Kwanini vikosi vya Uganda vimeingia DRC kwa mara nyingine?

    • Author, Patience Atuhaire
    • Nafasi, BBC News, Kampala
  • Iliyochapishwa

Vikosi vya Uganda kwa mara nyingine vimevuka mpaka wa magharibi mwa nchi hiyo na kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Uvamizi wa hapo awali umekuwa na utata mkubwa huku wanajeshi hapo awali wakipambana na wanajeshi kutoka Rwanda, wakifanya ukatili na kupora maliasili za nchi hiyo.

Lakini wakati huu ni kwa idhini ya serikali ya DR Congo.

Kwa nini wanajeshi wa Uganda wako DR Congo?

Akizungumza siku chache baada ya shambulio la kujitoa muhanga mwezi uliopita katikati mwa mji mkuu, Kampala, Rais Yoweri Museveni alitoa wito kwa waliohusika kujisalimisha: "Ushauri wangu kwa wote ... ikiwa hawatatoka nje, watakufa."

Serikali ilikuwa imedhamiria wazi kuwafuatilia wapiganaji hao popote pale walipo.

Katika shambulio la mwisho na kali zaidi la msururu wa mashambulio ya tarehe 16 Novemba, washambuliaji watatu walijilipua na kuwauwa takriban wengine wanne katika harakati hizo.

Serikali ililaumu kundi la waasi la Kiislamu linaloitwa Allied Democratic Forces (ADF), ambalo lilianzishwa nchini Uganda kisha kulazimishwa kuingia DR Congo. Inasema sasa ni sehemu ya kundi la Islamic state.

Siku ya Jumanne, jeshi la Uganda lilithibitisha kuwa lilifanya mashambulizi ya anga katika maeneo ya ADF mpakani. Kisha siku ya Jumatano mamia ya wanajeshi wa Uganda walionekana wakivuka kuelekea DR Congo.

Serikali ya Congo ilisema kuwa imealika wanajeshi wa majirani zake nchini humo kwani ADF ni mojawapo ya makundi mengi yenye silaha yanayofanya uharibifu mashariki mwa DR Congo.

Kundi la ADF, lililofurushwa kutoka Uganda mwanzoni mwa miaka ya 2000, limekuwa likishambulia na kupora vijiji vya Congo, na kuua watu na kuwasajili watoto kwa nguvu kwa takribani muongo mmoja uliopita.

Mapigano ni makubwa kiasi gani?

Mkazi wa mji wa Beni, karibu na mpaka, aliiambia BBC kwamba aliweza kusikia sauti ya milipuko.

"Kuna mapigano makali. Wanajeshi wa Uganda waliingia kwa miguu na magari. Tumeona ndege zisizo na rubani zikiruka."

Kanda za video zimesambaa kwenye mitandao ya kijamii zikionesha wanakijiji walio karibu na Beni wakitazama safu za wanajeshi wa Uganda wakipita.

Lakini maafisa kutoka serikali ya Uganda na Congo hawajatoa maelezo mengi, isipokuwa kuthibitisha uwepo wa wanajeshi wa Uganda.

Jeshi la Uganda limetoa msururu wa picha zinazoonesha safu za wanajeshi nchini DR Congo wakiwa wameandamana na magari ya kivita na vifaru.

Inasema maelfu ya wapiganaji wa ADF waliuawa katika mashambulizi hayo ya anga lakini haijatoa ushahidi wowote na haijawezekana kuthibitisha.

Operesheni hiyo itatathiminiwa kila baada ya miezi miwili, ilisema katika taarifa.

Msemaji wa jeshi la Congo, Jenerali Leon Kasonga, alisema mapigano hayo yanatokea katika maeneo ya mbali, ikiwa ni pamoja na katikati ya msitu na Hifadhi ya Taifa ya Virunga, ambayo inaenea kwenye mpaka wa nchi hizo mbili.

Aliongeza kuwa harakati za kijeshi, muda wa operesheni na takwimu za majeruhi ni siri.

Je, majibu yamekuwaje nchini Uganda?

