Majaji wa kike waliokuwa na ushawishi mkubwa Afghanistan sasa wapo mashakani

Iliyochapishwa

Hadi mwezi Agosti mwak huu, Farishta alikua mwendesha mashtaka mwenye ushawishi na ambaye alitumia mamlaka yake ipasavyo kutekeleza majukumu yake.

Aliwashtaki wahalifu, wanamgambo wa Taliban, watendaji wakuu mafisadi na wanaume ambao walipiga wanawake na watoto.

Leo, Farishta mwenye miaka 27- yuko mafichoni. Kama mkimbizi kila mara anabadilisha mahali alipo. Kwa ajili ya usalama wake, tumebadilisha jina lake.

Farishta anayetokea mkoa wa Paktia kusini -mashariki mwa Afghanistan, ni miongoni mwa wanawake wa Afghanistan waliofanikiwa katika taaluma zao katika miaka ya baada ya Taliban kushindwa, na kudhubutu kufikia malengo yao katika jamii ya kihafidhina na inayotawaliwa na wanaume.

Miaka mitano iliyopita, chini ya utawala uliondoka madarakani huko Afghanistan, alikuwa mwendesha mashtaka katika ofisi ya Mwanasheria mkuu wa Afghanistan.

Baadhi ya majukumu yake yalikua "kushtaki na kupendekeza hukumu dhidi ya wale waliofanya ubakaji, mauaji na unyanyasaji wa kinyumbani", aliambia BBC kutoka mafichoni mwake nchini Afghanistan. Ilikuwa "kazi ngumu lakini ya kuridhisha'' alisema.

Lakini wakati Taliban walipoanza kuteka maeneo tofauti ya Afghanistan katika miezi ya hivi karibuni , kabla ya kuchukua uongozi wa nchi, na kuwaachilia huru wafungwa, wakiwemo maelfu ya wahalifu sugu na wanamgambo wa Kiislam.

Miongoni mwa walioachiliwa huru na Taliban ni Mohamad Gol, ambaye alikua anakabiliwa na mashataka ya kupanga mashambulio ya bomu la kujitoa mhanga kufa.

Farishta alikuwa amekusanya ushahidi wa kutosha dhidi ya Gol na kufanikiwa kumfungulia mashataka, na hatimaye akahukumiwa kifungo cha miaka 20.

Siku kadhaa baada ya Taliban kuchukua udhibiti wa mji wa Kabul, Mohammed Gol alimpigia simu, Farishta. "Aliniambia anakuja kulipiza kisasi, na siwezi kujificha popote.''

Tangu wakati huo, amekua mbioni. Bila ya kuwa na mshahara imekuwa vigumu kwake kujikimu kimaisha.

Farishta na wafanyakazi wenzake wa zamani wanasema Taliban wanapinga wanawake kufanya kazi ya kuendesha mashataka na majaji na wanataka wanawake wasifanye kazi, kama walivyofanya wakati wa utawala wao wa hadi mwishoni mwa miaka ya 1990.

Wanawake kama Farishta wana kila sababu ya kuwa na hofu. Mnamo mwezi Januari majaji wawili wa kike katika mahakama ya Juu zaidi nchini Afghanistan waliuawa kwa kupigwa risasi - katika msururu wa wimbi la mauaji yaliyowalenga wanawake, yanayosadikiwa kufanywa na Taliban.

Maafisa wawili wa sheria waliokuwa wakifanya kazi katika Wizara ya Haki ya Afghanistan pia waliuawa mjini Kabul katika wiki za hivi karibuni katika kile kinachoaminiwa kuwa mashambulio ya kulipiza kisasi.

Makundi ya kimataifa ya kutetea haki yakiwemo mashirika ya kutetea haki ya Amnesty na Human Rights watch yameripoti mauaji ya kiholela na utekaji, licha ya msamaha uliotangazwa na Taliban kwa wafanyakazi wa serikali.

Mamia ya majaji wanawake walikimbilia mafichoni baada ya kundi hilo kuchukua madaraka mwezi Agosti.

Baadhi yao waling'ang'ania kuondoka nchini wakati Marekani ilipokuwa ikiongoza shughuli ya kuwaondoa wafanyakazi wake nchini humo mwezi Agosti, wengine walisalia Afhanistan kwa kukosa budi.

"Mimi binafsi nimepokea simu kadhaa za vitisho kutoka kwa Taliban na wanachama wao," alisema jaji mwanamke katika mkoa wa Parwan, amabye ni miongoni mwa wale waliotaka kuondoka nchini humo.

