Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je Tanzania kutegua kitendawili cha Tume Huru ya Uchaguzi?
- Author, Markus Mpangala
- Nafasi, Mchambuzi, Tanzania
- Iliyochapishwa
Mvutano mkali unaendelea kutamalaki miongoni mwa watu binafsi, wanaharakati, wanasiasa, vyama vya siasa na viongozi wa chama tawala na vyama vya upinzani na serikali kuhusu uwezekano wa kupatikana Tume Huru ya Uchaguzi .
Ikiwa na au bila katiba mpya hali ambayo imeibua kitendawili kigumu ambacho kinatakiwa kuteguliwa ndani ya Taifa hilo, huku wataalamu tofauti wakibainisha kuwa Katiba mpya ndilo jawabu la mambo mengi yanayolalamikiwa.
Madai ya Tume Huru ya Uchaguzi yanasukumwa na hoja kwamba uwanja wa shughuli za siasa hauna usawa, bali unaweka mazingira ya kukipa faida zaidi chama tawala, huku kukiwa na madai ya mara kwa mara ya ukiukwaji wa sheria, ukosefu wa uhuru na kuwepo kwa mamlaka makubwa ya Rais juu ya Tume hiyo.
Uhuru wa Tume na viongozi wake ni miongoni mwa mambo yanayochukua mkondo na kukoleza ajenda ya madai ya Katiba mpya, licha ya Rais Samia Suluhu Hassan mnamo Juni mwaka 2021 kubainisha kuwa mpango wake ni kujikita katika masuala ya uchumi na kuweka kando katiba kwa sasa.
Kumekuwa na malalamiko kutoka vyama na wadau wa siasa kuhusu michakato ya uchaguzi mkuu, ikiwemo ukosefu wa uhuru wa Tume, jambo ambalo linaungwa mkono na viongozi wastaafu walioshiriki Kongamano la viongozi na wadau wa siasa lilioitishwa na Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa jijini Dodoma mnamo Deseamba 15 hadi 17 mwaka 2021 ambao uliibuka na azimio la kuunda kikosi kazi cha watu 23 cha kushughulikia hoja mbalimbali za demokrasia zilizojadiliwa mkutanoni, ikiwemo kuundwa Tume huru ya Uchaguzi.
Kikosi kazi hicho kinaundwa Mwenyekiti Profesa Rwekeza Mukandala na wajumbe ni Zitto Kabwe, Hamad Rashid Mohamed, Siyst L Nyahoza, Profesa Bernadetta Kilian, Profesa Alexander Makulilo, Amina Salum Ali, Haji Omari Heri, Juma Ali Khatib na Christina Mndeme.
Ni hadidu rejea zake ndizo zinakoleza hoja ya Tume Huru na Katiba Mpya kwa sababu uundwaji wake unapingwa na kuaminika kuwa si suluhisho la kudumu katika uwanja wa demokrasia nchini humo.
Aidha, kitendawili kigumu kinapatikana kwenye muundo wa Tume Huru; itaundwaje, viongozi watapatikanaje, kwa katiba hii au ije mpya, mamlaka ya uteuzi yatakuwa kwa nani,uendeshaji na vigezo vinavyohitajika kwa wajumbe vitakuja vipya au kubaki vilevie, ni maeneo ambayo yamegusiwa katika mijadala hiyo.
Je nani wanaongoza Tume ya Uchaguzi?
Mnamo Desemba 27, mwaka 2021 Rais Samia alitangaza kumteua Jaji Jacob Casthom Mwambegele kuwa Mwenyekiti mpya wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi akichukua nafasi ya Jaji Mstaafu Semistocles Kaijage ambaye amemaliza muda wake wa uongozi.
Kwa mujibu wa Katiba ya nchi hiyo Ibara ya 74(1) pamoja na vipengele vyake inafafanua vigezo vya watu wanaotakiwa kuwa vongozi wa Tume ya uchaguzi na kuwataja kuwa;
Mwenyekiti anatakiwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufani au mtu mwenye sifa ya kuwa wakili kwa kipindi kisichopungua miaka 15
Makamu Mwenyekiti anatakiwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Mahakama ya Rufani au ni mtu mwenye sifa ya kuwa wakili kwa muda usiopungua miaka 15.
