Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mvutano wa Ukraine: Putin amwambia Biden vikwazo vipya vinaweza kuvunja uhusiano
Rais wa Urusi Vladimir Putin amemuonya mwenzake wa Marekani Joe Biden kwamba kuiwekea vikwazo kuhusu Ukraine kunaweza kusababisha kuvunjika kabisa kwa mahusiano.
Katika simu siku ya Alhamisi, rais wa Urusi alisema vikwazo kama hivyo vitakuwa "kosa kubwa".
Wakati huo huo, Bw Biden alimwambia Putin kwamba Marekani na washirika wake watajibu kwa dhati uvamizi wowote wa Ukraine.
Simu hiyo, iliyoombwa na Urusi, ilikuwa mazungumzo ya pili kati ya wawili hao mwezi huu na ilidumu kwa karibu saa moja.
Ilikuwa ni juhudi za hivi punde za kutuliza mvutano kuhusu mpaka wa mashariki mwa Ukraine na Urusi, ambapo maafisa wa Ukraine wanasema zaidi ya wanajeshi 100,000 wa Urusi wametumwa.
Kuwepo kwa wanajeshi hao kumezua wasiwasi katika nchi za Magharibi, huku Marekani ikimtishia Bw Putin kwa vikwazo "kama ambavyo hajawahi kuviona" ikiwa Ukraine itashambuliwa.
Urusi, hata hivyo, inakanusha kuwa inapanga kuivamia nchi hiyo na kusema kuwa wanajeshi wapo kwa ajili ya mazoezi. Inasema ina haki ya kuhamisha wanajeshi wake kwa uhuru kwenye ardhi yake.
Ingawa pande hizo mbili zilipeana onyo wakati wa simu hiyo, mshauri wa sera za kigeni wa Urusi Yuri Ushakov aliwaambia waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuwa Bw Putin "amefurahishwa" na mazungumzo hayo. Aliongeza kuwa imeunda "hali nzuri" kwa mazungumzo yajayo.
Afisa mkuu wa Marekani, ambaye alizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, alisema sauti kwenye simu hiyo zilikuwa "nzito."
"Rais Biden alisisitiza kwamba maendeleo makubwa katika mazungumzo haya yanaweza kutokea tu katika mazingira ya kupunguzwa kwa mvutano na taharuki," Katibu wa Vyombo vya Habari wa Ikulu ya White House Jen Psaki alisema.
"Aliweka wazi kuwa Marekani na washirika wake watajibu vikali ikiwa Urusi itaivamia Ukraine," aliongeza.
Maafisa wa Marekani na Urusi wanatazamiwa kukutana kwa mazungumzo ya ana kwa ana mjini Geneva mwezi ujao, na Ikulu ya White House ilisema Bw Biden alimtaka mwenzake wa Urusi kutafuta suluhu ya kidiplomasia.
Katika ujumbe wa likizo kabla ya simu ya Alhamisi, Bw Putin alimwambia Bw Biden "anasadiki" wawili hao wanaweza kufanya kazi pamoja kwa kuzingatia "kuheshimiana na kuzingatia masilahi ya kitaifa ya kila mmoja".
Msemaji wake, Dmitry Peskov, alisema Moscow ilikuwa "katika hali ya mazungumzo".
"Tunaamini kwamba ni kwa mazungumzo pekee ndipo tunaweza kutatua matatizo yote ya mara moja ambayo tunayo kwa wingi kati yetu," Bw Peskov aliongeza.
Wasiwasi mkubwa huko Washington
Maafisa wa Ikulu ya White House wanasikika wakiwa watulivu wanapozungumza kuhusu Ukraine, angalau wakati wakizungumza nje ya West Wing.
Simu kati ya Rais Biden na Rais Putin siku ya Alhamisi, kama afisa mkuu wa utawala alivyowaambia waandishi wa habari mapema jioni, ilikuwa "mazungumzo mazito, makubwa".
Afisa huyo alizungumza kwa sauti iliyopimwa kuhusu mazungumzo hayo, na akasikika mwenye hasira alipozungumza kuhusu tishio kutoka kwa Urusi. Nyuma ya pazia, hata hivyo, yeye na wengine katika Ikulu ya White House wana wasiwasi mkubwa juu ya uwezekano wa uvamizi wa Ukraine.
Ishara kutoka Urusi ni "za kutisha", kama mtu mmoja wa ndani alivyoniambia, na kwa hivyo kasi ya kidiplomasia imeongezwa.
Siku ya Alhamisi, angalau, viongozi hao wawili walikuwa wakizungumza na wale wa White House wanaona hii kama ishara nzuri. Kwa sasa. wanajaribu kufanya kila wawezalo ili kuhakikisha wanaendelea kuzungumza hadi mwaka mpya.
Waziri wa ulinzi wa Ukraine aliliambia bunge mwanzoni mwa Disemba kwamba Urusi ilikuwa imekusanya makumi ya maelfu ya wanajeshi karibu na mpaka, na inaweza kuwa inajiandaa kwa mashambulizi makubwa ya kijeshi mwishoni mwa Januari.
Urusi imesema kuwa kuhamishwa kwa majeshi kwenye mpaka ni hatua ya ulinzi dhidi ya Nato, muungano wa kijeshi wa Magharibi. Inataka uhakikisho wa kisheria kwamba Nato haitapanua zaidi kuelekea mashariki, na kwamba silaha fulani hazitatumwa Ukraine au nchi yoyote jirani.
Marekani imekataa kile inachokiita kama nia ya Kremlin kudhibiti mustakabali wa nchi huru.
Ukraine haijapewa uanachama wa Nato, lakini ina uhusiano wa karibu na umoja huo.
Mvutano kati ya Urusi na Ukraine sio jambo geni. Mnamo mwaka wa 2014, Urusi iliteka Rasi ya Crimea ya Ukraine na baadaye kuanza kuunga mkono waasi wanaotaka kujitenga mashariki mwa Ukraine ambao wamesababisha takriban watu 14,000 kuuawa katika mapigano ya mara kwa mara.
Washington na washirika wake wa Ulaya wameionya Urusi kutarajia vikwazo vikali vya kiuchumi ikiwa wanajeshi watavuka tena kuingia Ukraine.