwa namna fulani kuwa Majaliwa kawekwa kwenye mtego kiutendaji hasa ikizingatiwa hakuna mstari bayana wa kutenganisha wigo wake na ule wa Lukuvi wa kuratibu shghuli za serikali.
Majukumu ya Kabudi pia yana utata kwa sababu kisheria na kikatiba, mshauri mkuu wa serikali kwenye masuala ya sheria ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali na hakuna uhakika hasa ni mashauri yapi yataishia kwa Kabudi na yapi yatakwenda kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Katiba ya Tanzania inasemaje?
Katiba ya Tanzania iko wazi katika maeneo kadhaa kuhusu hatua hii ya Rais Samia. Kwanza, Katiba inazungumza kwamba Rais ana wajibu wa kuwapa watu majukumu mbalimbali ya kiserikali kwa mujibu wa wadhifa wake. Ibara ya 36 inasema yafuatayo; (1) …Rais atakuwa na mamlaka ya kuanzisha na kufuta nafasi za madaraka ya namna mbalimbali katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano." (2) ..Atakuwa na madaraka ya kuteua watu wa kushika nafasi za madaraka ya viongozi wanaowajibika kuweka sera za idara na taasisi za Serikali…"
Kwa sababu hiyo, kama Mkuu wa Serikali, Rais ana uwezo wa kuteua, kupangua na pia kugawa majukumu mbalimbali kwa watu anaoona wanafaa kwa ajili ya maslahi ya nchi. Kama ameona anaweza kusaidiwa na wawili hao katika majukumu yake ya urais, anaruhusiwa kuwateua.
Kwenye nafasi ya Waziri Mkuu, Katiba inasema yafuatayo kuhusu shughuli zake kupitia ibara ya 52; (1) Waziri Mkuu atakuwa na madaraka juu ya udhibiti, usimamiaji, utekelezaji wa siku hata siku wa kazi na shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Waziri mpya katika serikali ya Rais Samia, Pindi Chana, ndiye atakayekuwa akipewa majukumu ya Bunge, Sera na Uratibu ambayo kwa kawaida ndiyo yamekuwa majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Swali kubwa la kujiuliza hapa ni kwamba je- ni majukumu yapi yataratibiwa na Majaliwa kwa mujibu wa maelekezo ya Katiba na yapi yataratibiwa na Lukuvi kwa mujibu wa maelekezo ya mamlaka ya uteuzi?.
Jambo kubwa katika majukumu haya mapya ya mawaziri hawa wa zamani ni kwamba hakuna sheria wala utaratibu uliovunjwa lakini ni jambo la kusubiri na kuona ni kwa vipi watatekeleza majukumu yao pasipo 'kukanyagana miguu' na wenzao ambao kisheria na kikatiba wanatakiwa kutimiza majukumu waliyopewa.

Chanzo cha picha, Ikulu Tanzania
Rais Samia na kete ya mamlaka ya uteuzi
Uamuzi wa kumwondoa Lukuvi na kumwingiza Pindi Chana umefanya vitu viwili kwa Rais Samia; kwanza umehakikisha mkoa wa Iringa umeendelea kuwa na waziri kwa vile wote wanatoka mkoa mmoja lakini pili umeongeza idadi ya mawaziri wanawake. Lakini kauli ya Rais wakati akifafanua majukumu mapya ya mawaziri hao waandamizi -akiwaita kaka zake, yanaonesha kwamba Samia alikuwa anataka pia kupunguza mawaziri wenye umri mkubwa.
Kuna hoja kwamba Waziri wa Kazi Maalum- Ikulu, George Mkuchika ana umri mkubwa (miaka 73) kuliko wawili hao; Kabudi na Lukuvi, lakini walau ofisi yake (Mkuchika) mara nyingi imekuwa ikishikwa na wanasiasa wenye umri mkubwa; kuanzia zama za akina Kingunge Ngombale Mwiru, Brigedia Moses Nnauye, na Mark Mwandosya. Huku Stephen Wassira wakati mmoja akihusika na Uratibu na Uhusiano wa Umma.
Na kwa sababu Kabudi na Lukuvi wanawakilisha makundi tofauti ndani ya CCM, majukumu haya mapya ni aina ya ujumbe kwamba wote wawili bado ni sehemu ya chama tawala na serikali. Na kama kuna jambo lolote ambalo lina utata kwa wawili hao, maana yake ni kwamba bado watakuwa chini ya mbawa za Rais, hivyo hawatakuwa mbali na macho ya wanaomlinda urais.
Namna ambavyo jambo hili - la kuwatema kwenye baraza la mawaziri ambachi ni chombo rasmi na mahsusi kikatiba cha kumshauri rais juu ya shughuli za uendeshaji wa serikali na kuwapa majukumu mapya mawaziri wake hao wa zamani, limefanyika-ni ushahidi mwingine kwamba Rais Samia ni mwanasiasa mpevu na anayejua kuchanga karata zake za kisiasa. Ni kana kwamba kaweka karata zake chache mezani na kusubiri wengine wacheze huku zile turufu akibaki nazo mkononi jirani na kifuani na kungoja kuzicheza wakati ufaao.
Je mbinu hii ni kwa kiasi gani itabakia kuiweka hali ya kisiasa na kiuongozi wa serikali Tanzania katika mstari mnyoofu, hakika ni suala la kungojea tu.













