Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Chanjo ya pasipoti: Cheti cha kidijitali cha Covid Muungano wa Ulaya na jinsi kitakavyowaathiri wasafiri
Watu wanaoishi barani Ulaya watahitajika kutumia pasipoti mbili kila wanapotaka kusafiri.
Kwanzia mwanzo wa mwezi huu, vyeti vya kidijitali vya COVID-19 (EUDCC) vimeanza kutumika, kuwawezesha raia wa muungano wa Ulaya (EU) kuusafiri kutoka nchi moja hadi nyingine.
Madhumuni ya cheti hicho ni kuruhusu usafiri ndani ya bara hilo, bila vikwazo, kwa watu wote waliopewa chanjo dhidi ya Covid-19, waliofanyiwa vipimo karibuni na kubainishwa hawana virusi na wale waliopona kutokana na ugonjwa huo.
Inajulikana kama "Pasipoti ya chanjo ya Ulaya" na inatambuliwa na nchi zote 27 wanachama wa EU na mataifa mengine kama vile Iceland, Norway na Uswizi.
"Tunataka kusaidia nchi wanachama kurejesha bila hofu uhuru wa kutembea,"alisema Rais wa Tume ya Ulaya Ursula Von der Leyen alipoanzisha mpango huo.
Hatahivyo, pendekezo la pasipoti ya chanjo lilipingwa na baadhi ya mataifa huku kukiwa na wasi wasi kwama zinaweza kutumiwa kama zana za ubaguzi.
Wakijibu hoja hiyo,Maafisa wa Tume ya Ulaya walisema kwamba wanataka kuwadhibitii raia wowote ambao kwa sababu moja au nyingine hawajapata chanjo.
EU imeonesha kwamba hatua hiyo inakusudua kuwahakikishia raia na wakazi wa muungano huo uhuru wa kutembea.
Hata hivyo, nchi kama Ujerumani na Uhispania tayari zimelegeza masharti ya usafiri kutoka nje ya EU.
Pasipoti hii inafanyaje kazi na itawaathiri vipi wasafiri?
1. EUDCC ni nini?
Hivi ndivyo vigezo vilivyozingatiwa kabla ya kuidhinisha cheti hiki cha kidijitali:
- Inatumiwa na raia wote wa Muungano wa Ulaya (EU).
- Inathibitisha chanjo au vipimo maalum vinavyobainisha mtumiaji hana Covid-19 au amepona hivi karibuni kutokana na maambukizi (ndani ya siku 180 zilizopita).
- Inatolewa kwa muundo wa kidijitali na karatasi.
- Miundo yote inajumuisha Nambari ya QR kuhakikisha uhalali wa cheti.
- Pia itakuwa na maelezo muhimu, kumanisha italinda maelezo binafsi ya mhusika.
- Itachapishwa kwa lugha rasmi au lugha za nchi zinazotoa pamoja na Kiingereza.
- Itatolewa bila malipo.
Nchi yoyote mwanachama ambayo itawaruhusu wasafiri waliochanjwa kuepuka masharti (kama ya kukaa karantini) lazima ikubali vyeti kutoka nchi zingine za EU kwa kuzingatia hali sawa na hiyo.
Muungana wa Ulaya kufikia sasa umeidhinisha chanjo za Pfizer-BioNTech, Moderna, Oxford-AstraZeneca na Johnson & Johnson, lakini chanjo ya Urusi ya Sputnik V na zile za China za Sinovac na Sinopharm bado hazijaidhinishwa.
Chanjo ya Oxford-AstraZeneca iliyotengenezwa India, inayofahamika kama Covishield,pia haijajumuishwa katika mpango wa EUDCC.
Hatua ambayo itawaathiri wasafiri wengi kutoka Asia na Afrika, chanjo hiyo iliyotengenezwa na Taasisi ya Serum ya India, imetumika kwa wingi.
Lakini mendekezo hilo linaongeza kuwa nchi wanachama zimepewa uamuzi wa kuamua ikiwa zitakubali vyeti vya chanjo vilivyoidhinishwa na Shirika la Afya Dunianu (WHO), kama ilivyofanywa chanjo Covishield.
Nchi saba za EU (Uhispania,Ujerumani, Slovenia, Ugiriki, Ireland, Austria na Estonia) - Pamoja na Iceland na Uswizi - zimeidhinisha Covishield kwa wasafiri wanaowasili, vyanzo vya Habari vimeiambia BBC Alhamisi iliyopita.
Chanjo za China ambazo zimetumiwa sana duniani (katika nchi 61 tofauti), zimeidhinishwa na WHO kwa utumizi wa dharura.
Chanjo ya Urusi ya Sputnik V bado haijapata kibali cha WHO. Licha ya hilo nchi kama Ugiriki imeijumuisha katika orodha yake ya masharti ya kuruhusiwa kuingia nchini humo.
