Ethiopia:Hofu yaibuka kuhusu umoja wa Ethiopia huku mzozo wa Tigray ukisambaa

et

Chanzo cha picha, AFP

Iliyochapishwa

Kuna wasiwasi unaoongezeka juu ya umoja nchini Ethiopia wakati mzozo katika eneo la kaskazini la Tigray unazidi kuongezeka.

Vita vya miezi tisa kati ya vikosi vya waasi vya Tigray na jeshi la Ethiopia na washirika wake vinaelekea kudhibitiwa katika eneo la Tigray lenyewe.

Lakini mapigano yanaenea katika maeneo jirani ya Amhara na Afar.

Hii inafuatia hatua ya vikosi vya Tigray kuendelea kuchukua maeneo mengi, pamoja na kuteka mji mkuu wa eneo hilo, Mekelle, mnamo mwezi Juni baada ya wanajeshi wa Ethiopia kujiondoa na serikali kutangaza kusitisha mapigano ya upande mmoja.

Ni ishara kwamba mgogoro wa Tigray unazidi kuwa mbaya, lakini haya sio mapigano pekee yanayotokea hivi sasa nchini Ethiopia.

Ni jimbo la pili lenye idadi kubwa ya watu barani Afrika lenye historia ya mivutano ya kikabila.

Mnamo mwaka 1994, katiba mpya ilianzishwa ambayo iliunda msururu wa mikoa yenye misingi ya kikabila iliyokusudiwa kushughulikia shida ya uwepo was nguvu kubwa ya kiutawala katika eneo moja.

Hadi mwaka 2018, muungano unaotawala ulitawaliwa na chama cha Tigray Peoples Liberation Front (TPLF) na kilikosolewa kwa kukandamiza wapinzani wowote waliojitokeza.

ETH

Chanzo cha picha, AFP

Baada ya Abiy Ahmed - anayetoka moja ya kabila kubwa zaidi, Oromo - kuwa waziri mkuu mnamo 2018, alifanya mfululizo wa harakati za ujasiri za kukomesha ukandamizaji wa serikali.

Lakini ukombozi huu uliambatana na utaifa wa kikabila kwa kiasi kikubwa tu na vikundi tofauti vikadai nguvu zaidi na ardhi.

"Kuna vita vya kikabila vingi", anasema Rashid Abdi, mtaalam wa masuala ya usalama katika eneo la pembe ya Afrika.

"Eneo moja ni la magharibi la Benishangul-Gumuz - ambalo linapakana na Sudan na Sudan Kusini - na linaelezewa na Bwana Abdi kama "lenye mgogoro wa kidumu kisiasa."

Karibu watu 200 waliuawa katika shambulio katika eneo hilo.

Wiki iliyopita, viongozi wa eneo walisema vikosi vya usalama viliwaua zaidi ya wapiganaji 100 kutoka kikundi chenye silaha ambacho kililaumiwa kwa kuchochea mashambulio ya kikabila mnamo mwezi Desemba.

Pia kinachozorotesha uthabiti ni mzozo wa mpaka wa kihistoria kati ya Sudan na Ethiopia juu ya eneo la kilimo lenye rotuba katika sehemu inayofahamika kama al-Fashaga ambayo pia majimbo yote mawili yanadai kulimiliki.

Mzozo huo umesababisha mapigano kati ya majeshi mawili wakati mzozo huko Tigray unendelea.

"Una uwezo wa kuongezeka lakini kwa sasa bado", Bwana Abdi anasema.

Na kwa siku moja wiki iliyopita, wakimbizi 1,100 kutoka kabila dogo la Ethiopia la Qemant walikimbilia Sudan kutoroka mapigano huko Amhara, eneo la Ethiopia ambao linapakana na Tigray, vyombo vya habari vya Sudan viliripoti.

Mamlaka ya eneo la Amhara katika miaka kumi iliyopita wameshtumu Tigray kwa kuchochea uhasama wa kikabila, madai ambayo mamlaka ya Tigray imeyakanusha.

ETH

Chanzo cha picha, Reuters

Ameongeza kwamba kuongezeka kwa mzozo wa muda mrefu kati ya Somalia na Afar huko Ethiopia, karibu na eneo la mpaka wa Djibouti, na uasi unaoongezeka dhidi ya jeshi la Ethiopia katika mkoa wa Oromia, ni rahisi kuona ni kwanini waangalizi wa Ethiopia wana wasiwasi.

"Ethiopia ina historia ya kuwa imara na kisha kuwa hatari na ni katika moja wapo ya nyakati mbaya sana", anasema Alex de Waal, mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Amani Duniani huko Merekani.

Wataalam wengine wa Ethiopia sasa wanazungumza juu ya kuanguka kwa serikali kama uwezekano wa kweli.

"Hakuna kukana kwamba Ethiopia iko katika kipindi cha mzozo", anasema Bw Abdi.

"Je itakabiliana vipi na mgogoro huu huko Tigray pamoja na vita vya kikabila kadhaa ambavyo hakuna mtu anayeweza kuwa na uhakika, lakini iko katika shida kubwa na kuna hatari kubwa ya Ethiopia kusambaratika", amesema.

