Wagonjwa wa kike wana uwezekano wa kufa wanapofanyiwa upasuaji na wapasuaji wa kiume, Kwa nini?

Iliyochapishwa

Jaribu kuwaza akilini mwako daktari wa upasuaji, akiwa amevaa na yuko tayari kukufanyia upasuaji.

Je, unawaza daktari mwanamume au mwanamke?

Ikiwa wewe ni mwanamke, unapaswa kuzingatia kumchagua daktari wako wa upasuaji kwa sababu yaweza kuokoa maisha yako.

Hiyo ni kwa sababu wanawake wana uwezekano wa asilimia 3 zaidi wa kufa wanapofanyiwa upasuaji na madaktari wapasuaji wa kiume ikilinganishwa na wapasuaji wa kike, kulingana na utafiti wa hivi majuzi.

Ingawa jinsia ya daktari wa upasuaji ilikuwa na tofauti kidogo sana kwa wagonjwa wa kiume, utafiti huo pia uligundua kuwa wanawake walikuwa na uwezekano mkubwa wa kupata matatizo ikiwa daktari wao alikuwa mwanamume. Lakini ni kwa nini?

Mwanamume aliyeongoza utafiti huo (uliochapishwa katika jarida la matibabu la JAMA Surgery), Dk Christopher Wallis, hana uhakika.

Aliiambia BBC kuwa bado hawana maelezo ya matokeo haya, lakini wanafanyia utafiti.

Kwa hiyo tuliwauliza madaktari wa upasuaji mbalimbali wa kike maoni yao kuhusu kwa nini mwanamke anaweza kuwa salama zaidi mikononi mwao.

Mtazamo wa maumivu

Utafiti huo uliangazia zaidi ya wagonjwa milioni 1.3 waliotibiwa na madaktari wa upasuaji 2,937 huko Ontario, Canada, kutoka mwaka 2007 hadi 2019.

Unadaiwa kuwa "utafiti wa kwanza kushughulikia swali la uhusiano kati ya jinsia ya daktari na mgonjwa na matokeo ya upasuaji".

Pendekezo moja katika utafiti ambalo linaweza kuelezea matokeo ni kwamba kuna tofauti kubwa katika mtazamo wa maumivu na madaktari wa kiume na athari na dalili uchungu kwa wagonjwa wa kike".

Daktari Oneeka Williams, kutoka chuo cha Tufts huko Boston, Marekani, anakubali.

"Nadhani kuna upendeleo wa kiume wa kupuuza malalamiko ya wanawake. Wanafikiri kwamba wanawake wana wasiwasi zaidi na kwa hivyo hawazingatii malalamiko. Malalamiko yanatupiliwa mbali, maumivu hupunguzwa, na ukali wa ugonjwa mara nyingi hupuzwa," aliambia BBC.

Dk Jennifer Svahn, daktari wa upasuaji wa mishipa katika Chuo Kikuu cha Afya cha Northwell huko New York, anakubaliana.

Anafikiri kiwango cha juu cha vifo kinaweza kuwa "kwa sababu madaktari wa upasuaji wa kiume wana uwezekano mkubwa wa kubatilisha au kuweka pembeni wasiwasi na dalili za mgonjwa wa kike".

Mitazamo

Dk Nancy Baxter, daktari wa upasuaji wa utumbo katika Hospitali ya Chuo cha St Michael cha Toronto, pia anaamini kwamba "watu huwa wanapuuza maumivu kwa wanawake zaidi kuliko kwa wanaume," lakini anaongeza kwamba mambo mengine yanaweza pia kuchangia

"Unapomuona mgonjwa unafanya maamuzi ya aina gani wewe kama daktari wa upasuaji? Unampeleka nani kwenye chumba cha upasuaji? Kuna uwezekano kuwa kuna tofauti kati ya madaktari wa upasuaji kwa jinsia zao na jinsi wanavyowahudumia wagonjwa wa kike na kiume. ," aliiambia BBC.

Alinukuu utafiti kwa wagonjwa wenye malalamiko ya moyo unaoonyesha kwamba madaktari wa moyo wa kike uhudumia wagonjwa wa kike vizuri zaidi kuliko vile madaktari wa moyo wa kiume wanavyofanya, na hivyo kusababisha matokeo bora.

Lakini pia anaonyesha tofauti za mitazamo kwa wapasuaji wa kiume na wa kike.

