Afrika Kusini imesema 'imeadhibiwa' kwa kugundua virusi vipya vya corona aina ya Omicron

Takriban 24% tu ya Waafrika Kusini wamepatiwa chanjo kamili hadi sasa

Chanzo cha picha, Reuters

Iliyochapishwa

Afrika Kusini imelalamika kuwa inaadhibiwa - badala ya kupongezwa - kwa kugundua kirusi kipya cha corona aina ya Omicron.

Wizara ya mambo ya nje ilitoa kauli hiyo huku mataifa duniani kote yakizuia kusafiri kutoka kusini mwa Afrika huku taarifa za kuenea kwa ugonjwa huo yakiibuka.

Ushahidi wa mapema unaonesha kuwa Omicron ina hatari kubwa ya kuambukiza tena.

Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) lilisema Ijumaa kwamba aina mpya ya virusi "inatia wasiwasi".

Maambukizi ya watu kadhaa yamegunduliwa barani Ulaya - wawili nchini Uingereza,wawili nchini Ujerumani, mmoja Ubelgiji na nyingine nchini Italia, huku mtu mmoja akishukiwa kuwa na maambukizi nchini Jamhuri ya Czech.

Israel, ambapo aina mpya ya virusi imethibitishwa, imeamua kuwapiga marufuku wageni wote kuingia nchini humo kuanzia saa sita usiku Jumapili.

Hatua hiyo itaendelea kwa siku 14, kulingana na gazeti la Times of Israel.

Kesi za Omicron pia zimegunduliwa nchini Botswana, Hong Kong na Israel.

Mamia ya abiria wanaowasili Uholanzi kutoka Afrika Kusini wanafanyiwa kipimo kubaini kama wameambukizwa

Karibu watu 61 kwenye ndege mbili za KLM walikuwa na virusi vya Covid-19 na wametengwa katika hoteli karibu na uwanja wa ndege wa Amsterdam wa Schiphol huku wakifanyiwa vipimo zaidi, maafisa wa Uholanzi walisema.

Uholanzi kwa sasa inapambana na kuongezeka kwa rekodi ya maambukizi. Kufungiwa kwa sehemu kwa muda kunaanza kutekelezwa Jumapili jioni.

Aina mpya ya kirusi cha Omicron iliripotiwa kwa mara ya kwanza kwa WHO kutoka Afrika Kusini tarehe 24 Novemba.

'Sayansi bora'

Taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Afrika Kusini siku ya Jumamosi ilikosoa vikali marufuku ya kusafiri.

"Sayansi bora inapaswa kupongezwa na sio kuadhibiwa," ilisema.

Marufuku ilikuwa "sawa na kuadhibu Afrika Kusini kwa mpangilio wake wa hali ya juu wa jeni na uwezo wa kugundua kirusi kipya haraka".

Taarifa hiyo iliongeza kuwa majibu yalikuwa tofauti kabisa wakati virusi vipya vilipogunduliwa mahali pengine ulimwenguni.

Afisa wa Umoja wa Afrika aliiambia BBC kuwa nchi zilizoendelea ndizo zinazolaumiwa kwa kuibuka kwa tofauti hiyo.

"Kinachoendelea hivi sasa hakiepukiki, ni matokeo ya dunia kushindwa kutoa chanjo kwa njia ya usawa na ya haraka. Ni matokeo ya uhifadhi [wa chanjo] wa nchi za kipato cha juu duniani, na kabisa. kusema ukweli haikubaliki," mwenyekiti mwenza wa muungano wa utoaji chanjo wa AU Ayoade Alakija alisema.

"Marufuku haya ya kusafiri yanatokana na siasa, na sio sayansi. Ni makosa... Kwa nini tunaifungia Afrika wakati virusi hivi tayari viko katika mabara matatu?"

Siku ya Ijumaa na Jumamosi, nchi kadhaa zilitangaza hatua mpya;

  • Wasafiri kutoka Afrika Kusini, Namibia, Zimbabwe, Botswana, Angola, Msumbiji, Malawi, Zambia, Lesotho na Eswatini hawataweza kuingia Uingereza isipokuwa wawe raia wa Uingereza au Ireland, au wakazi wa Uingereza.
  • Maafisa wa Marekani walisema wageni watazuiwa kusafiri kutoka Afrika Kusini, Botswana, Zimbabwe, Namibia, Lesotho, Eswatini, Msumbiji na Malawi, wakiakisi hatua za awali zilizochukuliwa na EU. Zitaanza kutumika Jumatatu.
  • Australia ilitangaza Jumamosi kuwa safari za ndege kutoka Afrika Kusini, Namibia, Zimbabwe, Botswana, Lesotho, Eswatini, Ushelisheli, Malawi, na Msumbiji zitasitishwa kwa siku 14. Wasio Waaustralia ambao wamekuwa katika nchi hizo katika muda wa wiki mbili zilizopita sasa wamepigwa marufuku kuingia Australia
  • Japan imetangaza kuwa kuanzia Jumamosi, wasafiri kutoka sehemu kubwa ya kusini mwa Afrika watahitaji kuwekwa karantini kwa siku 10 na kuchukua jumla ya vipimo vinne wakati huo.
  • India imeamuru uchunguzi na upimaji mkali zaidi kwa wasafiri wanaowasili kutoka Afrika Kusini, Botswana na Hong Kong.
  • Canada inawazuia raia wote wa kigeni ambao wamesafiri kupitia Afrika Kusini, Namibia, Zimbabwe, Botswana, Lesotho, Eswatini au Msumbiji katika siku 14 zilizopita.