Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Virusi vya Corona: Rais Samia Suluhu na Changamoto ya Corona na Chanjo
- Author, Mohammed Abdulrahaman
- Nafasi, Mchambuzi
- Iliyochapishwa
Mojawapo ya taarifa kubwa zinazoendelea kugonga sana vichwa vya habari kuhusu Tanzania tokea Machi 2020 ni kuhusu maambukizi ya Corona (Covid-19) janga lililoikumba dunia kwa jumla. Chanzo cha kumulikwa taifa hilo la Afrika Mashariki ni msimamo wa aliyekuwa Rais wake John Pombe Joseph Maguful .
Magufuli aliripotiwa sana kwa staili yake ya uongozi kuanzia ahadi ya kupambana na rushwa ambapo alipongezwa na wengi , hadi ukandamizaji wa demokrasia na haki za binaadamu ambapo alikosolewa vikali.
Corona na msimamo wa awali
Msimamo wa awali wa Rais Magufuli kuhusu Corona, ulitafautiana kabisa na wa viongozi wengine duniani. Magufuli alikataa kabisa kwamba kuna Covid-19 nchini mwake na hatimaye kusisitiza kuwa sala na maombi yameinusuru nchi hiyo na akapiga marufuku kuchapishwa ripoti kuhusu idadi ya mambukizi au vifo vilivyotokana na ugonjwa huo. Akisisitiza," Kila mtu atakufa, iwe ni kwa maradhi haya au malaria au ugonjwa mwengine."
Lakini kinyume na msimamo wake, taasisi kadhaa za umma zikiwemo shule zilionya juu ya kusambaa kwa virusi.Viongozi kadhaa wa kanisa wakajitokeza kuwa mstari wa mbele kuutahadharisha umma kuhusu janga la Corona.
Viongozi wa baadhi ya vyama vya kisiasa kikiwemo chama kikuu cha upinzani CHADEMA, nao wakapaza sauti kumkosoa Rais Magufuli, huku katika mitandao ya kijamii kukionekana picha za vifo vya wagonjwa wa Covid katika maeneo kadhaa ya Tanzania.
Msimamo wa Tanzania chini ya Magufuli ulitafautiana na ule wa nchi tatu jirani na wanachama ndugu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Kenya, Uganda na Rwanda ambazo zote katika hatua za awali zilichukua uamuzi wa kufunga shughuli na hafla zote za mikusanyiko, ikiwa ni pamoja na kutangaza amri ya kutotoaka nje usiku hadi saa 12 asubuhi.
Hatua za haraka za serikali za mataifa hayo ikiwemo kutoa taarifa kuhusu idadi ya maambukizi na vifo zilisaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza kiwango cha athari za Corona. Ni Burundi pekee, mwanachama mwengine wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, iliokataa hapo awali kwamba kulikuwa na Corona nchini humo, lakini baadae ikakiri kuwepo na kuanza kutoa taarfa juu y aidadi ya mambukizi na idadi ya waliofariki. Rais Magufuli alifariki dunia Machi 17, 2021 na Juni 8, Rais Burundi Pierre Nkurunzizanaye akaaga dunia..
Taarifa ya serikali ya Tanzania ilisema kifo cha Magufuli kilitokana na matatizo ya moyo yaliomsumbua muda mrefu na serikali ya Burundi alielezea sababu ya kifo cha Nkurunziza kuwa mshtuko wa moyo. Lakini baadhi ya duru zikiwemo zile za Habari zilieleza kuwa vifo vya viongozi hao vilisababishwa na maambukizi ya Covid-19. Mapema mwezi Februari aliyekuwa Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Seif Shariff Hamadi alitangaza ameambukizwa Covid-19 na akafariki tarehe 17 ya mwezi huo huo, akimtangulia Rais Magufuli.
Mrithi wa Magufuli aitambua hali halisi
Tanzania ilibadili msimamo baada ya Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan kushika hatamu za kuliongoza taifa hilo akiwa mrithi wa Magufuli. Rais Samia Suluhu pia alizungumza kwa wazi juu ya kitisho cha Corona na kuutanabahisha umma akisema kila mtu anapaswa kuchukua tahadhari. Akizungumza katika hafla moja, alikuwa na ujumbe kwa wanaokataa kuwepo kwa Corona na kusema," Wanaokataa kuwa haupo janga hili halijawafika wao au familia zao. Akionyesha mfano Rais Samia Suluhu akaanza kuovaa barakao, Msimamo huo mpya ulitafautiana na ule wa mtangulizi wake ambapo wakati wake si yeye binafsi wala mawziri wa serikali waliothubutu kufanya hivyo. Hivi sasa hata waliokuwa wale waliokuwa wakipiga debe kwa kusema Corona imekwisha Tanzania wanaonekana wakivaa barakoa.
Miongoni mwao ni Waziri wa afya Dorothy Gwajima aliyewataka watu kutumia dawa za asili na hata kuonyesha kinywaji alichodai kinazuwia maambukizi ya Corona.