2. Nani anaweza kupata cheti hicho?
Kamishena wa Tume ya Haki barani Ulaya, Didier Reynders, vyeti hivyo vimetolewa kwa lengo la kuhakikisha "usafiri salama na vikwazo kidogo msimu huu wa joto".
Katika tovuti yake, Tume ya Ulaya inaelezea kuwa cheti hicho lazima kitolewe kwa raia wote wa EU citizens na familia zao,bila kujali uraia wao.
Cheti hicho pia kunawajumuisha raia wa kigeni wanaoishi EU na wageni ambao wana vibali vya kusafiri katika nchi wanachama wa muungano huo.
3. Ukosoaji
Kumekuwa na pingamizi dhidi ya wazo la kubuniwa kwa "pasipoti ya chanjo", ambayo wengi wanachukulia kama ubaguzi.
Baadhi wanahoji kuwa ni watu wachache watakaoweza kusafiri bila vikwazo, huku wengine - hususan vijana, ambao sio kundi muhimu la chanjo hizo- wakiendelea kukabiliwa na masharti kama ya karantini ya lazima.
Pia kuna mashaka ya jinsi chanjo inavyomzuia mtu aliyepewa chanjo kuwa mbebaji au msambazaji wa virusi.
Ikisubiri tangazo la Muungano wa EU, WHO ilisema inafanyia kazi "mfumo wa kuaminika wa kimataifa" kwa usafiri salama na kwamba chanjo haitakuwa kigezo.
EU inasema watu waliochanjwa na wale ambao hawajachanjwa watanufaika na EUDCC kwa sababu inawajumuisha wale waliofanyiwa vipimo vya Covid-19 au waliopona kutokana na ugonjwa huo.
Kuhusu suala la kulinda maelezo binafsi, mamlaka za Ulaya zinasisitiza kwamba maelezo katika cheti hicho yatakuwa yale ya msingi, kama vile jina, siku ya kuzaliwa, siku ya kutolewa kwa cheti na maelezo muhimu kuhusu chanjo au vipimo vya Corona.
4. Itawaathiri vipi wasafiri?
Muungano wa Ulaya umekubali kwamba huu ni mchakato mgumu, kwa hivyo umeacha jukumu la kukusanya taarifa kwa nchi wanachama.
Kila nchi mwanachama pia itaamua jinsi itakavyoruhusu wasafiri kutoka nchi zinazoendelea na ambao wamefikia masharti yanayohitajika watakavyoingia nchini.
Uhipania na Ujerumani, kwa mfano zimefungua mipaka yao kwa watalii ambao wanaweza kuthibitisha wamepokea dozi ya mwisho ya chanjo angalau siku 14 kabla kuwasili katika nchi hizo.
Nchi Ujerumani chanjo pekee zitakazokubaliwa ni zile zilizoidhinishwa na mamlaka za Ulaya: Pfizer, AstraZeneca, Moderna na Janssen.
Msemaji wa Muungano wa Ulaya ameiambia BBC that, ijapokuwa kila nchi ina haki ya kuamua jinsi wasafiri wa kigeni wanaweza kuingia katika himaya yao, maeneo mengi huenda yatasubiri kubuniwa kwa vyeti ya kidijitali vya Covid 19 kutoka nchi zinazoendelea.
"Inawezekana kuwa uamuzi wa 'usawa': wakati Tume itakapojiridhisha kwamba nchi izinazoendelea zina uwezo wa kutoa vyeti vinavyofikia viwango na mifumo ya inayokubalika EU, ihuenda ikaamua kukubali vyeti hivyo,"alisema.
Hii inamanisha, kulingana na EU, kwamba vyeti kutoka nje ya bara hilo vinaweza - siku zijazo - kufikia masharti ya Cheti cha Kidijitali cha Covid kwa mataifa ya Ulaya.
Pia alipendekeza watu wafike katika balozi za nchi husika kujifahamisha masharti hayo kabla ya kuaza safari za kitalii.
Hata hivyo, raia wa Ulaya wanaoishi katika nchi zingine na ambao wapewa chanjo katika nchi hizo, wanaweza kutoa ombi la kupewa cheti cha kidijitali.
"Raia wa EU waliochanjwa katika nchi ambazo sio wanacha wa Muungano wa Ulaya wanaweza kuwasilisha ombi la kupewa [EUDCC] kwa nchi zao husika(wanachama) au walikopewa makazi," msemaji alifafanua.
"Cheti cha EUDCC kitatolewa ikiwa kuna uthibitisho wa chanjo kwa mhusika na ikiwa mifumo ya afya ya alipo inakubalika. Kwa maelezo zaidi, raia wanaweza kwenda kwa nchi wanachama wa utaifa au makazi, aliongeza.