Simulizi ya vijana waliolazimishwa kuingia kwenye magenge ya biashara ya dawa za kulenya Uingereza

Iliyochapishwa

Si wachache: karibu vijana 4,000 wako katika hatari ya kutumiwa kila mwaka kusafirisha dawa za kulevya katika maeneo ya vijijini nchini Uingereza, kwa mujibu wa data iliyotolewa na taasisi isiyo ya kiserikali Safer London.

Wanaangukia mikononi mwa magenge ya kihalifu yanayotumia watoto, wengine hata wakiwa na umri wa miaka 12, kuuza dawa za kulevya kwa kutumia laini maalumu ya simu ya mkononi, kwa hivyo jina la utani ambalo wanajulikana: "laini za kaunti."

Mmoja wa watoto hawa alizungumza na BBC kuhusu jinsi wanavyoajiriwa na magenge ya wahalifu, kwa kile viongozi wanaona kama aina ya unyonyaji.

Michael * alikuwa na umri wa miaka 13 wakati rafiki yake wa shuleni alipomwendea kwa nia ya kumfanya muuzaji wa dawa za kulevya.

Akijaribiwa na wazo la kupata pesa, Michael alianza kuuza dawa za kulevya, maeneo ya jirani na kwake, lakini kidogo kidogo akafikia viwango vingine.

Genge lililompatia bidhaa hivi karibuni lilianza kumsafirisha nje kidogo ya jiji la London kwa ahadi kwamba yeye, kijana, angeweza kupata karibu dola 650 kwa wiki.

Alipelekwa kwenye nyumba ya mraibu ambaye genge hilo lilikuwa limemchukua katikati ya Uingereza, ili kuuzia bidhaa hiyo. (Na hupewa jina la cuckoo, ndege anayetaga mayai yake kwenye viota vilivyoachwa na ndege wengine.)

Ningeweza kupata zaidi kidogo

Kutumia nyumba hii kama msingi, Michael alitumia muda wake mitaani kuuza heroin, cocaine na usiku na mchana.

"Nilisumbuliwa kwa kiasi fulani, nilikuwa na hofu kweli," alisema.

"Lakini nilipopokea pesa, hapo nilibadilisha mawazo yangu na kufikiria 'sawa, ningeweza kupata zaidi kidogo'".

Na familia yake, haikugundua kutokuwepo kwake? Kulingana na simulizi yake, Michael alikuwa na maisha ya kawaida na uhusiano wa karibu sana na wazazi wake.

Lakini wakiwa na wasiwasi juu ya kutokuwepo kwake kwa muda mrefu, walijaribu kumzuia na kuficha simu yake ya mkononi, lakini mara tu alipoondoka nyumbani, genge lilianza kumsumbua tena.

Washirika wa genge walimpeleka kwenye nyumba ambapo waliwahudumia kifungua kinywa vijana kadhaa kabla ya shule.

"Halafu walitupeleka shuleni na kutufuata baada ya masomo," alisema.

Ingawa aliishi katika kundi la walevi wa dawa za kulevya, Michael anasema "hakuwahi kutambua hatari" au kuona jinsi angeweza kuwa mwathirika.

Anakumbuka kwamba usiku mmoja, baada ya kukwama mamia ya kilomita kutoka nyumbani kwake, aliishia kulala kwenye kaburi ndani ya eneo la makaburi.

"Mraibu wa madawa ya kulevya angeweza kuzungumza na muuzaji mwingine (muuzaji wa dawa za kulevya) na kusema" mtu huyu amelala kaburini na ana dawa za kulevya. "Kutoka hapo kitu chochote kingeweza kunitokea. Ilikuwa ni suala baya sana."

Baada ya kukamatwa na dawa za kulevya, Michael aliamua kuacha kuuza, lakini haikuwa rahisi kuacha genge hilo.

"Walijaribu kuniajiri tena, lakini niliweza kutoka eneo lao na nadhani hiyo ilisaidia sana," alielezea.

"Nilianza kupata maarifa tofauti kufanya kitu kingine maishani mwangu.''

Ahadi zinazogeuka kuwa vitisho

Taasisi ya Safer London imeshughulika na vijana wengi kama Michael, ambao wamenyonywa na watu wa umri mkubwa kuliko wao kwenye makundi ya wahalifu ili kuuza dawa.

Mkurugenzi wa Safer London Claire Hubberstey anabainisha kuwa idadi kubwa ya vijana wako katika hatari ya kunaswa kwenye hizi zinazoitwa "laini za kaunti".

"Tunaanza kumsajili kijana wakati tunapoona kuwa kuna aina ya tishio ambalo linatuogopesha," alisema.

Kulingana na hesabu kulingana na idadi ya vijana ambayo taasisi hiyo inawahudumia, wanakadiria kuwa watoto 4,000 huingia kwenye changamoto hiyo kila mwaka kwa kuingia katika mitandao hii ya biashara.

Hubberstey anaifananisha na jinsi vijana wanavyoingizwa katika biashara ya ngono: ahadi za mwanzoni hubadilika kuwa vitisho.

"Vijana mara nyingi huzungumza kuhusu kufungwa kimwili katika maeneo ambayo hawawezi kutoroka," alisema.

"Vitisho vinavyohusisha vurugu vina maana kwamba wanaweza kuogopa sana na hawawezi kutoroka. Hata ikiwa wana uwezo wa kufanya hivyo," ameongeza.

Kwa Hubberstey, vijana hawa wanapaswa kutibiwa kama waathirika wa biashara ya binadamu na sio kama wahalifu.

"Hawa ni watoto wanaonyonywa na wanatumiwa. Hata ikiwa hawatambui, haimaanishi (unyanyasaji) haufanyiki," alisema.

Idadi inayoogopesha

Kevin Hyland, Kamishna wa Kupambana na Utumwa - ofisi ya Uingereza iliyojitolea kupigana na biashara ya binadamu - alibaini kuwa kile kinachoitwa "laini za kaunti" zinaanza kutambuliwa.

"Tunaamka, lakini je, tumeamka kabisa kuhusiana na jambo hili? Labda sivyo, lakini tunaanza ," Hyland alisema.

Na akaongeza kuwa kumaliza tatizo hili itahitaji kubadilisha mawazo ya polisi na mamlaka nyingine ili waweze kuwatambua wafanyabiashara wadogo kama waathirika, na sio kama wahalifu.

Sarah Newton, Waziri anayeshughulikia masuala ya Uhalifu wa Uingereza, Ulinzi na Mazingira Hatarishi, alibainisha kuwa - pamoja na kuongeza rasilimali kufadhili kampeni ya kupambana na utumwa - serikali imechukua hatua ikiwa ni pamoja na sheria inayoruhusu polisi kuchukua simu ambayo inatumika katika soko la dawa za kulevya. .