Majeshi ya Uganda, DRC yanasema kambi za ADF ziliharibiwa

Iliyochapishwa

Vikosi vya jeshi la Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo vimesema kuwa kambi nne za waasi wa Allied Democratic Forces ziliharibiwa wakati wa mashambulizi ya angani yaliyotekelezwa tarehe 30 Novemba.

Taarifa kutoka kwa vikosi vya serikali zote mbili zinasema kuwa wanamgambo 34 wa ADF walikamatwa na raia 31 wa Congo ambao walikuwa wakishikiliwa mateka wameachiliwa.

Majeshi hayo mawili sasa yameanza kufungua barabara katika maeneo ya karibu na Beni, ambako waasi wanaaminika kuishi.

Oparesheni za ardhini zilisitishwa takriban wiki moja iliyopita, kutokana na barabara zisizopitika.

Jeshi la Uganda liliingia Mashariki mwa Kongo kwa mwaliko wa serikali ya DRC, kuwatimua waasi wa kundi la ADF, walio na ufungamano na Islamic State kufuatia mfululizo wa mashambulizi ya mabomu ndani na karibu na Kampala katika wiki zilizopita.

Uganda inalaumu mashambulio hayo yalitekelezwa na wanamgambo wa ADF, ambao polisi walisema walikuwa wamepangisha vyumba vya kulala na kuanza wakisajili wafuasi wao ndani ya nchi.

Kundi la Islamic State lilidai kuhusika na mashambulizi matatu, yakiwemo milipuko miwili ya mabomu katikati mwa jiji la Kampala mnamo Novemba 16.

Kundi la ADF, ambalo liliundwa awali nchini Uganda, limekuwa likihudumu Mashariki mwa DRC kwa zaidi ya miaka ishirini.

Serikali ya Congo imesema kuwa imealika wanajeshi wa majirani zake nchini humo kwani ADF ni mojawapo ya makundi mengi yenye silaha yanayofanya uharibifu mashariki mwa DR Congo.

Kundi la ADF, lililofurushwa kutoka Uganda mwanzoni mwa miaka ya 2000, limekuwa likishambulia na kupora vijiji vya Congo, na kuua watu na kuwasajili watoto kwa nguvu kwa takribani muongo mmoja uliopita.

Je, hatua ya majeshi ya Uganda kuingia DRC imepokelewaje?

Wanasiasa wa upinzani na baadhi ya wachambuzi wamepinga vikali uvamizi wa wanajeshi hao katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Hii kwa kiasi fulani ni kwa sababu utumaji wa vikosi ulifanywa bila kushauriana au kupata kibali kutoka kwa bunge, kama katiba inavyotaka.

Lakini Uganda imepuuza hili hapo awali. Hakukuwa na mashauriano wakati wanajeshi walipoingia DR Congo katika miaka ya 1990. Na mwaka 2013, vikosi vya Uganda vilivuka hadi Sudan Kusini kumuunga mkono Rais Salva Kiir bila idhini ya bunge.

Wakati Wacongo wengi wanatamani kuona mwisho wa mashambulizi ya ADF, wengine hawana kumbukumbu nzuri ya uvamizi wa awali wa Uganda.

Kundi la wanaharakati la Lucha pia limeelezea wasiwasi wake, likisema kuwa hiyo haikuwa njia ya kuleta amani katika eneo hilo lenye matatizo.

Likihutubia jeshi la Congo, ilisema katika taarifa yake kwamba "imani… lazima ipatikane. Watu wanahitaji kuwa na serikali na jeshi ambalo wanaweza kuweka imani yao yote."

Msemaji wa Monusco, kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini DR Congo, alisema kuwaalika Waganda ni chaguo halali na Umoja wa Mataifa unahimiza "nchi za kikanda kufanya kazi pamoja kutatua tishio la kuvuka mpaka".

Hapo awali Monusco iliendesha operesheni za pamoja na jeshi la Congo kujaribu kuzuia mashambulizi ya ADF lakini bado yanaendelea.