Lakini msomi katika Chuo Kikuu cha Gondar cha Ethiopia, Menychle Meseret, alisema haamini kwamba serikali ya Ethiopia iko karibu na kusambaratika.

"Hata haifai kuwa na majadiliano juu ya suala hili, kwanza, tuna serikali inayofanya kazi inayodhibiti nchi, isipokuwa Tigray", alisema.

Mgogoro wa Tigray, kwa kweli, uliimarisha "mshikamano wa kitaifa" kati ya maeneo mingine na vikundi vya kikabila, ambavyo vimeunga mkono serikali na jeshi, Bwana Menychle ameongeza.

Vikosi vya Tigray vimesema havitaacha kupigana hadi mambo kadhaa yatimizwe na Bwana Abiy.

Hii ni pamoja na kumalizika kwa zuio la serikali dhidi ya Tigray na kuondolewa kwa wanajeshi wote wanaopinga - jeshi la Ethiopia, vikosi kutoka maeneo mingine ya Ethiopia na Waeritrea wanaopigana nao.

Uzuiaji huo unamaanisha vile serikali ya Ethiopia ilivyositisha huduma zote za umeme, kifedha na mawasiliano ya simu huko Tigray tangu kujiondoa katika mji wa Mekelle mnamo Juni.

ETH

Chanzo cha picha, AFP

Mashirika ya kimataifa pia yamekuwa na shida kupata misaada inayohitajika.

Jenerali Tsadkan Gebretensae aliambia kipindi cha Newshour cha BBC Jumapili kwamba vikosi vya Tigray vitaendelea kupigana - ikiwa ni pamoja na eneo la Afar na Amhara - hadi masharti yao ya kusitisha vita yatakapotimizwa.

"Shughuli zetu zote za kijeshi kwa wakati huu zinatawaliwa na malengo mawili makuu. Moja ni kuvunja zuio. La pili ni kulazimisha serikali kukubali masharti yetu ya kusitisha mapigano na kisha kutafuta suluhisho la kisiasa".

Jenerali huyo aliongezea kuwa Watigray hawalengi kutawala Ethiopia kisiasa kama walivyokuwa zamani.

Badala yake wanataka Watigray wapigie kura maoni ya kujitawala.

Waziri wa demokrasia wa Ethiopia, Zadig Abraha, ameiambia BBC, waasi wa Tigray walikuwa na hisia potofu ya nguvu ya madaraka na watafukuzwa kutoka kila kijiji cha eneo wakati serikali itaishiwa uvumilivu.

Bwana Zadig alikanusha madai ya waasi kwamba kulikuwa na kizuizi dhidi ya Tigray na akasema ni jukumu la serikali kuhakikisha utoaji wa misaada ya kibinadamu.

Katika ishara mzozo huo unawavutia wapiganaji zaidi, vijana wa Ethiopia walikusanyika kwenye mkutano katika mji mkuu, Addis Ababa, wiki iliyopita, kujibu mwito wa viongozi wa eneo kujiunga na mapambano dhidi ya waasi wa Tigray.

Mzozo huo umesababisha mgogoro mkubwa wa kibinadamu.

Shirika la watoto la Umoja wa Mataifa, Unicef, lilisema Ijumaa kuwa zaidi ya watoto 100,000 huko Tigray wanaweza kupata utapiamlo mwaka ujao, wakati nusu ya wanawake wajawazito na wanaonyonyesha wanaochunguzwa katika eneo hilo hawana lishe bora.

Njia zote za misaada zinazoingia Tigray zimezuiliwa isipokuwa barabara moja kutoka eneo la Afar ambapo misafara ya chakula imeshambuliwa hivi karibuni, ikiripotiwa na wanamgambo wanaounga mkono serikali.

Vikosi vya Tigray vinasema vinatarajia kulazimisha kufungua barabara mpya ya misaada kupitia Sudan kwa kushinda jeshi la Ethiopia na wanajeshi wa Amhara walioko hapo.

UN inasema watu wanaokadiriwa kuwa milioni 5.2 huko Tigray wanahitaji msaada wa kibinadamu, mapigano yaliyoenea hivi karibuni katika mkoa wa Afar yamewaacha maelfu huko wakitoroka makazi yao na wakihitaji chakula na malazi kwa dharura.

Matt Bryden, kutoka jopo la utafiti la Sahan, ana shaka kuwa suluhisho la kisiasa linaweza kupatikana katika hatua hii, haswa kati ya wahusika wakuu wawili.

"Vikosi vya Ulinzi vya Tigray vinapaswa kupima uwezekano wa mazungumzo ya kisiasa na hatari ya kupoteza mpango [wa kijeshi]. Kwa upande mwingine, Bwana Abiy haonyeshi nia au uelewa kwamba anaweza kuhitaji kushiriki katika mazungumzo ya kisiasa. Ana. .. imani isiyoweza kutetereka katika dhamira yake.

"Nina hofu tuna uwezekano wa kuona mzozo ukiendelea hadi Tigray ipewe uhuru wake au - uwezekano mdogo - hadi pande zote mbili zijikute katika mkwamo unaowaumiza", Bwana Bryden anasema.