Mwengine ni Profesa Palamagamba Kabudi, aliyesafiri kwenda Madagascar kupokea shehena ya kinywaji kilichopewa jina Covid Organic (CVO) ambacho Rais wa Madagascar alidai ni tiba dhidi ya Corona. Kabudi aliitisha mkutano na waandishi habari na kutoa maelezo juu ya kinywaji hicho, huku akinywa kuonesha mfano.
Kabudi alibadilishwa wizara kuwa katiba mabadiliko ya baraza la mawaziri ya Rais Suluhu Machi 2021 na sasa ni Waziri wa masuala ya Katiba na Sheria.
Athari za tamko la chanjo ni kwa hiyari
Changamoto kubwa baada ya Rais Samia Suluhu kutambua ukubwa wa janga la Corona ugonjwa, imekuwa ni chanjo na kwanza kabisa alilazimika kurejesha ushirikiano na Shirika la Afya Dunia-WHO. Wakati Jamii ikigawika kuhusu suala zima la chanjo, aliunda kamati maalum ya wataalamu kutathmini ikiwa chanjo ni salama. Kamati hiyo iliwasilisha ripoti yake na kueleza kwamba chanjo ni salama na kuonya juu ya kitisho cha wimbi la tatu Corona.
Rais Samia Suluhu alizindua rasmi akampeni ya chanjo akiwa wa kwanza kuchanjwa mwezi Julai. Tanzania alianza kupokea chanjo ikiwemo ile ya mara moja ya Johnson Johnson iliotolewa na Marekani na Covax kupitia mpango wa chanjo wa Umoja wa Mataifa.
Kuanza kutolewa kwa chanjo, kumeizindua pia serikali ya Zanzibar yenye mamlaka yake ya ndani. Miezi michache iliopita Zanzibar ambayo sasa ni maarufu kwa utalii ilielekea kuweka mbele tamaa ya tija za kiuchumi kuliko afya, iliporuhusu wimbi kubwa la watalii kutoka Urusi kuingia visiwani humo bila kuwepo utaratibu maalum na wa vitendo kuhusu Covid-19.
Tokea Julai Zanzibar imezindua zoezi la chanjo ya Cinovac kutoka China.Wiki iliopita aziri wa afya Nassor Mazrui akatangaza utoaji kadi maalum kwa waliochanjwa wakitozwa ada ya Shilingi 20,000.
Ingawa mwitikio wa chanjo Tanzania kwa jumla ni mkubwa, bado kuna baadhi wanaolibeza zoezi hilo na kwa kutoa matamshi yanayopinga matumizi ya chanjo kuwa si salama. Kwa upande mwengine, tamko la serikali kuwa chanjo ni hiyari, linahofiwa linaweza kudhoofisha mafanikio ya kukabiliana na Covid-19, kwa watu kudharau. Matokeo yake yatakuwa ni kuwa na matatizo katika kupunguza maambukizi.
Katika kile kilichoonekana kuwa ni Rais Samia Suluhu kukabiliwa na upinzani hata miongoni mwa viongozi kutoka chama chake tawala, Chama cha Mapinduzi-CCM, chama hicho kilitoa taarifa kuwaonya wenye kutafautiana na Rais na Mwenyekiti wao kuhusu Corona.
Waliotokeza wazi hadharni kuwa na msimamo tofauti ni wabunge wawili, Askofu Josephat Gwajima (mbunge wa kuchaguliwa) na Humpfrey Polepole Katibu Mwenezi wa zamani wa CCM na sasa mbunge wa kuteuliwa. Wakati Chama hicho kikitishia kuwachukulia hatua , Askofu Gwajima ameendelea kuwashawaishi waumini wa Kanisa lake kwamba chanjo ni hatari kwa maisha yao na kusisitiza ataendelea na msimamo wake kuipinga.
Athari ya tamko chanjo ni hiyari
Wadadisi wana wasiwasi kwamba lile tamko la serikali kwamba kuchanja ni hiyari, linafifisha juhudi za kufanikisha zoezi hilo kwa haraka. Sababu kubwa ni kuwa bado kuna watu ambao wanaoamini na kushawishika na msimamo ule ule aliokuwa nao Rais Magufuli wakati wa uhai wake kuhusu Corona. Taarifa za hivi karibuni zimeashiria kuongezeka kwa mambukizi na vifo hata mikoani nje ya jiji la Dar-es-salaam, wakiwemo watu mashuhuri katika duru za kibiashara.
Mwamko juu ya umuhimu wa chanjo unaendelea, lakini vyombo vya habari kupitia wizara ya habari , taasisi na asasi za kijamii vinawajibu wa kuimarisha kampeni ya kuuzindua umma kwamba janga la Corona bado lipo na kwamba chanjo ni muhimu katika kujinusuru, sambamba na hatua nyengine kama kunawa mikono kila wakati, kuvaa barakoa na kuepuka mikusanyiko mikubwa ya watu, ili kukabiliana vyema na wimbi hili la tatu la Covid-19 ambayo imepewa msamiati mpya wa Kiswahili wa UVIKO-19.