Miaka 60 ya Uhuru :Jina la Nyerere lilivyojengeka na siasa za Tanzania

    • Author, Mohammed AbdulRahman
    • Nafasi, Mchambuzi wa Siasa
  • Iliyochapishwa

Desemba 9, 2021, imetimia miaka 60 tangu Uhuru wa Tanganyika kutoka kwa Uingereza, ambao muasisi wake ni Julius Kambarage Nyerere . Nyerere aliitawala Tanganyika takriban miaka miwili na nusu kabla ya kuungana na visiwa vya Zanzibar Aprili 1994. Kuzaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kulilifuta jina la Tanganyika. Nyerere akawa pia Rais wa Jamhuri hiyo mpya hadi alipon´gatuka (neno alilopenda kulitumia kutokana na lugha ya kabila lake la Wazanaki likimaanisha kuondoka ) madarakani kwa hiyari 1985.

Nyerere alihitimu Chuo kikuu maarufu cha Makerere Uganda na Edinburgh, Scotland nchini Uingereza. Aliporudi nyumbani alisomesha muda wa miaka mitatu, kabla ya kuamua kuingia katika siasa na kupewa jina la "Mwalimu," ambalo mwenyewe alipenda sana kulitumia. Bila ya shaka likimkubusha taaluma yake.

Utawala wake na sera ya Ujamaa

Kipindi cha utawala wake kinaangaliwa kwa mitazamo tafauti ndani ya nchi yake na Kimataifa. Aliwavutia wengi na kukosolewa na wengine. Nyerere aliamua kufuata sera ya Ujamaa kwa kutangaza Azimio la Arusha 1967 ambapo miongoni mwa mambo mengine dola iliwapokonya ardhi waliokuwa na mashamba makubwa ili kuigawa kwa wasio na ardhi katika mfumo wa wanavijiji. Sambamba na hayo ikaanza pia kuwapa wananchi elimu na afya bure.

Nyerere na ujamaa ulikuwa ndiyo utambulisho wao. Ujamaa wa kiliberali uliozingatia mazingira ya kiafrika ya wananchi wa nchi yake. Nikisema ujamaa wa kiliberali ni kwamba ulitafautiana na sera kali za ujamaa kwa mfano katika mataifa ya Kisoshalisti ya Ulaya mashariki.

Hata wasomi waumini wa falsafa ya mrengo wa kushoto nje ya bara hilo walivutiwa na muelekeo wa Tanzania, kama njia ya kujiondoa katika tabia ya kuwa taifa tegemezi. Ujamaa kilikuwa kipimo cha Nyerere katika jukwa la siasa za kimataifa, katika wakati ambapo mataifa mengi barani Afrika yakitegemea misaada ya nchi fadhili zikiongozwa na dola zilizolitawala bara hilo.

Nyerere alisimama kidete katika wakati ambapo dunia iligawika kisiasa kutokana na mivutano ya kifalsafa kati ya Ujamaa na Upepari, matokeo ya vita baridi baina ya kambi ya mashariki na magharibi. Mwisho wa miaka ya 1970, mafanikio ya ujamaa yalianza kuwekewa alama ya kuuliza na kuonekana ujamaa umeshindwa.

Lakini kuna wasiokubaliana na dhana hiyo wakiwemo wasomi. Mchambuzi wa masuala ya kisiasa kutoka Kenya Martin Oloo ni mmoja wao. Anasema, "Licha ya kwamba tunaweza kuwa na tafauti za kimawazo lakini Azimio la Arusha na sera ya Ujamaa vimeleta Umoja na misingi ambayo ingalipo licha ya kwamba Tanzania imebadili mkondo na kufuata kile kinachoitwa utandawazi."

Alipoondoka madarakani 1985, alianza kushuhudia Tanzania ikibadili dira taratibu. Ingawa hakupendekezwa na mabadiliko yaliyotokana na hali mbaya ya uchumi lalisema anaheshimu msimamo wa wanaosema Ujamaa umeshindwa lakini yeye atabakia mjamaa.

Nyerere alizungumza sana juu ya hatari ya viongozi kuwa na madaraka makubwa akisema kunaweza kuwafanya kuwa madikteta. Lakini binafsi hakuyakataa madaraka makubwa na aliyatumia kuwadhibiti na kuwaweka kizuizini wanasiasa waliompinga kwa kutumia kanuni iliyoyapa nguvu mamlaka aliyokuwa nayo yaani Presidential detention order.

Hakuwahi kukiri kwamba binafsi aliitumia kanuni hiyo vibaya ambapo aliwaweka kizuizini waliotafautiana naye wakiwemo walioupinga mfumo wa chama kimoja. Vyama vya kisiasa vilipigwa marufuku miaka minne hivi baada ya Uhuru na kubakia chama kimoja cha Tanganyika African National Union (TANU)

Kwa upande mwingine, jambo ambalo waliokuwa karibu na Nyerere wanasema lilimuumiza kichwa ni hali ya kisiasa Zanzibar wakati wa utawala wa Abedi Karume, aliyeunda naye muungano. Mbali na watu kadhaa kutoweka na kutojulikana waliko, suala kubwa lilikuwa kuwapeleka Zanzibar wakiwemo waliokuwa katika serikali ya mapinduzi na muungano na kupotea. Karume akiamini wakimpinga. Hatua za kimapinduzi visiwani zilimpa mtihani katika sura ya kimataifa.

