Paul Anyakun: Kijana aliyeanzisha utalii wa simu huko Uganda

    • Author, Roncliff Odit
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Iliyochapishwa

Kijiji cha kitamaduni. Densi za kitamaduni. Mifugo na wafugaji vijana. Hiyo ndio taswira inayokukaribisha katika eneo la Karamoja, mashariki mwa Uganda. Na kwa muda mrefu hiki kimekuwa kivutio kikubwa cha watalii kutoka maeneo mbali mbali kote duniani.

Lakini janga la Corona liliporindima, ndege zikaegeshwa na safari za kimataifa kukoma, eneo hili sawia na meneo mengine ya kitaliii, liliathirika pakubwa. Wenyeji ambao walitegemea utalii, wakajipata katika lindi la umaskini.

Lakini Paul Anyakun alikuwa na wazo tofauti. Chini ya mwavuli wa kampuni yake, Destination Nomad Afrika, Paul Anyakun, ama DNA kama anavyojulikana na wengi, alianzisha utalii wa mtandao, kwa kutumia video za simu.

'Awali tulikuwa tunajiuliza mtu ataona vipi video kwa simu na awe anafurahia utalii? Lakini sasa hauhitaji kulipia ndege ama gari, na bado unaweza kutalii eneo la Karamoja,' anasimulia DNA.

Sasa utalii huu unafanywaje?

Kimsingi ni kwamba kama uko Marekani au Ulaya, unatembezwa katika kijiji cha kitamaduni cha jamii ya Karamoja kwa kutumia simu yako tu.

'Wanapolipia ziara ya kitalii na sisi, kwanza kabisa tunauliza ungependa nini, kwa mfano kama unataka kupanda mlima au kutembelea kijiji cha jamii ya Karamoja. Kisha tunaenda kuangalia kama eneo hilo lina mtandao mzuri wa intaneti. Halafu siku ya ziara yenyewe, kwanza tunakupatia taswira na picha ya eneo tulipo, mimi sionekani kwenye video, kisha baada ya kukueleza kuhusu hapo, narudi kwenye kamera sasa, maana watu wanaamini zaidi wanapoona sura na hisi za macho yako unavyojieleza,' anaeleza DNA.

Wengi wa wateja wake ni wanafunzi kutoka Marekani na mataifa ya Ulaya ambao hawajahi kufika Afrika. Uwezekano wa kutembelea kijiji cha kitamaduni cha Karamoja wakiwa kwao nyumbani ni jambo la kusherehekewa kabisa.

Na sawia na biashara nyingine yoyote, utalii wa mtandao una changamoto zake.

'Kwanza ni simu, maana unaweza ukawa na simu ya Android kwa mfano, labda video yake si nzuri sana, wewe unamuona mteja vizuri, lakini mtalii anaona ni kama umemwagiwa maji usoni. Pia mtandao wetu si mzuri sana katika maeneo mengi ya Afrika, na hiyo inafanya kazi hii kua ngumu kidogo.'

Janga la Corona lilikwamisha kabisa shughuli za utalii katika maeneo mbali mbali duniani, lakini hapa Karamoja, mashariki mwa Uganda, Paul Anyakun almaarufu DNA, ametumia ubunifu kuhakikisha kwamba bado watalii wanazuru eneo hili, hata wakiwa kwa majumba yao iwe ni Marekani ama Ulaya.