Wanasiasa wa upinzani na baadhi ya wachambuzi wamepinga vikali uvamizi wa wanajeshi hao katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Hii kwa kiasi fulani ni kwa sababu utumaji wa vikosi ulifanywa bila kushauriana au kupata kibali kutoka kwa bunge, kama katiba inavyotaka.

Lakini Uganda imepuuza hili hapo awali. Hakukuwa na mashauriano wakati wanajeshi walipoingia DR Congo katika miaka ya 1990. Na mwaka 2013, vikosi vya Uganda vilivuka hadi Sudan Kusini kumuunga mkono Rais Salva Kiir bila idhini ya bunge.

Wakati Wacongo wengi wanatamani kuona mwisho wa mashambulizi ya ADF, wengine hawana kumbukumbu nzuri ya uvamizi wa awali wa Uganda.

"Si kwa wachoma moto/wazima moto, makosa yale yale yataleta madhara yale yale. Simameni Wacongo, Taifa liko hatarini!" alitweet mapema wiki hii.

Kundi la wanaharakati la Lucha pia limeelezea wasiwasi wake, likisema kuwa hiyo haikuwa njia ya kuleta amani katika eneo hilo lenye matatizo.

Likihutubia jeshi la Congo, ilisema katika taarifa yake kwamba "imani… lazima ipatikane. Watu wanahitaji kuwa na serikali na jeshi ambalo wanaweza kuweka imani yao yote."

Msemaji wa Monusco, kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini DR Congo, alisema kuwaalika Waganda ni chaguo halali na Umoja wa Mataifa unahimiza "nchi za kikanda kufanya kazi pamoja kutatua tishio la kuvuka mpaka".

Hapo awali Monusco iliendesha operesheni za pamoja na jeshi la Congo kujaribu kuzuia mashambulizi ya ADF lakini bado yanaendelea.

Awali kilitokea nini ?

Jeshi la Uganda lina sifa chafu kwa uvamizi wake nchini DR Congo katika miaka ya 1990 na mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Mwaka 1999 na 2000, wanajeshi wa Uganda na Rwanda, kila moja likiunga mkono kundi tofauti la waasi wa RCD, walipambana katika mji wa Kisangani nchini Congo.

RCD ilikuwa ikipigania kumpindua rais wakati huo, Laurent Kabila.

Katika kile kinachojulikana kama Vita vya Siku Sita, zaidi ya watu 1,000 wanasemekana kuuawa mnamo Juni 2000, wakati majeshi ya Uganda na Rwanda yakipigana kuudhibiti mji huo.

Wanajeshi wa Uganda walishutumiwa kwa ukiukaji wa haki za binadamu wakati wa awamu hii ya mapigano.

Miongoni mwa madai hayo ni kwamba waliwanyanyasa kingono wanawake wa eneo hilo.

Vikosi vya Uganda pia vilishutumiwa kwa kupora maliasili kubwa ya DR Congo.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2001 ilisema vikosi kutoka Uganda, pamoja na majirani wengine, vilipora madini, kahawa, mbao na mifugo.

Mwaka 2005, Mahakama ya Kimataifa ya Haki ilisema Uganda ilipaswa kulipa fidia kwa DR Congo kwa uvamizi huo haramu. Pesa hizo bado hazijakabidhiwa.

Kwa nini mashariki mwa DR Congo ni kimbilio la makundi ya waasi?

Eneo hilo lenye rasilimali nyingi limevutia waasi kwa miongo kadhaa. Baadhi ya ripoti zinaonesha kunaweza kuwa na takribani vikundi 120 tofauti vya wanamgambo vilivyoko huko.

Mapigano yamekuwa kama vile udhibiti wa utajiri wa nchi kama nguvu ya kisiasa. Baadhi ya nchi jirani zimeshutumiwa kuwaunga mkono waasi ili kufaidika na machafuko hayo kupitia uporaji.

Licha ya Rais Felix Tshisekedi kutangaza kile kilichoitwa "hali ya kuzingirwa" - katika majimbo mawili yaliyoathirika, mashambulizi na mauaji ya wakazi yameendelea.