Nikitafakari nina amini kizingiti kikubwa kilikuwa ni kila upande kuwa na chama tawala tafauti, TANU kwa Tanganyika na Afro Shirazi Party (ASP) Zanzibar, kila chama kikiwa na mamlaka yake. Vyama hivyo viliungana 1977 kuunda Chama cha Mapinduzi (CCM).

Haiba ya Nyerere Kimataifa

Nje ya Tanzania Nyerere alisifiwa na kuheshimika kwa kujitoa kwa hali na mali kusaidia ukombozi wa nchi za Afrika. Mji mkuu wa Tanzania Dar-es-salaam ukawa makao makuu ya Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa nchi huru za Afrika (OAU). Alikuwa mhimili katika kuimarishwa uhusiano kati ya nchi za Kaskazini na Kusini, kwa kushirikiana na wanasiasa maarufu barani Ulaya Willy Brandt na Olaf Palme. Brandt alikuwa Kansela wa Ujerumani na Palme Waziri mkuu wa Sweden.

Pamoja na hayo katika kile baadhi ya wachambuzi wanachokiona kulikuwa ni kuteleza kwa Nyerere ni pale alipochukua msimamo wa kuunga mkono kujitenga jimbo la mashariki mwa Nigeria la Biafra 1967. Alijiingiza katika mgogoro huo na kuitambua Biafra, akijiunga na nchi nyengine tatu za kiafrika, Zambia, Cote d`Ivoire na Gabon.

Hatimaye zote zilisahau yaliyopita na kufikia mapatano kwa upatanishi wa baada vita kumalizika kwa upatanishi wa Mfalme Haile Selassie wa Ethiopia baada ya Nigeria kushinda vita vilivyomalizika 1970. Mfalme huyo aliwakutanisha Nyerere na Kiongozi wa kijeshi wa Nigeria Jenerali Yakubu Gowon wakati wa mkutano wa viongozi wa nchi za Afrika mjini Addis Ababa.

Itakumbukwa walikuwa wanajeshi wa Nigeria waliopelekwa kusimamia usalama baada ya Uingereza kumsaidia Nyerere kwa kuuzima uasi wa wanajeshi wa Tanganyika Januari 1964. Wadadisi hadi leo wanajiuliza ilikuwaje akaunga mkono kujitenga Biafra wakati alipigania kwa nguvu zote Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na hata kabla ya hapo Shirikisho la Afrika Mashariki na Afrika?

Jicho na mtazamo wa majirani

Licha ya ndoto ya Shirikisho hilo la nchi nne Tanganyika, Kenya, Uganda na Zanzibar kushindwa kutimizwa lakini hadi leo jina la Nyerere linaenziwa katika nchini hizo jirani na Tanzania. Kwa mfano nchini, Kenya jina la Mwalimu hutajwa sana kuliko la baba wa uhuru wa Taifa hilo Mzee Jomo Kenyatta.

Mchambuzi Oloo anasema,"Nyerere amekuwa kipenzi cha wengi miongoni mwa Wakenya kwa sababu ya mvuto aliokuwa nao katika kuwaleta pamoja Watanzania kwa kuwa na lugha moja. Aliwapa sababu ya kujivunia kuwa Watanzania Ni kinyume na Kenya ambako wengi wangefikiria Mzee Kenyatta angeweza kuwaongoza kwa msingi huo wa Umoja na lugha badala ya ukabila, lakini haikuwa hivyo. Ukabila ni chanzo cha matatizo yalioko hadi leo."

Unapoiangalia historia ya Afrika baada ya uhuru ni nadra kuthaminiwa mchango wa viongozi waliotangulia. Nyerere alikuwa Sauti ya Afrika na amebakia kuwa katika orodha ya viongozi wanaosifika hadi leo. Kwa Tanzania jina la Nyerere limendelea kutawala, ingawa kuna wanaodai halienziwi ipasavyo. Mjadala kuhusu hilo, ulizuka Oktoba 14 mwaka huu wakati wa kukumbuka ya miaka 22 tangu alipofariki. Nyerere alifariki 1999 wakati akitibiwa katika hospitali ya Mtakatifu Thomas mjini London.

Kiini cha mjadala katika mitandao ya kijamii kilikuwa Rais Samia Suluhu Hassan kushindwa kufika Butima kulizuru kaburi la Mwalimu siku ya kumbukumbu. Kufika Butiama ujumbe wa Bavicha (Baraza la vijana wa chama maarufu cha upinzani Chadema) kulizuru kaburi la muasisi wa taifa lao kulilufanya mjadala upambe moto. Kisiasa kumekuwa na maelezo yanayokinzana.

Kama binadamu mwingine yeyote na kiongozi, Nyerere alikuwa na mazuri na mapungufu yake. Lakini unapoyatathmini yote hayo, ukweli ni kwamba miaka 60 baada ya uhuru wa Tanganyika bado kivuli cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kinaendelea kuigubika siasa nchini Tanzania. Wapo wanaolalama kwamba dira ya Tanzania iliyokuweko enzi ya Nyerere imepotea. Ikiwa wako sahihi, basi ni ishara ya kwamba huenda bado Tanzania inahitaji kuwa na Mwalimu.