"Wakati wa upasuaji, tunajua kuwa madaktari wa upasuaji wanawake wanaadhibiwa kwa matokeo mabaya, ikiwa wana matokeo mabaya. Wana uwezekano mkubwa wa kupungua kwa rufaa zao, wana uwezekano mdogo wa kusamehewa kwa matokeo mabaya.

"Na matokeo mabaya yanahusishwa na ujuzi wao, ambapo kwa madaktari wa upasuaji wa kiume, matokeo mabaya yanahusishwa na bahati mbaya.

"Kwa hivyo madaktari wa upasuaji wanawake uhitajika kufanya vizuri zaidi ili wachukuliwe kuwa sawa."

'Naonekana kama daktari wa upasuaji'

Ubaguzi wa kijinsia katika taaluma inayotawaliwa na wanaume umetambuliwa kwa muda mrefu na unaweza kuwa sababu ya wanawake kuacha taaluma hiyo.

Mwaka 2015, madaktari wa upasuaji wa kike walienda kwenye Twitter kupinga hili kwa kuanzisha "#ILookLikeaSurgeon". Bado leo, kuna ujumbe mwingi kuhusu jinsi wanawake katika taaluma hiyo wanachukuliwa kuwa katika taaluma tofauti, chochote isipokuwa daktari wa upasuaji.

Dk Williams anasema madaktari wa upasuaji wa kike hukumbushwa kila mara kuhusu jinsia zao.

"Wagonjwa wengi na wafanyikazi wanadhani naweza kuwa yeyote isipokuwa daktari wa upasuaji," anasema. "Mawazo ya mara kwa mara ni kwamba mimi ndiye msaidizi wa matibabu, mtaalamu wa lishe na ikiwa nina bahati, muuguzi.

Ukosefu wa usawa wa kijinsia

Wakati mwandishi mkuu Daktari Wallis anasisitiza kwamba utafiti wa Ontario unaonyesha mwelekeo wa watu, na haimaanishi kuwa mgonjwa wa kike atafanya vibaya zaidi na daktari wa upasuaji wa kiume, utafiti pia unaonyesha ukweli kamili wa upasuaji - katika zaidi ya upasuaji milioni 1.3, mgonjwa mwanamke alichukua zaidi ya 57% ya wakati huo, lakini daktari wa upasuaji akachukua chini ya 11% ya matukio.

Ukosefu huu wa madaktari wa upasuaji wa kike ni jambo ambalo Dk Svahn analaumu.

"Matibabu ya mgonjwa yeyote na daktari wa upasuaji haipaswi kupunguzwa kwamba hakuna wanawake wa kutosha katika taaluma hiyo," anasema.

Fiona Myint, makamu wa rais wa Chuo cha Royal cha Madaktari wa Upasuaji cha Uingereza, anatambua hitaji la kuboresha usawa wa kijinsia katika upasuaji.

"Nchini Uingereza, wanaume wengi zaidi kuliko wanawake wanachagua kuanza mafunzo kama madaktari wa upasuaji. Wanawake ni asilimia 41 ya madaktari wa upasuaji wa awamu ya kwanza na ni asilimia 30 tu ya wanafunzi wa mafunzo ya juu na asilimia 14 ya washauri," anasema.

Wale wanawake ambao hubakia wanaweza kukutana na ubaguzi wa kijinsia mahali pa kazi - Dk Williams anasema ni karibu kitu cha kila siku kwake.

Siku moja usiku anakumbuka aliitwa kwenye chumba cha dharura ili kuona mgonjwa wa kiume. Ili kumstarehesha mgonjwa, muuguzi mwanamume alimtania mgonjwa akimshauri 'ajizuia asije akamtamani'.

"Alinipunguza kuwa kitu akamshauri mgonjwa huyo asinione kama daktari wa upasuaji, lakini kama mwanamke ambaye anaweza kutomheshimu na ambaye anageweza kukiuka mipaka yake."

Kushinda ubaguzi wa kijinsia na upendeleo wa kijinsia itakuwa muhimu katika kupata wanawake zaidi katika taaluma, na kuwashawishi kubaki.

Lakini kwa sasa, inaonekana Dk Baxter yuko sahihi anaposema kuwa "watu wanapofikiria madaktari wa upasuaji, wanawafikiria wanaume."