Wajumbe wa Tume ya Uchaguzi ambao hudumu kwa miaka mitano
Mkurugenzi wa Uchaguzi ndiye Mtendaji mkuu wa shughuli za Tume
Kimsingi viongozi wote hao wanateuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge. Swali pekee lililosalia ni je ikiwa kutakuwa na mabadiliko, ni nani atabeba majukumu ya kuwateua au watapatikana vipi katika mazingira ya sasa.
Ni yapi majukumu ya Tume ya Uchaguzi?
Tume ya Uchaguzi ni kioo cha mwenendo wa demokrasia ndani ya Taifa lolote. Ni mwakilishi wa uhuru wa taasisi ndani ya taifa. Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania Ibara ya 74(6), Tume ya Uchaguzi ina majukumu yafuatayo;-
Kusimamia na kuratibu uandikishaji wa wapigakura katika uchaguzi wa Rais na Wabunge
Kusimamia na kuratibu uendeshaji wa uchaguzi wa Rais na Wabunge
Kuchunguza mipaka na kuigawa Jamhuri ya Muungano katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya uchaguzi wa wabunge
Kusimamia na kuratibu uandikishaji wa wapigakura na uendeshaji wa uchaguzi wa madiwani
Kutekeleza majukumu mengine yoyote kwa mujibu wa Sheria iliyotungwa na Bunge.
Je Tume huru,Katiba mpya bila Bunge huru?
Bunge la Tanzania la sasa ni matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, ambalo kwa 99% linaundwa na wabunge wa chama tawala CCM. Hilo lina maana CCM wanaweza kuamua jambo lolote ikiwemo marekebisho ya Katiba kutengeneza kitu kiitwacho Tume Huru, ikajadiliwa na kupitishwa na Bunge ikiwa limekidhi vigezo vyote. Kufika hapo hakutakuwa na hoja kwamba vigezo havikukidhi hadi sheria kutungwa ama ajenda.
Kimuundo Tume ya Uchaguzi ni zao la Katiba kulingana na sheria iliyotungwa na Bunge. Kwa uwiano wa sasa Bunge halishawishi kuamini kuwa linaweza kusaidia upatikanaji wa Tume huru kupitia marekebisho ya Katiba. Ni kitendawili kigumu mpaka sasa.
Ni sababu kama hizo ndizo zinaleta kitendawili kuwa kuwa Bunge la sasa linalohodhiwa na chama tawala ni mbunge gani atakwenda kinyume na chama chake? Vilevile je, rais akiondolewa madaraka ya kuteua viongozi wa Tume, watapatikanaje? Na je wabunge wa CCM watakubali mwenyekiti wao ambaye pia ni rais aondolewe madaraka ya kudhibiti Tume ya Uchaguzi kiufundi?
Hayo ni baadhi ya maswali ambayo yanazidi kuchochea mjadala huku wataalamu wakitoa mapendekezo na kusisitiza upatikanaji wa Tume Huru huambatana na gharama kubwa hadi kukamilisha kwake. Wanasisitiza kwamba inatakiwa kutanguliza Katiba mpya kwa sababu mengine yote yakifanyika kabla hayatakuwa na tija.
Kumbukumbu zinaonesha Tanzania ilianza mchakato wa Katiba mpya mwaka 2011 na zoezi hilo lilisitishwa mwaka 2014 kwa kupatikana Katiba inayopendekezwa, huku wawakilishi wa vyama vya upinzani wakiwa wamesusia vikao vya Bunge la Katiba wakati huo na kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi maarufu kama UKAWA uliokuja kuleta ushindani mkubwa kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Je mgawanyiko wa upinzani una maana gani?
Kwanza, vyama vya siasa vyote vipo kutetea maslahi, hivyo kila kimoja kinataka kuonekana kinara wa harakati na kujipatia umaarufu machoni mwa wananchi. Vyama vya NCCR-Mageuzi na Chadema vimeibuka kupinga hoja zilizowasilishwa na Mwenyekiti wa Baraza la Demokrasia na Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe.
Vyama hivyo haviamini katika kuomba mazungumzo na chama tawala, bali watuhumiwa wa kesi za kisiasa wote waachiwe huru pamoja na kurejeshwa shughuli za kisiasa ikiwemo mikutano ya hadhara.
