Mohammed bin Salman: Mwanamfalme nchini Saudia alipendekeza kumuua mfalme Abdullah kwa sumu

Saad al Jabri
Iliyochapishwa

Mwanamfalme nchini Saudi Arabia alitoa pendekezo la kutumia sumu kumuua aliyekuwa mfalme wa nchi hiyo hayati Abdullah, kwa mujibu wa aliyekuwa afisa wa ujasusi wa cheo cha juu nchini Saudi Arabia.

Wakati wa mahojiano na kituo cha CBS, Saad al-Jabri alisema Mohammed bin Salman alimuambia binamu yake mwaka 2014 kuwa alitaka kufanya hivyo ili baba yake aweze kupata fursa ya kuingia mamlakani.

Kulikuwa na misukosuko ndani ya familia tawala wakati huo kuhusu ni nani angekuwa mrithi.

Serikali ya Saudi Arabia imemtaja Bw. Jabri kama afisa wa zamani asiye na maana mwenye historia ya kusema uongo.

Mohammed bin Salman kushoto alichukua mahala pake Mohamed bin Nayef kama mwamfalme wa Saudia

Chanzo cha picha, ANADOLU AGENCY

Maelezo ya picha, Mohammed bin Salman kushoto alichukua mahala pake Mohamed bin Nayef kama mwamfalme wa Saudia

Wakati wa mahojiano na kipindi cha CBS 60 Minutes, Bw. Jabri alionya kuwa mwanamfalme Mohammed, mtoto wa kiume wa Mfalme Salman ni mtu asiye na hisia, muuaji mashariki ya kati, aliye tisho kwa watu wake, Wamarekani na kwa dunia.

Alidai kuwa wakati wa mkutano uliofanyika mwaka 2014, mwanamfalme huyo alipendekeza kwa binamu yake kuwa Prince Mohammed bin Nayef, aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani wakati huo, kuwa angepanga mauaji ya Mfalme Abdullah.

"Alimuambia: Ninataka kumuua Mfalme Abdullah. Nitatafuta sumu kutoka Urusi. Inatosha kwangu kumsalimia tu kwa mkono na ni hivyo," alisema Bw Jabri.

"Huenda alikuwa anajigamba…alisema hayo na tuliyatilia sana maanani.

Alisema suala hilo lilitatuliwa kisiri. Lakini aliongeza kuwa mkutano huo ulirekodiwa kisiri kwenye video na kuwa anajua mahala zilipo nakala mbili za video hiyo.

Abdullah alifariki akiwa na miaka 90 mwaka 2015 na akarithiwa na ndugu wake wa kambo Salman, baba yake Mohammed bin Salman, ambaye alimteua Mohamed bin Nayef kuwa mwanamfalme.

Mfalme Abdullah kushoto alirithiwa na nduguye wa kambo Salman kulia baada ya kufariki 2015 akiwa na umri wa miaka 90

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Mfalme Abdullah kushoto alirithiwa na nduguye wa kambo Salman kulia baada ya kufariki 2015 akiwa na umri wa miaka 90

Mwaka 2017 Mohammed bin Nayef alivuliwa nafasi ya mrithi wa ufalme na Mohammed bin Salman. Pia akapoteza wadhifa wake kama waziri wa mambo ya ndani na inaripotiwa kuwa aliwekwa kwenye kifungo cha nyumbani kabla ya kufungwa mwaka uliopita kwa makosa ambayo hayajulikani.

Bw. Jabri alitoroka kwenda Canada baada ya Mohammed bin Nayef kuvuliwa wadhifa wake. Alisema kwenye mahojiano kuwa alionywa na rafiki yake katika idara ya ujasusi ya Mashariki ya Kati kuwa Mohammed bin Salman alikuwa anatumia watu wamuue Oktoba mwaka 2018, siku chache baada ya maajenti wa Saudi Arabia kumuua mwandishi wa habari raia wa Saudi Arabia Jamal Khashoggi nchini uturuki.

Alidai kuwa kundi la watu 6 waliwasili kwenye uwanja wa ndege wa Ottawa lakini wakarudishwa baada ya maafisa wa forodha kugundua kuwa walikuwa wamebeba vifaa vilivyotiliwa shaka vya kutumika kuchunguza DNA.

Mwaka uliopita Bw Jabri alimlaumu mwanamfalme kwa kujaribu kuua katika kesi iliyoandikishwa kwenye mahakama nchini Marekani.

Mwanamfalme alikana madai hayo. Pia amekana kuhusika kwenye mauaji ya Jamal Khashoggi, lakini idara za ujasusi nchini Marekani zilisema aliidhinisha oparesheni hiyo.

BBC imewasiliana na serikali ya Saudi Arabia juu ya madai hayo.

Katika taarifa iliyotumwa kwa CBS, ubalozi wa Saudi Arabia mjini Washington ulimtaja Bw Jabri kama afisa wa zamani wa serikali asiye wa maana aliye na historia ya kuongea uongo ili kuficha uhalifu wa kifedha aliotenda wa mabilioni ya dola, kufadhili maisha yake ya anasa na familia yake.

Bw Jabri anashtakiwa kwa ufisadi na mashirika kadhaa ya Saudi Arabia na jaji nchini Canada ametwaa mali yake akisema kuna ushahidi kuwa ufisadi ulitendeka.

Anakana kuiba pesa za serikali, akisema waajiri wake wa zamani walimzawadi vizuri.

Machi 2020 mamlaka za Saudi Arabia zilimkamata Omar, mtoto wa kiume wa Bw. Jabri na binti yake Sarah katika kile makundi ya haki za binadamu yanasema zilikuwa jitihada za kumlamzimisha arudi Saudi Arabia.

Novemba iliyopita miezi miwili baada ya baba yao kumshtaki mwanamfalme, watoto hao wake walihukumiwa miaka tisa na sita unusu mtawalia na mahakama ya Saudi Arabia, baada ya kushtakiwa kwa ulanguzi wa pesa na kujaribu kutoroka nchi humo.

Walikana mashtaka hayo.

Mahakama ya rufaa ilidumisha hukumu zao kwenye kesi iliyofanyika kisiri na ambayo hawakuwepo.