Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Waridi wa BBC: Mfahamu Teresia Njeri mwanamke asiyeweza kutabasamu
- Author, Anne Ngugi
- Nafasi, BBC Swahili
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Kutabasamu ni jambo la kawaida kwa mwanadamu yeyote yule ambaye anahisi furaha duniani .
Lakini kwa Teresia Njeri , mwanamke mwenye umri wa miaka 35 kutoka Kenya , hana uwezo wa kutabasamu hata kidogo baada ya kuugua saratani kwa jina Adenoid cystc Carcinoma - aina ya saratani ambayo inaathiri maeneo ya uso hususan pua , macho na mdomo .
Alipofanyiwa upasuaji kuondoa sehemu ya juu ya mdomo wake hapo ndipo maisha yake yalipobadilika kwa kiasi cha kuathiri muonekano wake na hasa kutabasamu kwake.
Je tatizo lake lilianzaje?
Matatizo yake yalianzia mwanzoni mwa mwaka jana wakati akiwa na umri wa miaka 34.
Lakini ni nini hufanyika wakati maumivu ya kichwa ya kawaida asubuhi hubadilika na kuwa ndoto mbaya ? ndoto ambayo ilitishia hadi kuyachukua maisha yake bi Njeri .
''Nilianza kuumwa kwa ghafla nilipoamka tarehe 13 mwezi Februari 2020 . Nilikuwa na uchungu mwingi ulioanzia sehemu ya chini ya shingo yangu, pia nilikuwa natokwa na kamasi nyepesi ''anakumbuka.
Mwanamke huyo alikuwa anaelekea katika shule mmoja ambapo yeye ni mwalimu , ila alipowasili siku hiyo ilikuwa vigumu kwake kuzungumza kutokana na uchungu mwingi aliokuwa anauhisi .
Licha ya kuomba ruhusa apumzike aliendelea kuhisi maumivu makali kichwani.
Alilazimika kwenda hospitalini ili apewe dawa za kupunguza maumivu ya kichwa .
Alipowasili hospitali, daktari aliyekuwa anamshughulikia alimshauri apitie vipimo mbalimbali na pia kupigwa picha za uso na hususan aktika pua na mashavu ambapo alikuwa anahisi uchungu mwingi.
Baada ya siku chache, matokeo yake yalikuwa sio ya kuridhisha mno na yaliashiria mwanzo wa mahangaiko ya kuokoa maisha yake na kuenea kwa ugonjwa uliogundulika
''Mwishowe niligunduliwa nina aina adimu ya Saratani inayojulikana kama Adenoid cystc Carcinoma - inayoathiri maeneo ya uso ikiwemo macho, pua na masikio, matokeo ya uchunguzi huo ulimshtua sana bi Njeri.
Kwa kawaida mtu anapopokea habari za kuugua ugonjwa sugu , wengi hukata tamaa na kuanza kuwa na mafikra ya kifo hivyobasi haikuwa tofauti na jinsi mwanadada huyu alivyopokea habari hizo za kuvunja moyo.
'Nakumbuka kuwa kwenye chumba cha kunipa majibu ya utafiti waliofanyia mwili wangu kulikuwa na kikosi cha madaktari , waliponieleza hayo , nakumbuka nikikosa la kusema . Niliposikia tu neno saratani nilihisi kifo , nilianza mara moja kufikiria kuwa sina wakati mwingi duniani'
Cha ajabu ni kuwa mwanadada huyu anasema kuwa anakumbuka wakati huo hakuwa na dalili zozote za kuonesha kwamba alikuwa anaugua ugonjwa fulani licha ya maumivu makali aliyokuwa akihisi kutoka sehemu ya shingo na kichwa .
Teresiah alianza harakati za kutafuta matibabu ili kuokoa maisha yake.
Alikumbuka kwamba ana mtoto mwenye umri wa miaka 12 ambaye anamtegemea kwa kila jambo hivyobasi akapiga moyo konde na kuamua apambane hadi mwisho.
Anasema kwamba ilibidi matibabu yake yaharakishwe kufuatia kutangazwa kwa janga la corona nchini na duniani kwa jumla.
Matibabu yake yalikuwa ya kipekee hivyobasi alihitaji akubali kuwa sehemu muhimu za sura yake kwa mfano upande mmoja wa uso wake kwa ndani ufizi na koromeo ziondolewe kabisa na badala yake awekwe zilizobandia
Bila shaka ni matibabu yaliobadilisha muonekano wake wa uso kiasi cha kuwa anasema, watu waliokuwa wanamfahamu miaka mitatu nyuma hawakumfahamu tena hasa kutokana na vyuma vingi kuwekwa mdomoni mwake na sehemu yake ya pua na macho .
Mbali na kuwa sura yake ilibadilika , majukumu yaliokuwa yanafanywa na sehemu zilizoondolewa kwa mfano kutafuna chakula cha kawaida mdomoni , haikuwezekana tena .
Bi Njeri anasema kuwa tatizo hilo lilimfanya kushindwa kutafuna vyakula vigumu na badala yake kuanza kutumia vyakula vilivyosagwa kama vile vya watoto wachanga .
Hilo linatokana na kuathirika kwa mfupa mkuu unaoshikilia shavu la upande ulioathirika pamoja na sehemu inayounganisha mdomo na pua ambapo badala yake amewekwa chuma maalumu.
Aidha mwanamke huyo anasema kwamba mdomo wake hauwezi kufunguka wote na amekuwa akihitaji kutumia makasi maalum.
Changamoto nyengine ambayo amekuwa nayo ni ile kushundwa kuzungumza kwa sauti ya juu hali iliomfanya aache kazi yake ya kuwa mwalimu kwani hana tena uwezo wa kuzungumza kwa sauti kubwa .
Je saratani ya Adenoid Cystic Carcinoma ni ipi ?
Saratani hii pia inajulikana kama Adenoid Cystic Carcinoma (ACC) ni aina nadra sana na isiyo ya kawaida ya saratani.
Kwa kawaida huwaathiri sana watu wazima wenye umri wa kati na wazee na visa vingi hutokea katika sehemu za kichwa na shingo, ila wataalam hawatupilii mbali uwezekano wa watu wa umri mwengine kuathirika .
Visa asilimia 60% vya maradhi hayo vimeonekana kuathiri eneo la mdomo pamoja na tezi kuu na ndogo za mate, ulimi, ufizi, midomo, na koromeo. Maeneo mengine ya mwili ni pamoja na ngozi, masikio, mapafu, pua, zoloto, umio, matiti, uke na eneo la kizazi .
Tatizo kuu ni kwamba aina hii ya saratani sio ya kawaida hivyobasi ufahamu wake ni mchache miongoni mwa wataalamu.
Kinachojulikana kuhusu maradhi haya ni kwamba mara nyingi uvimbe unapoanza hakuna maumivu yoyote yanayohisiwa , hivyobasi uvimbe huendelea kukua polepole.
Matibabu yake ni kupitia njia ya upasuaji au tiba ya mionzi chemo.
Je! ni nini kinachosababisha maradhi haya?
Hadi kufikia sasa hakuna sababu za moja kwa moja zilizotajwa zinazodaiwa kuwa chanzo cha maradhi haya.
Hatahivyo saratani inaweza kuongezeka kulingana na sababu kadhaa za hatari ambazo ni pamoja na: kuendelea kuongeza uzani au kunenepa , matumizi ya tumbaku, sigara , unywaji wa pombe kupitia kiasi, lishe duni na iwapo kuna historia yoyote ya maradhi ya saratani katika familia.