Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Rais Samia ataka uchunguzi ufanyike kubaini chanzo cha moto soko la Kariakoo
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa pole kwa wafanyabiashara wa soko kuu la Kariakoo kwa hasara kubwa waliyoipata kutokana na moto uliokumba soko hilo.
Rais Samia amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina kujua chanzo cha moto huo uliosababisha hasara kubwa kwenye soko.
Soko Kuu Kariakoo ni soko kubwa jijini Dar es Salaam ambalo linawakutanisha wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali ya nchi lakini pia ni kitovu cha biashara kwa nchi za Afrika Mashariki
Shughuli za wafanyabiashara wa soko kuu la Kariakoo jijini Dar es Salaam zimelazimika kusimama kwa muda baada ya sehemu ya soko hilo kuungua moto usiku wa kuamkia leo.
Kutokana na ukubwa wa eneo lililoungua bado kutaendelea kuwa na gesi ambayo haifai, hivyo wafanyabiashara hawataweza kufanya shughuli zao hadi pale watakapopewa taarifa rasmi.
Kamishna jenerali wa jeshi la zima moto na uokoaji John Masunga amesema moto umedhibitiwa kwa asilimia 100.
Amesema taarifa za moto zilipokewa katika Kituo cha zimamoto cha Ilala saa 2:40 usiku.
''Ilichukua muda mrefu kuzima moto huo kwa kuwa moto ulikuwa mkubwa sana, hakuna sehemu za kuchukulia maji na badala yake tulikuwa tukipata maji mbali, tulikuwa tukipata maji Airport, sasa umbali huo ni mkubwa sana,changamoto hiyo ilifaya kazi yetu ionekane kuwa ngumu.''
''Na tatizo la pili ni watu kuzingira eneo la tukio hali iliyosababisha magari yetu kushindwa kuingia na kutoka kwa urahisi," amsema Masunga.
Kamishna wa zima moto amesema kuwa taarifa itatolewa kwa wafanyabiashara hao kurejea kwenye shughuli zao hapo baadae.
''Kwa mujibu wa kanuni zetu kila tunapomaliza kuzima moto kinachofuata ni uchunguzi na sasa uchunguzi umeshaanza, utakapokamilika tutajua chanzo cha moto huo''. Alisema mkuu huyo wa jeshi la zimamoto.