Pili, vyama vya upinzani vinakubaliana na ajenda za Tume huru na Katiba mpya, tofauti zao zinaibuka kwenye namna ya kupatikana kwake. Mathalani viongozi na wafuasi wa vyama vya NCCR-Mageuzi na Chadema wanaamini njia pekee ni kuhakikisha Katiba mpya inapatikana ambayo ndani mwake kutakuwa na marekebisho yote muhimu yanayohusu uhuru, muundo na mamlaka ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
"Mabadiliko ni hatua, Taifa hili linao uwezo huo. Hii Tume huru haliwezi kusaidia ikiwa Katiba ni ileile. Katiba ni ileile kwa maana Mwenyekiti na Makamu wake wanateuliwa na rais kwa mamlaka aliyopewa. Pia Mkurugenzi ni mteule wa rais.
Hata kama rais akiondolewa madaraka ya kuwateua viongozi wakuu wa Tume, bado itakuwa chini yake kwa njia mbalimbali sababu Katiba itakuwa ileile, na tutakuwa tumeingia kwenye njia ileile kama ya kuruhusu siasa za vyama vingi chini ya Katiba yenye msingi wa chama kimoja, ikabidi viraka vishonwe kusitiri demokrasia.
Katiba ndicho kitu muhimu. Kwa hiyo iwe ajenda ya umma," amesema kiongozi mmoja mwandamizi toka chama cha upinzani.
Tatu, mgawanyiko unakisaidia chama tawala, kwa sababu vyama vya upinzani vimekosa umoja katika ajenda hii. Wakati Zitto Kabwe ni mjumbe kwenye kikosi kilichoundwa na Msajili wa vyama vya siasa, Jaji Francis Mutungi, viongozi wenzake wa kisiasa hawaafiki na kila kukicha wanakikosoa kkkosi kazi hicho.
Katika mazingira hayo kukosekana umoja ni fursa kwa chama tawala kupunguza shinikizo la kisasa katika ajenda husika na kuendelea kuvuta muda zaidi, huku Katiba mpya ikiwekwa kando.
Je ni upi mustakabali wa Tume na Katiba?
Richard Ngaya, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine ambaye pia ni mchambuzi wa masuala ya siasa amemwambia mwandishi wa makala hii kuwa muundo wa Tume ulivyoainishwa kwenye katiba ya sasa unazingatia marekebisho ya baada ya mwaka 1992 yaliyorejesha mfumo wa siasa za vyama vingi.
Kwa hiyo, marekebisho yanaweza kuingizwa kwenye Katiba ya sasa kama kiraka na kuwezesha uwepo wa Tume huru kama ilivyotokea kwa vyama vingi ambapo nchi haikulazimika kuandika upya katiba nzima.
"Madai ya Katiba mpya yanaweza kuendelezwa pia. Nadhani kwa kutumia mtandao mpana walionao vyama vya upinzani na hasa Chadema endapo watasimama kidete kupigania Katiba mpya na kusema bila hilo 'hakitaeleweka', huenda ikaingia gharama ambayo huenda haikuwahi kufikiriwa lakini inayoweza kuleta matunda makubwa kwa taifa.
Aliongeza: "Tukizingatia mazingira ya sasa, hoja kwa hoja iliyopo mezani, kinachoweza kufanyika ni kuingia gharama ya kuingiza watu wapatao 150 kutokea vyama vya upinzani na kisha wengine 100 kutokea taasisi au makundi mbalimbali nje ya siasa kisha waungane na wabunge bungeni kufanya marekebisho ya Katiba yanayoruhusu Tume Huru ya uchaguzi kisha ndio ilete Bunge lenye uwakilishi wa wananchi kwenye uchaguzi wa mwaka 2025, pamoja na wajumbe wengine litaweza kujadili mambo ya Katiba mpya kati ya 2025-2030".
Baada ya michakato ya awali kupata maoni ya wananchi nchi nzima kufanyika kama ilivyokuwa mwaka 2013-2014. Hilo linawezekana lakini litagharimu rasilimali fedha ambayo sidhani kama zaweza kuwa nyingi sababu kikao chaweza kuwa cha muda mfupi lakini kinachokidhi mahitaji.
Pili, itategemea utashi wa Rais wa nchi, Samia Suluhu Hassan katika kuonesha anafikiria nchi yake kwa miaka 100 ijayo. Tofauti za njia hazizuii kupatikana Katiba mpya wala Tume.