Jaji aliyeanza kazi mwaka 2018, sasa anaishi Uingereza. Anasema mali zake na vitu vyote alivyomiliki vinashikiliwa na Taliban na jamaa zake wanakabiliwa na hatari ya kuteswa na kundi hilo la kijihadi.

"Majaji wanawake walikuwa na jukumu muhimu la kubuni sheria ya kukabiliana na ufisadi ndani ya serikali," alisema. "Wakiondoka nchi wataacha, pengo kubwa katika idara ya mahakama."

Kuna karibu majaji wanawake 230 Afghanistan ambao wamekwama nchin humo, na wote wako mafichoni. Kulingana na mahojiano na majaji na wanaharakati wanaofanya kazi kwa niaba yao, wakazi wa zamani wamekua wakiwatafuta kila mahali huku jamaa zao wakitishiwa.

"Taaluma zao zimeisha, akaunti zao za benki zimefungwana hatma yao ya baadaye kama wanawake wa Afghanistan haijulikani," alisema jaji Anisa Dhanji, mwakilishi wa Uingereza wa Chama cha Kimataifa cha Majaji Wanawake, IAWJ.

IAWJ, ambayo imewahi kuwapatia mafunzo majaji kadhaa wa kike wa Afghanistan, waliingilia kati mpango wa kuwaondoa makumi ya majaji hao nchini licha ya vurugu zilizoshuhudiwa katia uwanja wa ndege wa Kabul baada ya Taliban kuchukua uongozi.

Ilikuwa oparesheni ngumu iliyojumuisha timu kadhaa kufanya kazi usiku na mchana kwa kutumia ramani,wakalimani na kushirikisha ripoti za kijasusi kuhusu kile kilichofanyika katika lango kuu la kuingia uwanja wa ndege wa Kabul.

Katika mazingira yasiyokua ya kawaida karibu majaji 40 wa kike wa Afghanistan ana familia zao waliondolewa nchini.

Baadhi yao sasa wanaishi Marekani, Ulaya na wengine wako Uturuki, Tajikistan, Iran na mataifa ya Ghuba. Lakini wengine wengi waliachwa nyuma.

Mmoja wa majaji wanaojificha mjini Kabul aliambia IAWJ kwamba mwanamume aliyemhukumu kwa mashtaka ya ugaidi kando na kumtishia baada ya akuachiliwa, lakini pia ametuliwa kama jaji wa Taliban.

Jaji mwingine amesema anakaribia kujifungua kupitia upasuaji uliopangwa, lakini anahofia kwenda hospitali kwani huenda akatambuliwa.

Zaidi ya visa hivi vya kushangaza, kusambaratika ghafla kwa mfumo wa mahakama umewaathiri vibaya wanawake wanaotafuta haki nchini Afghanistan.

"Kwa kuwa mahakama zimefungwa, wanawake hawana mahali pa kuwasilisha malalamiko yao ya kubakwa au kutelekezwa na waume zao na wanaume wengine," alisema Zainab, wakili huru anayeendesha kampuni za kisheria katika miji kadhaa ya Afghanistan, ambaye tumebadilisha jina lake.

"Hakuna mtu anayejitokeza kuwasilisha masuala hayo kwa sababu hakuna tena mawakili wa kike," alisema.

Ofisi zote za Zainab zimefungwa na wafanyakazi wake kupoteza ajira zaos. Anasema amekuwa akipokea vitisho, kutoka kwa mwanamume aliyewahi kumfungulia mashtaka ya ubakaji lakini aliwachiliwa huru naTaliban.

"Alisema, 'Nitakupata, hata ukijificha Herat, kisha nikuwasilishe kwa Taliban'."

Msemaji wa Taliban wa ngazi ya juu ambaye pia ni waziri ametenga kundi hilo na vitisho hivyo na visa vya upekuzi wa maeneo ya kazi ya majaji wa kike na maafisa wengine wa sheria.

"Tunapinga madai hayo, wapiganaji wetu hawawezi kufanya kitu kama hicho," Zabihullah Mujahid aliambia BBC.

Alipoulizwa kama majaji na waendesha mashtaka wa kike wataruhusiwa kurejea kazini, Mujahid alisema, "Uamuzi utafanywa na mfumo unaendelea kufanyiwa kazi. Baada ya hapo ndipo kila kitu kitawekwa wazi."

Wanaharakati wanasema muda unayoyoma kwa majaji na mawakili wanawake wa Afghanistan walio mafichoni.

"Cha msingi kwa sasa nikuwasidia wale wanoataka kuondoka nchini humo," alisema jaji Dhanji.

"Maisha yao na ya familia zao ziko hatarini. Wanawindwa kwa kuwa waliwahukumu wanaume waliokua na hatia."