Freeman Mbowe: Polisi Tanzania wathibitisha mwenyekiti wa Chadema amefikishwa mahakamani leo

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 2

Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania Chadema, Freeman Mbowe amepandishwa kizimbani hii leo jijini Dar es Salaam, polisi imethibitisha.

Kamanda wa polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Jumanne Muliro ameiambia BBC kuwa Mbowe amepandishwa mahakamani hii leo kwa "tuhuma mbalimbali zenye mahusiano na masuala ambayo yangeweza kuvunja amani katika nchi hii."

Kamanda Muliro ameiambia BBC kuwa tuhuma zinazomkabili Mbowe zimeainishwa katika hati ya mashtaka "ambayo nakala yake (Mbowe) anayo, kwa hiyo nisingependa kuharibu ladha halisi ya jinsi ambavyo mashtaka yaliaandaliwa na ofisi ya mashtaka."

BBC ilimpigia simu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania bwana Sylivester Mwakitalu ili kujua mashtaka rasmi aliyofunguliwa Mbowe lakini alisema kuwa yupo mkutanoni.

Awali taarifa iliyotumwa kupitia mtandao wa twitter wa Chadema inaeleza kuwa Mbowe "amefikishwa katika Mahakama ya Kisutu na amesomewa mashtaka ya ugaidi."

Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi, Mbowe "amesomewa mashtaka ya uhujumu uchumi ambayo ni kula njama na kutoa fedha kwa ajili kufadhili shughuli za ugaidi."

Alhamisi ya wiki iliyopita, msemaji wa jeshi la polisi nchini Tanzania David Misime alisema anakabiliwa na tuhuma mbalimbali ikiwemo za kupanga njama za kufanya vitendo vya kigaidi na kuua viongozi wa Serikali.

Taarifa ya Misime imesema kuwa Mbowe hakukamatwa kwa tuhuma za kupanga na kuandaa kongamano la Katiba mpya jijini Mwanza bali alifahamu tuhuma zinazomkabili .

"Mbowe alikuwa anafahamu fika kuwa tuhuma zinazomkabili zilikuwa zinachunguzwa na wakati wowote angehitajika Polisi kwa hatua za kisheria mara tu uchunguzi wake utakapokamilika. Hatua hiyo imefikiwa sasa," alisema Misime.

Mbowe 'augua kituo cha polisi'

Chadema pamoja na familia ya Mbowe wanaripoti kuwa kiongozi huyo ameamka leo Jumatatu akiwa na maumivu ya viungo pamoja na mgongo.

Binti wa Mbowe, Nicolle ameiambia BBC kuwa walionana naye leo asubuhi katika kituo cha polisi cha Oysterbay "na alikuwa analamikia maumivu ya mwili, aliomba apelekwe hospitali aonane na daktari wa mifupa...amekuwa akilala sakafuni katika kituo cha polisi na kipindi hiki kuna baridi...kwa afya yake na umri wake umeenda hali hiyo si njema kwake."

Nicolle anasema walihakikishiwa kuwa atapelekwa hospitali, "lakini alipokuwa njiani akapelekwa mahakamani na kosomewa mashtaka ya ugaidi ambayo hayana dhamana...hatukuwa na taarifa, hata mawakili hawakujua, tulipofika mahakamani alikuwa tayari kashapelekwa mahabusu gerezani ukonga."

Hata hivyo, kamanda Muliro amesema Mbowe hana tatizo; "...afya yake ni njema...kwa kifupi Freeman Aikaeli Mbowe amefikishwa mahakamani akiwa kwenye hali nzuri na alikuwa na uwezo wa kutambua mashtaka aliyokuwa akisomewa na alikuwa na uwezo wa kutembea."

Mbowe alikamtwa na wafuasi wengine wa Chadema jijini Mwanza usiku wa kuamkia Jumatano ya wiki iliyopita wakijianda kufanya kongamano la kudai katiba mpya. Wafuasi hao wengine 15 wote wameachiwa na polisi.